Na Oscar Assenga, Muheza
MWENGE wa Uhuru 2026 unatarajiwa kuingia Wilaya ya Muheza kesho saa 4:00 asubuhi na kukimbizwa kupitia miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.5, huku viongozi wa wilaya wakitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo.
Mwenge huo utapokewa katika eneo la Kilapura, Kijiji cha Muungano, Kata ya Mlingano na utapitia miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wa wilaya hiyo.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya ujio wa Mwenge huo, Mkuu wa wilaya ya Muheza Ayoub Sebabili alisema kati ya miradi saba itakayopitiwa, miwili itazinduliwa rasmi, miwili itawekewa mawe ya msingi na mitatu itatembelewa na kukaguliwa.
Alisema mradi wa kwanza ni Zahanati ya Muungano, ikifuatiwa na mradi wa maji wa Kijiji cha Magoda unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Pia Mwenge wa Uhuru utazindua mabweni ya Shule ya Sekondari Mangenya pamoja na kuweka jiwe la msingi katika darasa jipya linalojengwa kwa ajili ya maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2027.
Mbali na miradi hiyo, viongozi wa mbio za Mwenge watatembelea Klabu ya Wapinga Rushwa ya wanafunzi ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha maadili mema na mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa katika jamii.
Katika kuunga mkono juhudi za serikali za matumizi ya nishati safi, Mwenge wa Uhuru pia utashuhudia utoaji wa mitungi ya gesi kwa wananchi ili kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala na kulinda mazingira.
Ratiba hiyo itahusisha pia uzinduzi wa boksi kalavati katika Kijiji cha Tongwe, Kata ya Tongwe, kabla ya kutembelea kikundi cha vijana wa Kijiji cha Magila, Kata ya Genge, waliopata mkopo wa asilimia 10 kutoka mapato ya halmashauri kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Aidha, Mwenge huo utafungua rasmi Hoteli ya Harvest Inn, mradi wa uwekezaji wa mwananchi wenye thamani ya Sh milioni 950, unaotarajiwa kuongeza fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii na huduma wilayani Muheza.
Baada ya shughuli za miradi kukamilika, mbio za Mwenge wa Uhuru zitahitimishwa katika viwanja vya Mkesha Jitegemee, ambapo kutafanyika maonesho mbalimbali ya utalii, biashara za wajasiriamali, burudani kutoka kwa wasanii wa ndani na nje ya wilaya pamoja na maonesho ya vipaji vya vijana.
Vilevile, wananchi watapata fursa ya kupatiwa elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, matumizi ya dawa za kulevya, maambukizi ya UKIMWI, malaria na masuala mengine ya kijamii yanayogusa maendeleo ya taifa.
Wananchi wa Muheza wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo za Mwenge wa Uhuru, zinazobeba kaulimbiu ya kuhamasisha uzalendo, uwajibikaji na maendeleo ya wananchi.
EmoticonEmoticon