Mkuu wa Kitengo cha Lishe kutoka
Wizara ya Afya Asha Hassan akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
zoezi la kuwapatia matone ya Vitamin A watoto wenye umri wa miaka miwili
hadi mitano katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe.
Washiriki wa mkutano huo wakiwa
katika kazi za vikundi kupanga mikakati ya kuihamasisha jamii kuitikia
kampeni ya kuwapatia watoto matone ya Vitamin A katika ukumbi wa Malaria
Mwanakwerekwe.
Mwandishi wa habari wa Gazeti la
Zanzibar Leo Nasra Manzi akiwasilisha kazi ya kukundi chake katika
mkutano wa kuwaelimisha waandishi kuhusu matone ya Vitamin A katika
ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe.
Picha na Makame Mshenga.
…………………………….
Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar
Mkuu wa Kitengo cha Lishe kutoka
Wizara ya Afya Bi. Asha Hassan amesema Zanzibar bado ipo nyuma katika
kiwango cha Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) cha kuwapatia matone ya
Vitamn A watoto wenye umri kuanzia miaka miwili hadi miaka mitano.
Bi. Asha alieleza hayo katika
mkutano na waandishi wa habari kuhusu zoezi la kuwapatia matone ya
Vitamen A watoto wenye umri huo lililoanza tarehe 1 Juni ambalo
linategemea kumalizika mwishoni mwa mwezi huu kwa awamu ya kwanza mwaka
huu na awamu ya pili itafanyika mwezi Disemba.
Alisema Zanzibar hadi hivi sasa
imefikia asilimia 82 katika mpango huo wakati kiwango kilichowekwa na
Shirika la Afya Ulimwenguni ni asilimia 95.
Alizitaja Wilaya tatu za Mkoa
Mjini Magharibi ndizo zenye asilimia ndogo zaidi chini ya asilimia 70
wakati Wilaya ya Kati inaongoza kwa kuwa na zaidi ya asilimia 95.
Alisema Kitengo kimeanzisha
utaratibu wa kuwafuata wazazi wanaoishi mbali na vituo vya afya ili
kuwapatia watoto matone ya Vitamin A lakini baadhi ya wazazi wamekuwa
hawatoi mashirikiano.
Aliwasisitiza wazazi kufanya
juhudi kuhakikisha watoto wao wanapata matone hayo kwa vile ni muhimu
katika kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya maambukizo ya maradhi ikiwemo
kuharisha na kutoona vizuri.
Afisa Kitengo cha Lishe Wilaya ya
Mjini Fatma Ali Saidi alisema kumekuwa na dhana potofu kwa wananchi
hasa wanaoishi mjini kwamba watoto wao hawahitaji matone ya Vitamin A
kwa vile wanakula vizuri lakini dhana hiyo sio sahihi.
Alisema utafiti uliofanywa na
Kitengo hicho unaonyesha kwamba watoto wenye hali nzuri ya Vitamin A
Zanzibar ni asilimia 12 na asilimia 88 iliyobaki wanaupungufu.
Aliwatoa wasi wasi wazazi kuwa
hata wale wachache wenye Vitamin A vya kutosha mwilini wanapopewa matone
hayo hayana madhara yoyote na wanaweza kutumia.
Washiriki wa mkutano huo
walikishauri Kitengo cha Lishe kuongeza kutoa elimu kwa wazazi kwani
baadhi yao bado hawajaelewa umuhimu wa matone ya Vitamin A na wengine
wanadhani kuwa matone hayo ni sawa na chanjo jambo ambalo sio
sahihi.
EmoticonEmoticon