MANISPAA YA UBUNGO YAINGIA MIKATABA KAZI YA BILIONI NNE

June 10, 2017
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo (Kulia) akikabidhi mikataba ya Wazabuni, Mwingine ni Mstahiki Meya Manispaa ya Ubungo Me Boniface Jacob (Katikati)
Zoezi la utiliaji saini Mikataba kazi za Manispaa ya Ubungo likiongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo (Kulia) na Mstahiki Meya Manispaa ya Ubungo Me Boniface Jacob (Katikati)
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo (mwenye maiki?) Akizungumza wakati wa kusaini mikataba kazi, Mwingine ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob na Naibu Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Ramadhan Kwangaya
Zoezi la utiliaji saini Mikataba kazi za Manispaa ya Ubungo likiongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo (Kulia) na Mstahiki Meya Manispaa ya Ubungo Me Boniface Jacob (Katikati)
Jana June 10, 2017 Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo amesaini mikataba ya kazi mbali mbali na makampuni ya Ujenzi, Barabara na Wazabuni 29.
Mikataba hiyo imesainiwa mbele ya waandishi wa habari katika dhifa iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano uliopo Mtaa wa Kibamba CCM, Jijini Dar es salaam.
Katika dhifa hiyo iliyohudhuriwa pia na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob jumla ya mikataba 29 ilisainiwa na wakurugenzi wa makampuni mbalimbali ambapo kati ya makampuni hayo, Makampuni 14 yamepewa kazi za Billioni 3.2 kwa kazi ya kusafisha barabara na mazingira yote ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ili kuifanya Halmashauri ya Ubungo kuwa katika Hali ya usafi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa tukio hilo la kusaini mikataba Mkurugenzi Kayombo alisema kuwa mikataba kazi hiyo ipo katika makundi matatu ambayo ni miradi ya Maji, Barabara na usafi.
‘’Nawasihi wazabuni wote ambao mtasaini mikataba kazi hapa leo  mkatekeleze yale yaliyo katika mikataba yenu ya kazi mimi kama Mkurugenzi sitasita kufuata kanuni na taratibu za kisheria na kuwachukulia hatua wale wote watakaoshindwa kufuata yale ambayo yako katika mikataba yenu’’ . Alisema Kayombo
MD Kayombo alisema kuwa katika nakubaliano hayo jumla ya Shillingi Millioni 400 zimesainiwa kwa ajili ya uchongaji wa barabara za Mitaa mbalimbali ya Halmashauri na Shilingi Millioni 200 Ni kwa ajili ya Miradi ya upelekaji wa maji katika kata za Mbezi na Mabibo.
Alieleza kuwa Kiasi kingine cha shillingi Millioni 200 ni kwa ajili ya Ukarabati mfumo wa maji Hospitali ya Sinza na ujenzi wa madarasa ya shule ya Sekondari ya Matosa sambamba na Nyumba sita za walimu zilizopo Kata ya GOBA.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob alisema kuwa Manispaa ya Ubungo imeingia katika historia kwa kusaini mikataba kazi hiyo na historia hiyo inatokana na umahiri wa Watumishi wa Manispaa hiyo katika Kusimamia Ukusanyaji wa Mapato na kubana Matumizi ya ruzuku zinazotoka Serikali kuu.
“Manispaa yetu ina miezi nane tu na tayari leo tunasaini mikataba kazi ambayo italipwa kwa fedha zetu za ndani hili ni jambo la kujivunia sana ‘na baada ya miezi michache tutasaini tena mikataba kazi mingine na kwa hii mikataba tunayosaini hapa leo tayari fedha zake zipo kwenye akaunti kwa hiyo ni suala la utekelezaji tu Alisema Jacob.
Alisema kuwa  anaamini wote wanaosaini Mikataba hiyo hakuna hata mmoja aliyepenyeza Rushwa au Hongo yoyote na ndio maana mikataba hiyo imesainiwa kwa Uwazi na Ukweli na hakuna hata siku moja Manispaa ya Ubungo itasaini Mikataba kwa kujificga au kwenye giza alisisitiza Mstahiki Boniface Jacob.
Miongoni mwa mikataba kazi ambayo imesainiwa ni Ukarabati wa Mradi wa Maji  Goba, Ukamilishaji wa ujenzi wa madarasa na vyoo shule ya Sekondari Luguluni katika kata ya Kwembe, Ukamilishaji wa Ujenzi wa Madarasa ya shule ya Sekondari Matosa.
Pia ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba za walimu (6 in 1) katika Sekondari ya Matosa, Matengenezo ya Barabara ya Watani Makaburini (Makurumla), ujenzi na ukarabati wa mfumo wa maji katika hospitali ya Sinza, Ujenzi wa kivuko cha Mabibo katika Manispaa ya Ubungo, kutoboa na kuweka maji katika Barabara ya Sam Mujoma na Mandela Manispaa ya Ubungo, Mradi wa maji Mbezi Luiz na Ukarabati wa mradi wa Maji Mabibo Jeshini, Mabibo na Kawawa.
Akizungumza kwa niaba ya wazabuni wenzake,  mzabuni wa Kampuni ya  Singaruki Investment Ltd alisema kuwa kampuni zote zilizopata kazi katika Manispaa ya Ubungo ni dhahiri kuwa zilistahili kutokana na ufanisi katika utendaji kazi.
Alisema tayari wameshasaini mkataba kazi hivyo jambo la msingi ni kutekeleza yale yote yaliyopo katika mikataba kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za kisheria ambazo zimeainishwa kwenye Mikataba.
Aidha Mkurugenzi Kayombo ametoa siku 14 kwa wakandarasi wote kuhakikisha wanarudisha mikataba ya makubaliano mara baada ya kuisoma na kuielewa sambamba na kujaza mikataba hiyo.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA HABARI NA UHUSIANO
HALMASHAURI YA MANISPAA YA UBUNGO

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »