TUTAKUWA WAKALI -DKT.AKWILAPO

January 16, 2026


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amesema watakuwa wakali kwa watumishi watakaokiuka taratibu za utendaji na kusababisha migogoro ya ardhi.

Dkt. Akwilapo ametoa kauli hiyo leo tarehe 16 Januari, 2026 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii wakati wa kikao cha Wizara ya Ardhi na Kamati kilichokuwa na lengo la kuifahamu wizara ya ardhi na taasisi zake.

"Niihadi kamati, wizara yangu haiko tayari kuzalisha migogoro mipya na tunaona aibu kuongoza taasisi yenye migogoro" amesema Dkt. Akwilapo.


Amesema,  katika kutekeleza majukumu yake, wizara ya Ardhi itahakikisha inazingatia sheria, kanuni na taratibu ili  kupunguza migogoro ya ardhi iliyopo na kutokuzalisha migogoro ya ardhi mipya nchini.

"Tunona aibu migogoro ya ardhi kupelekwa  kwa Wakuu wa Wilaya wakati wizara inayohusika na masuala ya ardhi ipo" amesema.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya amewaambia wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii kuwa, Wizara ya Ardhi haina uhusiano na migogoro ya ardhi bali yapo malalamiko yanayohusiana na masuala ya ardhi.

Ameomba ushirikiano na wajumbe wa kamati katika kushughulikia migogoro ya ardhi huku akisisitizia wizara y ardhi kusimamia watumishi wa sekta ya ardhi kuwa na maadili sambamba na kutenda haki wakati wa kutekeleza majukumu yao.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utali Mhe. Timotheo Mnzava ameeleza kuwa, pamoja na kazi kubwa inayofanya wizara ya Ardhi katika kushughulikia migogoro ya ardhi lakini bado wizara ina jukumu la kuongeza nguvu katika kushugulikia migogoro ya ardhi nchini.


Aidha, Kamati hiyo imeelekeza Wizara kuona namna bora ya kutumia ardhi kwa kujenga majengo yanayoendana na mahitaji ya sasa na baadae kwa kuzingatia kasi ya ongezeko la watu wakati ardhi haiongezeki inabakia ni ileile.


Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja ametaka sheria na kanuni zifuatwe wakati wa kushughulika na watumishi wanaokiuka taratibu na kusababisha   migogoro ya ardhi.


"Hili suala la watumishi tujitahidi kusimamia sheria vizuri tunahurumiana sana, tufikirie kwenye sheria why mtumishi amegawa viwanja mara mbili , tukisimamia tutafanikiwa" amesema


Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia taasisi zake za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), vyuo vya Ardhi Morogoro (ARIMO) na Tabora (ARITA), Bodi ya Usimamizi wa Wapima, Bodi ya Usajili wa Wathamini pamoja na Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipangomiji imeelezea Muundo, majukumu, mafanikio na mipango ya taasisi zake mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii.


Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »