WAZIRI MKUU APOKEA MSAADA WA SH. MILIONI 27.62

October 14, 2016

shivyata
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa  akisalimiana na Ahmed Olotu(Mzee Chilo) mara baada ya kupokea shilingi laki sita na ishirini kutoka kwa Mtandao wa wasanii(SHIWATA) ikiwa ni msaada wa kusaidia waathirika wa tetemeko la Ardhi Mkoani Kagera.Wengine pichani ni Mkurugenzi  Idara ya uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brigedia Gen.Mbazi Msuya na Caasim Taalib(wa tano kushoto)  ambaye ni Mwenyekiti wa mtandao wa wasanii.
shivyata1
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa  akiwa katika picha ya pamoja na wafanyabiashara ndogondogo solo la kariakoo  mara baada ya kupokea msaada wa nguo mchanganyiko,midoli na kanzu wenye thamani ya  shilingi milioni 2 ikiwa ni msaada wa kusaidia waathirika wa tetemeko la Ardhi Mkoani Kagera.
……………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea fedha taslimu sh. milioni 25.62 pamoja na nguo zenye thamani ya sh. milioni mbili  kutoka kwa wadau mbalimbali.
Makabidhiano ya michango hiyo yamefanyika leo (Ijumaa, Oktoba 14, 2016) kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Akiwashukuru wadau hao Waziri Mkuu ameahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa.
“Nawashukuru kwa kuamua kutumia siku ya leo ya kukumbuku ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwachangia wenzetu waliopatwa na maafa,” amesema.
Waziri Mkuu amesema michango hiyo ni muhimu na inaonyesha mshikamano wa dhati uliopo baina ya Watanzania.

.
Misaada hiyo imetolewa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) sh. milioni 20, Mtandao wa Wasanii Tanzania sh. 620,000 na nguo mifuko miwili, Chama cha Makatibu Mahsusi (TAPSEA) sh. milioni tano.
Wengine ni Umoja wa Wafanyabiashara Ndogondogo soko la Kariakoo ambao wametoa marobota mawili ya nguo (suruali, kanzu na nguo za akinamama na moja la wanasesere kwa ajili ya watoto waliopatwa na maafa vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni mbili.
Fedha na nguo hizo vimetolewa kwa ajili ya  wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa.
Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali .

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »