Rais
Mhe. Dkt. Magufuli na Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga wakiwa katika
picha ya pamoja na Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Magufuli akutana na Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli amewashukuru Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa
kwa ushirikiano na mchango wao kwa Serikali ya Tanzania ambao umesaidia
kufikia malengo ya Serikali kwa mwaka uliopita wa 2016. Rais Magufuli
aliwasihi Waheshimiwa Mabalozi waendelee kuisaidia Serikali ili kufikia
malengo iliyojiwekea kwa mwaka 2017.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa shukrani hizo leo wakati wa hafla ya kuukaribisha
mwaka mpya (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam
kati yake, Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo
nchini.
Katika
hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli alisema kuwa mwaka 2016 ambao ulikuwa
mwaka wake wa kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais wa Awamu ya Tano umekuwa
wa mafanikio makubwa ambapo nchi imendelea kudumisha amani, mshikamano,
umoja na Muungano umeimarika. Aidha katika mwaka huo, Serikali
imeongeza jitihada za kuimarisha demokrasia, kupiga vita rushwa,
ujangili na ufisadi.
Mhe.
Rais Magufuli aliongeza kusema kuwa, Serikali ya Tanzania imefanikiwa
kiuchumi na kuwa nchi ya pili yenye uchumi unaokua kwa kasi barani
Afrika ikitanguliwa na Ivory Coast. Uchumi wa Tanzania ulitarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka jana kutoka asilimia 7.0 mwaka uliotangulia.
Pia kiwango cha mfumuko wa bei kilipungua kutoka asilimia 6.5 mwezi
Januari 2016 hadi kufikia asilimia 2.5 mwezi Oktoba mwaka huohuo.
Akizungumzia
suala la ukusanyaji mapato, Mhe. Rais Magufuli alisema kwamba Serikali
inasimamia kikamilifu suala hilo ambapo kwa sasa kiwango cha ukusanyaji
wa mapato kimeongezeka kutoka shilingi bilioni 850 hadi kufikia
shilingi trilioni 1.2 kwa mwezi.
Kuhusu
mpango wa maendeleo wa miaka mitano 2016/2021, Rais Magufuli aliwaeleza
Mabalozi hao kuwa, mpango huu unalenga kujenga Uchumi wa Viwanda ili
kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kama
Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyoelekeza.
Alieleza
kuwa katika kutekeleza Mpango huo kiasi cha shilingi Trilioni 107
kinahitajika na kati ya hizo Serikali itatoa shilingi trilioni 59
ambazo ni wastani wa shilingi trilioni 11.8 kila mwaka kwa kipindi cha
miaka mitano ijayo. Utekelezaji wa mpango huo umeshaanza ambapo Serikali
katika Bajeti yake ya mwaka 2016 imetenga kiasi cha shilingi trilioni
29.5 ambazo ni sawa na asilimia 40 ya Bajeti ya Serikali kwa ajili ya
Bajeti ya Maendeleo. Kiwango hicho ni cha juu zaidi kuwahi kutengwa
kwenye bajeti ya maendeleo katika historia ya Tanzania.
Fedha
hizo zimeelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya
uwekezaji wa viwanda kama vile nishati, barabara, reli na maji.
Aliongeza kusema kuwa Kati ya fedha hizo shilingi trilioni 5.5
zimetengwa kwa ajili ya miundombinu ya usafirishaji na shilingi trilioni
1.2 zimetengwa kwa ajili ya nishati ya umeme. “Hii
imetuwezesha kuendelea au kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa ya
usafiri ikiwemo reli, barabara, anga, maji pamoja na miradi ya umeme.
Tuliweza pia kununua ndege mpya sita ambazo bila shaka zitasaidia kukuza
sekta ya utalii nchini”
Kwa
muktadha huo, Rais Magufuli aliwaomba Mabalozi kushawishi wawekezaji
kuja kuwekeza katika ujenzi wa Reli wa kiwango cha kimataifa kutoka Dar
Es Salaam hadi Mwanza na Kigoma na kuunganisha hadi nchi za Burundi, DRC
na Rwanda. Serikali kwa kutumia fedha zake za ndani itaanza kujenga
kilomita 300 kuanzia Dar Es Salaam hadi Morogoro.
