Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Mh. Prof: Makame Mbarawa akiongea na wadau wa sekta ya
usafirishaji kabla ya zoezi la utiaji saini wa mkataba wa upanuzi na
uongezaji wa kina cha Bandari kati ya Serikali na Kampuni ya China
Harbour Engineering. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania (TPA) Mhandisi Deusdedit
Kakoko na kushoto ni Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya
Bandari Bw. Mkinga Mkinga. (Picha na Benjamin Sawe- Maelezo).
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Mh. Prof: Makame Mbarawa (katikati) akishuhudia makabidhiano
ya mkataba wa upanuzi na uongezaji wa kina cha Bandari kati ya Serikali
na Kampuni ya China Harbour Engineering. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania (TPA). Mhandisi Deusdedit Kakoko na kushoto ni Mtedaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. XU XINPEI. (Picha na Benjamin Sawe- Maelezo).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania (TPA). Mhandisi Deusdedit Kakoko kulia na Mtedaji Mkuu wa Kampuni ya China Harbour Engineering Bw. XU XINPEI
wakionyesha mkataba wa makubaliano ya upanuzi na uongezaji wa kina cha
Bandari kwa wadau wa sekta ya usafirishaji baada zoezi la utiaji saini
wa mkataba huo kukamilika. (Picha na Benjamin Sawe- Maelezo).
………………………………………………………………..
Benjamin Sawe-Maelezo
Mamlaka ya Bandari nchini (TPA),
imesaini mkataba wa upanuzi na uongezaji wa kina cha bandari
utakaowezesha bandari ya Dar es Salaam kupokea meli kubwa za mizigo na
kushindana na bandari nyingine katika pwani ya bahari ya hindi.
Upanuzi huo utakaofanywa na
kampuni ya China Harbor Construction ya China utagharimu kiasi cha
shilingi bilioni 336 na utadumu kwa miezi 36, ambapo utahusisha
uongezaji wa kina cha lango la bandari na uongezaji wa kina cha maji
kati ya gati namba 0, 1 hadi 7.
Akizungumza katika hafla ya
utiaji saini mkataba huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.
Makame Mbarawa amesema hatua hiyo inalenga kuifufua upya bandari ya Dar
es Salaam ili ifanye kazi kwa ushindani na kuhudumia wateja wengi
kuliko ilivyo sasa.
“ Kukamilika kwa upanuzi na
uongezaji wa kina cha maji katika gati namba 1 hadi 7 kutoka mita 8
hadi 15 kutawezesha meli kubwa na za kisasa zenye uwezo wa kubeba hadi
makontena elfu kumi na tisa kutia nanga katika bandari ya Dar es Salaam
na kuongeza ufanisi na kukuza uchumi wa Tanzania”, amesema Prof.
Mbarawa.
Aidha Prof. Mbarawa amesisitiza
kuwa pamoja na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam Serikali inaendelea
na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya reli na barabara ili kuhakikisha
mizigo haikai muda mrefu bandarini.
“Ujenzi wa reli ya kisasa ya
Standard Gauge toka Dare s Salaam hadi Kanda ya Ziwa na Kigoma na
ufufuaji wa reli ya Tazara kutawezesha bandari ya Dar e s Salaam kufanya
kazi kwa ufanisi na kuvutia wafanyabiashara wengi hivyo nawataka
wafanyakazi wote wa bandari kufanyakazi kwa bidii na uadilifu”,
amesisitiza Prof. Mbarawa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng.
Deusdedit Kakoko amesema kiasi cha dola za Marekani milioni 421,
kitapatikana kwaajili ya ujenzi huo ambapo kati ya fedha hizo Benki ya
Dunia itatoa mkopo wa masharti nafuu wa dola milioni 345.
Kukamilika kwa ujenzi huo
kutaondoa adha ya baadhi ya meli kusubiri kwa muda mrefu kupata nafasi
ya kutia nanga na kutaongeza hadhi ya bandari ya Dar es salaam na
kuvutia wasafirishaji wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
EmoticonEmoticon