Kamishna
wa Madini Tanzania Mhandisi Benjamini Mchwampaka akizungumza jambo wakati wa
Kufunga Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito ya Arusha.
Na
Asteria Muhozya, Arusha
Wadau wa Madini
nchini wametakiwa kujikita katika shughuli za ukataji na usanifu wa madini
badala ya kusanifiwa nje ya nchi ili kuwezesha adhma ya Serikali ya Tanzania ya Viwanda
kupitia Sekta ya Madini.
Hayo yalisemwa na Kamishna
wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamini
Mchwampaka wakati wa kufunga Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito
yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 3-5 Mei,2017.
Aliongeza kuwa, uwepo
wa shughuli za ukataji na unga'rishaji wa madini hayo nchini kutawezesha
kuyaongezea thamani ikiwemo kupanua wigo wa ajira kupitia sekta ya madini.
" Tanzania ya
sasa ni ya Viwanda. Na sisi sekta ya madini tuwe na viwanda vyetu vya kusanifu madini yetu hapa hapa nchini.
Kwanza tutayaongezea thamani madini yetu lakini pia tutazalisha ajira kwa
wingi," alisema Mchampaka.
Aidha, Kamishna Mchwampaka
aliongeza kuwa, tayari Wizara ya Nishati na Madini imewasiliana na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya
biashara ya Madini nchini ili kuondoa kero ambazo ni kikwazo katika biashara hiyo kwa watanzania.
"Tunataka kuweka
mazingira mazuri zaidi kwa wafanyabiashara wa madini wa Tanzania lakini pia
tunapenda wafanyabiashara wetu washiriki kwa wingi katika maonesho haya. Ni
fursa kubwa ya kibiashara kwao," alisisitiza Mchwampaka.
Akizungumzia Mnada wa
Madini ya Tanzanite uliofanyika tarehe 5 , Mei, alisema kuwa, minada
hiyo itaendelea kufanywa mara kwa
mara kutokana na mchango wake katika sekta husika kwa kuwa pia inasaidia kupata
bei halisi ya madini hayo.
Katika mnada wa
Madini ya Tanzanite jumla ya kampuni 48 zilishiriki mnada huo ambapo madini
ghafi ya Tanzanite kutoka Kampuni ya
TanzaniteOne yenye jumla ya gramu 691,060.33 ziliuzwa katika mnada huo kwa
dola za Marekani 3,161,860, sawa na
asilimia 100 ya madini yote yaliyowasilishwa kwa mauzo.
Pia, alizungumzia
ujumbe wa Serikali ya Nigeria iliyoshiriki Maonesho hayo na kueleza kuwa,
ujumbe huo ulifika kwa lengo la kujifunza namna Tanzania inavyoongeza thamani
madini yake ikiwemo pia kubadilisha uzoefu na kuongeza kuwa, lengo ni kuifanya
Afrika inufaike na rasilimali zake za madini.
Ujumbe wa Serikali ya
Nigeria uliongozwa na Waziri wa Madini
na Maendeleo ya Viwanda, Abubakar
Bwari aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Abbas Mohamed pamoja na
ujumbe wa wafanyabiashara wa Madini kutoka nchini humo.
EmoticonEmoticon