Vile
vile, Serikali imeweka kipaumbele kwenye kuboresha huduma za jamii
ikiwemo sekta ya elimu iliyotengewa trilioni 4.8 na sekta ya afya kiasi
cha trilioni 1.9. Kupitia mpango huu wa kuboresha sekta ya elimu,
kiwango cha udahili kwa watoto wanaojiunga na darasa la kwanza na kidato
cha kwanza na wale wanaopokea ufadhili wa masomo ya juu kimeongezeka
mara dufu ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Akizungumzia
masuala ya Diplomasia, Mhe. Rais Magufuli aliwaeleza Mabalozi na
Wawakilishi hao wa Mashirika ya Kimatifa kuwa mahusiano ya kidiplomasia
kati ya Tanzania na nchi ningine yameimarika ambapo Viongozi Wakuu
kutoka nchi mbalimbali wamefanya ziara nchini Tanzania. Aidha, yeye
binafsi, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Viongozi wengine Serikalini
wamefanya ziara za kuimarisha ushirikiano kwenye nchi mbalimbali. Katika
ziara hizo, Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya ushirikiano. Mhe.
Rais aliahidi kuwa Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu kwenye
Mashirika ya Kimataifa na Kikanda ikiwemo Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa
Mataifa (UN), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika Mashariki na
mengine.
“Tunawashukuru
sana Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda kwa
kazi nzuri mnayoifanya hapa nchini kwetu. Mafanikio yote haya
niliyoainisha yamewezeshwa na ushirikiano wenu na naahidi Serikali
itaendelea kutoa ushirikiano kwenu ili muweze kufanya kazi zenu vizuri”
alisema Rais Magufuli.
Vilevile
aliwaomba Mabalozi hao kuendelea kushirikiana na Tanzania ili
kuiwezesha kufikia malengo yake na aliwakaribisha wawekezaji kuja
kuwekeza nchini na kutumia fursa za malighafi, nguvukazi na soko kubwa
lililopo nchini.
Halikadhalika,
Mhe. Rais Magufuli alianisha changamoto zinazochangia kukwamisha
jitihada mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na Mabadiliko ya
Tabianchi na kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana katika
kukabiliana na changamoto hii ili kuziwezesha jamii zetu kufikia
maendeleo na ustawi. Pia kupitia Mabalozi hao alizipongeza nchi
zilizoridhia Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na kueleza
kuwa Tanzania imeanza mchakato wa kuridhia Mkataba huo tangu mwezi
Aprili, 2016.
Katika
hatua nyingine, Mhe. Rais aliwaeleza rasmi Mabalozi hao azma ya
Serikali ya kuhamishia Makao Makuu mjini Dodoma katika kipindi cha miaka
mitano ya utawala wake na kuwaomba Mabalozi hao nao waanze mchakato wa
kuhamia Dodoma.
“Mwaka
jana wakati nakabidhiwa uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi niliahidi
ndani ya miaka mitano Serikali itahamia Dodoma. Tayari Waziri Mkuu na
baadhi ya Wizara zipo Dodoma. Nawaomba Mabalozi nanyi muanze kufikiria
kuhamia Dodoma kwani Serikali imekwishatenga viwanja kwa ajili yenu,
alisisitiza Rais Magufuli.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkuu wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Zimbabwe
hapa nchini, Mhe. Edzai Chimonyo alisema kuwa anaipongeza Serikali ya
Tanzania chini ya uongozi wa Rais Magufuli kwa hatua kubwa ya maendeleo
iliyopiga katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wake. Alisema kuwa
katika kipindi hiki wameshuhudia uchumi ukikua, nidhamu katika utumishi
wa umma, ukusanyaji wa mapato kuongezeka, na kiwango cha mfumuko wa bei
kupungua.
Aidha,
aliongeza kuwa wanaunga mkono mpango wa Serikali wa kujenga miundombinu
wezeshi ikiwemo Reli kwa vile kutawezesha kukuza biashara na nchi
jirani na mataifa mengine kwa ujumla. Pia alipongeza jitihada za
Serikali katika kukuza ushirikiano na Sekta Binafsi ambayo ina mchango
mkubwa kwenye maendeleo na kupongeza juhudi za Tanzania kwenye
usuluhishi wa migogoro kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu na kuitaja Tanzania
kuwa ni Kisiwa cha Amani.
Kuhusu
Mabalozi kuhamia Dodoma, Balozi Chimonyo alisema Jumuiya ya Mabalozi
inaunga mkono wazo hilo na wapo tayari kuhamia Dodoma kama ilivyopangwa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 10 Februari, 2017
|
EmoticonEmoticon