MHANDISI SAMAMBA ASISITIZA UJENZI WA VIWANDA VYA UONGEZAJI THAMANI YA MADINI NCHINI

October 15, 2025




Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, ametoa wito kwa watendaji wa Tume ya Madini nchini kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uongezaji thamani ya madini ili kuongeza ajira, kukuza fursa za kiuchumi na kuimarisha mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa.


Akizungumza leo, Oktoba 15, 2025, jijini Tanga katika kikao cha menejimenti ya Tume ya Madini kilichoshirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, Makamishna wa Tume ya Madini Mhandisi Theonestina Mwasha na Dkt. Theresia Numbi, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Mhandisi Samamba amesema kuwa Sekta ya Madini ina nafasi kubwa katika kukuza uchumi endapo uongezaji thamani utawekewa kipaumbele.


“Mnapoweka mazingira rafiki ya uwekezaji kama vile kurahisisha upatikanaji wa vibali na miundombinu, wawekezaji wanaongezeka, ajira zinapatikana, mapato ya Serikali yanaongezeka na uchumi unakua,” amesema Mhandisi Samamba.


Amesisitiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kushirikiana na viongozi wa mikoa na taasisi nyingine za Serikali kuhakikisha mazingira ya uwekezaji kwenye viwanda vya uongezaji thamani wa madini yanakuwa wezeshi, ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Samamba amewataka Maafisa hao kuendelea kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo kwa kuwapatia elimu ya Sekta ya Madini, taarifa za kijiolojia kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), kuwaunganisha na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na taasisi za kifedha ili kuongeza tija na mapato yao.


“Ninaamini tukiwasaidia wachimbaji wadogo wataongeza ajira, kukuza mzunguko wa fedha na kuiwezesha Serikali kukusanya kodi zaidi kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii kama elimu, afya, barabara na maji,” amesisitiza.


Aidha, ameitaka Tume ya Madini kuendelea kutoa elimu kwa Chama cha Watoa Huduma kwenye Migodi (TAMISA) ili kuongeza ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini kupitia mpango wa Local Content.


Vilevile, amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa elimu ili kuepuka ajali na uharibifu wa mazingira. Pia amesisitiza umuhimu wa kusimamia haki katika utatuzi wa migogoro ya wachimbaji wadogo.


Mhandisi Samamba amehitimisha kwa kuwataka watumishi wote wa Tume ya Madini kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi litakalofanyika Oktoba 29, 2025, nchi nzima.


Kwa upande wao, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo na Katibu Mtendaji, Mhandisi Ramadhani Lwamo, wameishukuru Wizara ya Madini kwa kuendelea kuiwezesha Tume kupitia vitendea kazi ikiwemo magari, pikipiki, fedha na rasilimaliwatu, hali iliyochangia ongezeko la makusanyo ya maduhuli mwaka hadi mwaka.


Wamesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Julai–Septemba), Tume ya Madini imekusanya Shilingi Bilioni 315.4 sawa na asilimia 105.13 ya lengo la Shilingi Bilioni 299.99, na kuwataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuongeza ubunifu na juhudi ili kufikia na kuvuka lengo la Shilingi Trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.








Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »