Na Jumia Travel Tanzania
Kama biashara zingine, kuna msimu pia wateja hukauka mahotelini na wanakuwa ni wa kuhesabika tu. Kwa kawaida biashara ya hoteli huwa ni ya msimu yaani kipindi ambacho kunakuwa na sikukuu au mapumziko ndicho watu hufurika. Na hii ni kwa sababu kwamba wasafiri wengi huwa ni watalii ukilinganisha na wafanyabiashara.
Kipindi hiki ndicho wamiliki/mameneja wa hoteli hutakiwa kuwa wabunifu zaidi ili kuhakikisha kuwa wanawavutia wateja. Zipo mbinu kadhaa ambazo Jumia Travel ingependa kukushirikisha hizi chache ili kukabiliana na kipindi hiko kikifika ukiwa umejiandaa:
Zitambue tabia za wateja wako. Kitu cha kwanza kabisa kukizingatia ni kujua tabia za wateja wanaopenda kutembelea hotelini kwako. Tumia taarifa ulizonazo kwenye kumbukumbu yako kuangalia wengi ni wa aina gani, vipindi wapendeleavyo kutembelea na huvutiwa na huduma zipi zaidi. Kwa mfano, meneja wa hoteli ya Kendwa Rocks anaweza kulitumia tukio la ‘Full Moon Party’ kujifunza hadhira inayofika pale na namna ya kuwavutia tena endapo tukio hilo halitokuwepo.
Buni na toa ofa maalum za kuvutia. Baada ya kutambua ni wateja wa aina gani hupenda kutembelea zaidi hoteli yako, unaweza kubuni ofa maalum kuwalenga wao. Kwa kawaida kuna watu wanapenda kwenda kupumzika hotelini kipindi wateja wanakuwa sio wengi sana kwa sababu ya utulivu na gharama kushuka. Kama meneja wa hoteli unaweza kuitumia fursa hii kubuni ofa zitakazowavutia wateja wa aina hii. Itumie orodha ya wateja ambao wanaipendelea hoteli yako mara kwa mara kuwajulisha juu ya ofa hizo. Kwa sababu huwezi kujua kama wasipokuja wao wanaweza kuzipendekeza kwa marafiki, ndugu na jamaa zao.
Chunguza matukio yanayotarajia kutukia eneo ulilopo. Kipindi cha msimu ambao wateja sio wengi ni vema kutafiti shughuli ambazo zitawavutia watu kutembelea hotelini kwako. Unaweza kujua matukio yanayoendelea eneo ulilopo kupitia njia mbalimbali kama vile tovuti zinazoweka mtangazo nakadhalika. Ukishafahamu hayo jaribu kuwasiliana na waandaji ili ujue unaweza kushiriki kwa namna gani. Unaweza kushiriki kama washiriki wengine ili kuitangaza hoteli yako au kama mdhamini pengine hata kwa kutoa fursa kwa tukio hilo kufanyika hotelini kwako. Unaweza kuona kama ni gharama kufanya hivi lakini kuna faida nyingi kwani hoteli itajulikana kupitia matangazo, wahudhuriaji na pia huduma zako kutumika wakati wa tukio.
Boresha mwonekano na taarifa kwenye tovuti ya hoteli. Lakini pia kipindi ambacho pilikapilika za wateja zinakuwa sio nyingi sana hotelini, unaweza kukitumia kwa kuboresha mwonekano na taarifa mbalimbali kwenye tovuti. Kwa mfano, huduma, picha, matukio na habari unazoona zinafaa kwa wateja wako kuzifahamu.
Tumia fursa ya wateja wanaoependa kutembelea hotelini kwako. Kama ulikuwa haufahamu wateja wanaweza kutumika kama njia mojawapo ya kujitangaza na kuvutia wengine wapya. Mara nyingi watu huamini na kushawishika kiurahisi kutokana na maneno wanayoambiwa na watu wao wa karibu. Kwa kutumia orodha uliyonayo unaweza kuwaomba kuwataarifu wenzao na kisha kuwapatia ofa hotelini kwako kama chachu.
Tumia barua pepe kuwafikia wateja wako. Makampuni mbalimbali hutumia mbinu hii pia ambapo huwa na kumbukumbu ya anuani za wateja wao. Nadhani hata wewe utakuwa ushawahi kupokea jumbe za namna hiyo zikikutaka kutumia huduma fulani. Kwa hiyo baada ya kuandaa ofa zako kadhaa unaweza kuzituma kwa wale wateja ambao unajua huwa wanakuja hotelini kwako mara kwa mara.
Tumia mitandao ya kijamii kuongeza hamasa ya ofa na kampeni zako. Kwa sasa, hakuna njia rahisi na ya haraka zaidi inayowafikia na kuwaunganisha wateja wengi na makampuni kama mitandao ya kijamii. Hakikisha unaitumia vema mitandao hiyo kujenga na kueneza hamasa kwa kile unachotaka kukifanikisha. Watu wengi siku hizi wanatumia zaidi mitandao hiyo kwa kuwasiliana pamoja na kupata taarifa mbalimbali.
Zipo njia tofauti ambazo mahoteli huzitumia katika kukabiliana na kipindi hiki ikiwemo kukitumia kufanya maboresho. Kikubwa ni kutokukubalina na hali ya kwamba msimu huu huwa hakuna wateja au kushusha gharama ili kuwavutia wengi zaidi. Mbinu hizo hapo juu zilizoorodheshwa na Jumia Travel endapo zikizitumika ipasavyo basi hutoona tofauti ya misimu ya wateja kufurika hotelini kwako.
EmoticonEmoticon