DOZI
mwanzo mwisho! Hivyo ndivyo unavyoweza kuyaelezea mazoezi ya Azam FC ya
kujiandaa na msimu ujao, ambapo imeanza kujifua kwa staili ya aina yake
kwa wachezaji kupewa dozi mara tatu kwa siku.
Huo ni mwendelezo wa mazoezi ya Azam FC tokea ilipoanza maandalizi ya
msimu mpya Mei 28 mwaka huu, ikiwa na kikosi chenye sura mpya za
wachezaji wengi vijana wenye vipaji vya hali ya juu na baadhi wakiwa ni
wazoefu.
Mazoezi hayo ni maalumu kabisa katika kipindi hiki cha maandalizi ya
msimu ujao, ambapo Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, amepanga
kutengeneza kikosi kikali kitakachoweza kufanya makubwa katika siku za
usoni.
Kikosi hicho leo kimeshafanya mazoezi mara mbili, saa 1.00 asubuhi na
3.30 asubuhi na kitamalizia dozi ya mwisho saa 11.00 jioni ndani ya
viunga vya Azam Complex, Chamazi
Cioaba amesema faida kubwa ya kufanya mazoezi makali hivi sasa ni
kuwajenga wachezaji kwenye maeneo mbalimbali, kiufundi uwanjani, stamina
na ustahimilivu kwenye kupambana.
Baada ya kumaliza programu hiyo ya mazoezi, Azam FC itasafiri Julai
20, mwaka huu kuelekea kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ikienda
kucheza mechi tatu za kirafiki, ya kwanza ikiwa ya mwaliko dhidi ya
Mbeya City, itakayofanyika Julai 22 katika siku watakayokuwa
wakisherehekea Mbeya City Day.
Mechi nyingine za kirafiki itacheza na timu mbili zilizopanda daraja.
Njombe Mji Julai 24 mwaka huu mjini Njombe na ikimaliza ziara hiyo kwa
kukipiga na Lipuli ya Iringa Julai 26 kabla ya kurejea jijini Dar es
Salaam Julai 27.
EmoticonEmoticon