Na Mohammed Hammie Rajab
A.K.A ni kirefu cha maneno ya kiengereza ambayo ni "Also
known as", ikiwa na maana ya 'Pia nafahamika kama', ambapo mtu akitaka
kujulikana ama kufahamika kwa jina jengine ambalo sio rasmi, huwa anatumia a.k.a
kwa kiashirio cha jina mbadala.
Jina linapokuwa rasmi mara nyingi hutumika zaidi kwenye
vitambulisho, vyeti, shuleni na hata maofisini kutokana na taratibu za kisheria
zilizowekwa na serikali, huwezi kukuta mtu anatumia a.k.a kwenye masuala yanayotaka
utaratibu.
Muziki wa Bongo Fleva umekuwa maarufu sana hapa nchi na hata
nje, umaarufu wa muziki huu pia unachagizwa na majina ya wasanii wake ambapo
tumeshuhudia wasanii wengi wakitumia
zaidi a.k.a pasipo majina yao halisi, japokuwa kuna wasanii wachache wanaotumia
majina yao.
Alli Kiba na ndugu yake Abdul, ukiacha uhalisia wa majina
yao ya kati ambapo wote wanatumia Salehe lakini utagundua fika kuwa hawakutengeneza
a.k.a ili kupata majina yao ya kisanii, badala yake wametumia majina yao rasmi.
Wengine ni Banana Zorro na ndugu yake Maunda Zoro ambao hawakutumia
muda kutengeneza a.k.a na bado wanafahamika, wapo pia wasanii ambao A.K.A zao
zinashahabiana na majina yao halisi ambao ni Bernad Paul (Ben Paul), Jaffar
Msham Ally (Jaffarai), Snura Mushi (Snura) na Ambwene Yesayah (AY) ambaye
ameunganisha jina lake na ubini wake kupata A.K.A.
Kwa majina haya kidogo unaweza kusema afadhali kwa kuwa ni
rahisi hata kuyatabiri, tofauti unaposikia jina kama Omari Faraji Nyembo halafu
ukaambiwa kuwa ndio Ommy Dimpoz, au
Ibrahim Mussa ambaye ni ROMA, unaweza usielewe kidogo.
Wapo wasanii wengine pia ambao lazima ikuchukue muda kufahamu
majina yao halisi, mfano ni Emmanuel Simwanga (Izzo B), Abdul-Aziz Abubakar
Chende (Dogo Janja), Emmanuel Elibariki (Ney Wa Mitego), na hata Khery Sameer
Rajab (Mr Blue), zaidi utaangua kicheko tu.
Hao ni wachache tu, lakini ukienda ndani zaidi utagundua
kuna wimbi kubwa la wasanii wa Bongo Fleva wanaotumia zaidi a.k.a kiasi cha kupoteza
majina yao halisi nchini tofauti na fani nyengine kama vile soka na filamu.
Tofauti kubwa iliyopo baina ya wasanii wa Bongo Flava na
waliopo kwenye fani ya soka au filamu ni uwazi wa majina yao, mfano marehemu
Steven Kanumba pamoja na kutumia a.k.a
ya the Great, lakini jina lake halisi lilikuwa likifahamika zaidi kuliko
jina lake mbadala. Wengine ni Shamsa Ford, Jackline Wolper, na Yusufu Mlela
ambao hata kama wana A.K.A lakini hazisikiki kama yalivyo majina yao halisi.
Japokuwa utakubaliana na mimi kuwa wapo baadhi ya wasanii wa
filamu nchini ambao nao wamepoteza majina yao halisi na kutumia zaidi majina
mbadala, mmoja wapo ni Elizabeth Michael (Lulu), Blandina Chagula (Johari),
Mahsein Awadhi (Dokta Cheni), Single Mtambalike (Richie), na Vincent Kigosi
ambaye anafahamika zaidi kama Ray.
Huwa najiuliza kuna tatizo gani mtu akabakia na jina lake
halisi pasipo na kuwa na A.K.A, ikibidi alitumie hilo hata katika shughuli zake
za kisanii ama fani yake?
Kwa mfano Diamond angepungua nini endapo angetumia jina lake
la Naseeb katika muziki wake, au Ibrahim Mussa ambaye ni ROMA, mbona Banana Zorro
ni msanii mkubwa na bado anafahamika sana kupitia jina lake halisi.
Nimekuwa nikifatilia sana wacheza filamu kutokea nchini
Nigeria lakini nimegundua waigizaji wachache sana wanaotumia A.K.A, lakini
waigizaji wakubwa kama Genevieve Nnaji, Rita Dominic, Omotola Jalade Ekeinde,
na Ramsey Nouah hawana majina mbadala na badala yake wanatumia sana majina yao
halisi na bado wanabamba.
Utumiaji wa majina mbadala (A.K.A) ni utashi wa mtu
mwenyewe, hauna uhusiano wowote kuwa unapotumia jina mbadala ndio utafahamika
zaidi katika jamii inayokuzunguka.
Kufahamika kwako kunatokana na ubora wa kazi unayoifanya,
naamini kuwa hata kama Lulu angetumia jina lake halisi la Elizabeth Michael
katika uigizaji bado angefahamika tu kutokana na ubora wa kazi yake, hivyo
hivyo kwa Zuwena Mohamedi (Shilole)
Niseme tu A.K.A sio ishu, ishu ni kukomaa na ubora wa kazi
unazofanya na watu watakujua kupitia ubora huo na sio A.K.A, wapo wenye A.K.A
kali na bado hawafahamiki.
Makala Hii Imeandikwa na:
Mohammed Hammie Rajab
Email: ankomo25@yahoo.com
Phone: 0719000010
PR Manager/Radio Editor
Uzikwasa/Pangani Fm Radio
P.o Box 1, Pangani
E-mail: ankomo25@yahoo.comP.o Box 1, Pangani
Phone: +255678900424
+255719000010
EmoticonEmoticon