Matembezi ya UVCCM kuunga mkono maadhimisho ya sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar

January 10, 2017


                                                    Na Othman Khamis Ame, OMPR,
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Taifa linawategemea Vijana  wakati wowote katika dhana nzima itakayothibitisha kwamba wanasimamia kwa vitendo Mapinduzi katika kuondoa maovu yote yanayolikabili Taifa.
Alisema Serikali zote mbili ile na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na iIe ya Mapinduzi ya Zanzibar zinataka kuona  Vijana wake wanakuwa chem chem ya Maendeleo badala ya kuwa dimbwi la matatizo mitaani.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiyafunga Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi { UVCCM } kuunga mkono maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964  hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Alisema Vijana ambao ndio warithi wa kulinda Mapinduzi ya Zanzibar dhana iliyoanzishwa  na muasisi wa Mapinduzi hayo Mzee Abeid Amani Karume wana wajibu wa  kusimamia vita vya mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, udhalilishaji wa wanawake na watoto,  uonevu  pamoja na ufisadi.
Balozi Seif alikariri maneno ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume yaliyoeleza maana halisi ya Mapinduzi daima ambayo sio kupindua watu bali ni kuondoa matendo mabaya katika jamii na kusimamia haki na mazuri yote.
Akizungumzia changamoto kubwa zinazowakabili Vijana hasa  ukosefu wa ajira ambalo limekuwa likizikumba nchi mbali mbali Duniani  Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  imeandaa Mipango imara ya kukabiliana na changamoto hiyo .
Mapema akitoa taarifa ya matembezi hayo Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Tanzania Ndugu Shaka Hamdu Shaka  alisema Vijana wengi nchini huingia katika majaribu ya kudanganywa  historia ya Zanzibar  na kupelelekea kukejeli Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Nd. Shaka alisema Mapinduzi ya Zanzibar  yametandikwa kwa  zulia la Umoja, Upendo na mshikamano chini ya majemadari waliofanya mapinduzi hayo ambao wanastahiki kuendelea kuenziwa na wananchi na Vijana wa kizazi cha sasa.
Akitoa salamu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anyesimamia Mazingira na Muungano Mh. Januari Yussuf  Makamba alisema Mapinduzi ya Zanzibar ni kielelezo tosha cha kujitambua kwa waafrika wa Visiwa vya Zanzibar.
Mh. Januari alisema Wakombozi wa Mapinduzi ya Visiwa vya Zanzibar wameacha urithi mkubwa kwa vijana wa Kizazi kipya unayostahiki kulindwa na kuendelezwa kwa faida na maslahi ya Wananchi wake.
Alisema njia pekee na sahihi ya kuendelea  kuimarika kwa Muungano wa Tanganyika  na Zanzibar  ni kudumisha Mapinduzi ya Zanzibar kupitia njia ya kuipatia ushindi CCM katika chaguzi zote zinazoendelea kufanyika hapa Nchini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »