Sharjah, 15 Januari 2026
Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam H. Mwinyi, leo tarehe 15 Januari 2026, ametembelea House of Wisdom, maktaba ya kisasa iliyopo Sharjah, inayohifadhi zaidi ya vitabu 300,000 vikiwemo machapisho ya kielimu, fasihi na tafiti mbalimbali.
Maktaba hiyo ni kituo muhimu cha kimataifa katika kuhifadhi na kuwasilisha taarifa za kihistoria za watu mashuhuri kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Katika ziara hiyo, Mama Mariam alipata fursa ya kushuhudia urithi wa mashairi ya kale uliowasilishwa kwa mtindo wa kisasa unaochanganya teknolojia, ubunifu na fasihi, hali inayovutia kizazi cha sasa na kijacho kujifunza, kutafsiri na kutumia historia hiyo katika shughuli za maendeleo ya mataifa mbalimbali.
Aidha, Mama Mariam H. Mwinyi alitembelea Soko Asili la Al-Asra lililopo katikati ya mji wa Sharjah, ambako alijionea kazi mbalimbali za mikono zinazofanywa na wasanii wa ndani, wakiwemo vijana wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo.
Katika soko hilo, Mama Mariam alipata kuona ubunifu wa vijana hao katika utengenezaji wa misala, pochi za kubebea, vikombe vya kahawa vya aina mbalimbali pamoja na kazi nyengine za mikono zenye ubora, zinazotunza asili na utamaduni wa Kiemarati, na ambazo zimefanikiwa kuuzika sokoni.
Ziara hiyo inaonesha dhamira ya Mama Mariam H. Mwinyi katika kuunga mkono matumizi ya sanaa, fasihi, utamaduni na ubunifu kama nyenzo muhimu ya maendeleo na uwezeshaji wa jamii, hususan makundi maalum.



.jpeg)












EmoticonEmoticon