Na mwandishi wetu.
Mahakama Kuu ya Uhujumu Uchumi, Divisheni ya Makosa ya Rushwa, imemhukumu kifungo cha miaka 28 jela mshtakiwa Isso Lomward Lupembe, baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki katika kusafirisha dawa za kulevya kiasi cha kilogramu 268.50 aina ya heroin. Mshtakiwa huyo alikuwa mshtakiwa wa kwanza kati ya watatu waliokuwa wakikabiliwa na shauri hilo la uhujumu uchumi.
Akisoma hukumu hiyo tarehe 22 Januari, 2026, Mheshimiwa Jaji Otaru Joachimu alisema mahakama imezingatia muda wa miaka mitano na miezi tisa ambao mshtakiwa amekaa rumande tangu alipokamatwa. Kutokana na hilo, mahakama imeelekeza kuwa atatumikia kifungo cha miaka 22 na miezi mitatu iliyobaki ili kukamilisha adhabu yake.
Katika hatua nyingine, mahakama hiyo imemuondolea mashtaka mshtakiwa Alistair Amon Mbele, baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake bila kuacha shaka yoyote. Mshtakiwa huyo alikuwa anashtakiwa pamoja na wenzake katika shauri la uhujumu uchumi namba ECO 36/2020.
Shauri hilo liliwahusu watuhumiwa watatu ambao ni David Kanayo Chukwu, raia wa Nigeria, Isso Lomward Lupembe, raia wa Tanzania, na Alistair Amon Mbele, pia raia wa Tanzania.
Kwa upande wa mshtakiwa David Kanayo Chukwu, ambaye ni raia wa Nigeria, kesi yake bado inaendelea katika mahakama hiyo baada ya kukana shtaka linalomkabili.
Upande wa Jamhuri katika shauri hilo uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali Elizabeth Muhangwa na Phoibe Magili.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, watuhumiwa hao walikamatwa tarehe 15 Aprili 2020, katika eneo la Mbezi, Kibanda cha Mkaa, na maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), wakidaiwa kusafirisha dawa za kulevya kiasi cha kilogramu 268.50 aina ya heroin.




EmoticonEmoticon