MTATURU: JESHI LA POLISI HALIPASWI KUFANYA KAZI KWA MAZOEA

August 15, 2016
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akizungumza na askari wa Jeshi la polisi mara baada ya ziara yake katika makao makuu ya Wilaya hiyo eneo la Ikungi.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Kituoni hapo.
 Dc Mtaturu akikagua chumba cha mahabusu kituoni hapo
 Askari watiifu wa Jeshi la Polisi Wilayani Ikungi waliposimama kutoa heshima zao kwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi alipotembelea katika ofisi yao (Picha zote na Mathias Canal)
Dc Mtaturu akikagua maeneo mbalimbali katika viunga vya Jeshi la Polisi Mkao Makuu Wilayani Ikungi
Askari watiifu Wilayani Ikungi wakimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na usalama Wilaya Ya Ikungi Dc Miraji Jumanne Mtaturu
 
Na Mathias Canal, Singida
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu ameliasa jeshi la polisi Wilayani humo kutofanya kazi kwa mazoea badala yake kuimarisha ulinzi na usalama wa Raia na mali zao.

Mtaturu ameyasema hayo wakati wa kikao cha pamoja na askari wa jeshi hilo Wilayani humo ikiwa ni ziara yake ya mwanzo kudhuru katika ofisi za makao makuu ya Jeshi hilo kwa ajili ya kujionea hali ya utendaji wa askari hao sawia na kukagua ofisi hizo ili kujua changamoto zinazowakabili katika utendaji wao.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa kitendo cha baadhi ya askari kupokea Rushwa kutoka kwa wananchi ni miongoni mwa sababu zinazopelekea wananchi kukosa imani na serikali na kulipaka matope jeshi hilo ikiwa ni pamoja na kuifanya serikali ionekane haifanyi kazi yake ipasavyo.

“Hakuna asiyetambua kuwa Rushwa ni adui wa haki hivyo nawasihi askari wapambanaji kutochukua Rushwa ili kuifanya jamii kuwa na imani na askari wao jambo hilo litaongeza heshima kwenu na kwa serikali kwa ujumla, lakini mnapaswa kutambua kuwa kupokea Rushwa kunasababisha wananchi kujichukulia sheria mkononi jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa nchi yetu” Alisema Mtaturu

Mtaturu alisema kuwa Jeshi la Polisi ni sehemu ya ukombozi wa Taifa pia ni sehemu muhimu  ya  kuimarisha usalama wa Wananchi, hivyo ikifikia hatua wananchi wanakosa imani na jeshi la polisi ni wazi kuwa nchi itakuwa inaelekea mahali ambapo sio sahihi.

Pamoja na mambo mengine Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa serikali inatambua kuwa kuna upungufu wa nyumba za kuishi askari, vifaa vya utendaji kazi, Pamoja na mazingira na miundombinu kuwa duni hivyo serikali imejipanga kuimarisha kadhia hizo kwa Jeshi la Polisi ambapo tayari kuelekea kwenye maboresho wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es salaam kuwa eneo la mfano (Pilot Area) ili kuondoa changamoto hizo.

Dc Mtaturu ametoa mwito kwa askari hao kuwashirikisha wananchi kwa kiasi kikubwa pale inapobidi ili kupunguza sintofahamu iliyopo katika jamii ya askari kufanya kazi wenyewe pasina kushirikisha Raia kikamilifu.

“Nina amini katika utendaji wa ushirikishwaji kwa wananchi kufanya hivyo ni kuwasaidia wananchi kupunguza hisia hasi walizonazo juu ya utendaji wa Jeshi la Polisi, lakini pia nawaomba mfanye upelelezi kwa haraka kwa kesi zilizopo mezani kwenu ili kurahisisha kupunguza mlundikano wa kesi jambo linalopelekea kutotendewa haki kwa baadhi ya wananchi” Alisema Mtaturu

Kikao cha pamoja kati ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi na Askari wa Jeshi la Polisi Wilayani humo kilikuwa na taswira chanya ya kufahamiana, kuimarisha umoja kiutendaji pamoja na kukumbushana majukumu ya kazi.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Ikungi pia amewapongeza askari hao pamoja na mazingira magumu waliyonayo lakini wanafanya kazi vizuri kwa mujibu wa viapo vyao.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »