Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepanda miti 3850 nchi nzima ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake huku Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Yusuph Juma Mwenda ikiutaka umma kuitunza miti hiyo kwa lengo la kuhifadhi mazingira.
Akizungumza wakati wa tukio la upandaji wa miti katika Shule ya Msingi Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam Juni 28, 2026, Kamishna Mkuu wa TRA amesema lengo la upandaji miti hiyo ni kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari na kuwafundisha kwa vitendo wanafunzi umuhimu wa kulipa kodi.
Amesema pamoja na kuhamasisha ulipaji wa kodi pia wanafunzi watapata faida ya matunda, hewa safi na kivuli.
" Walipakodi wamechangia kiasi kikubwa katika kuliletea maendeleo Taifa, miti hii ni alama kwa wanafunzi kuwa wazazi wao wanalipa kodi hivyo nao kubakia na ujumbe huko mbele watakuja kuwa walipa kodi, ni muhimu sote kutambua ulipaji wa kodi ni jukumu la kila mmoja",amesema Mwenda.
Aidha akitoa ujumbe kwa uongozi wa Shule ya Msingi Mnazi mmoja ambapo TRA imepanda miti 30 ya matunda, Mwenda amesisitiza kuwa ni vyema ikatumzwa na kulindwa huku akitoa ahadi ya kugharamia ikiwa ni pamoja na kuwapa motisha wanafunzi watakaopewa jukumu la kuitunza kwa mudabwa mwaka mzima.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mnazi Mmoja mbali na kuishukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kujitolea kupanda miti hiyo kama moja ya njia ya utunzaji wa mazingira, amesema wamepokea tukio hilo la upandaji miti kwa upendo mkubwa huku wakiahidi kuitunza.
Aidha pamoja na hilo Mwalimu Mkuu huyo amemuomba Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Juma Mwenda kusaidia upatikanaji wa kisima shuleni hapo pamoja na kompyuta kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kitaaluma ombi lililopokelewa na Kamishna huyo akiahidi kulitekeleza kuanzia Jumatatu.


EmoticonEmoticon