HOTUBA YA MHE. SAMIA SULUHU HASSAN, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE KONGAMANO NA MAONESHO YA KITENGO CHA WAHANDISI WANAWAKE CHA TAASISI YA WAHANDISI TANZANIA, TAREHE 12 AGOSTI, 2016 KATIKA UKUMBI WA MAKUMBUSHO YA TAIFA, DAR ES SALAAM

August 15, 2016




Rais wa Taasisi ya Wahandisi;
 
Ndugu Mwenyekiti, Kitengo cha Wahandisi Wanawake cha Taasisi ya Wahandisi Tanzania;
 
Ubalozi wa Norway;
Msajili wa Bodi ya Wahandisi;
Ndugu Wanakamati ya Maandalizi;
Ndugu Wahandisi Wanawake;
Wanahabari;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
 
Asalaam Aleikum! Bwana Asifiwe!
Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na amani kwa kutujalia uzima wa afya kuweza kujumuika nanyi. Pili natoa shukrani zangu za dhati kwa Mhe. Mhandisi Stella Manyanya (Mb), Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Mwenyekiti wa Kitengo cha Wahandisi Wanawake Tanzania pamoja na kamati nzima ya maandalizi kwa mwaliko huu wa kuja kufungua kongamano hili na maonesho. Ni heshima kubwa kwangu.  Asanteni sana.
 
Naweza kusema nimekuwa mtu mwenye bahati kubwa ya kushirikishwa na kushiriki katika mikutano mbalimbali inayohusu fani mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na wanawake katika kujikwamua kiuchumi. Leo hii nina furaha isiyo kifani kuwa pamoja na wanawake ambao wameweza kumudu kikamilifu kazi ambazo hapo awali tuliaminishwa kuwa ni kazi za mwanaume. Inatia moyo sana kuona kuwa Tanzania tumeweza kupiga hatua katika kumkwamua mwanamke kiuchumi na kuwa mchango wa mwanamke sasa ni mkubwa hata kwenye sekta ambazo hapo awali zilitawaliwa na wanaume.
 
Rais wa Taasisi ya Wahandisi;
Ndugu Mwenyekiti, Kitengo cha Wahandisi Wanawake cha Taasisi ya Wahandisi Tanzania;
Mabibi na Mabwana;
Kama mlivyosikia katika hotuba ya Mwenyekiti; kitengo cha wanawake wahandisi ni miongoni mwa vitengo chini ya Taasisi ya Wahandisi Tanzania. Nichukue fursa hii kuipongeza Taasisi kwa kuunda kitengo hiki na kukipa majukumu ya kuratibu fursa na changamoto zinazogusa jamii ya Kitanzania; hususani wanawake wahandisi. Ni imani yangu kuwa mnaitumia fursa hii kuainisha vipaumbele; juhudi; na mafanikio ya wanawake wahandisi bila kusahau changamoto mbalimbali zinazowakabili wahandisi  hawa wanawake na jamii kwa ujumla.
 
Leo hii niwaase kwa kusema kuwa wahandisi wanawake wataongezeka na kuimarika ikiwa tu nyinyi ambao mko ndani ya tasnia mtashikamana na kufanya kazi kwa bidii.  Nataka kuwakumbusha ya kwamba iwapo na nyinyi msingepewa ushirikiano na wanawake wenzenu basi idadi hii  ninayoiona hapa leo ingekuwa ndogo zaidi.  Hivyo basi, Naomba mtambue nafasi zenu  na muwe walimu na walezi wa wenzenu katika fani hii. Vilevile muda umefika sasa wa nyinyi kujitolea kwa hali na mali katika kuendesha kampeni za kuwashawishi watoto wa kike ili wajenge ari ya kupenda masomo ya sayansi na hisabati ambayo ndiyo msingi wa mafunzo ya uhandisi.
 
Napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa Ndugu Mwenyekiti ambae pia ni Rais wa Wanawake Wahandisi na Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Wizara yake na Kitengo cha Wahandisi Wanawake cha Taasisi ya Wahandisi Tanzania kuandaa kampeni mbalimbali za kuwahimiza wanafunzi hasa wa kike kusoma masomo ya sayansi na hisabati. Nina imani kuwa kwa nafasi yake kama Mhandisi mwanamke; Naibu Waziri na Mzazi ana mchango mkubwa wa kuwaelimisha, kuwaunganisha na kuwaendeleza watoto wa kike  ili kuweza kujitambua na kuithamini nafasi yao katika kuchangia maendeleo ya nchi kupitia   fani za sayansi na teknolojia.
 
Ndugu Mwenyekiti na Washiriki wote;
Niwapongeze kwa kuchagua kauli mbiu yenye kwenda na wakati inayosema ‘Kumwezesha mhandisi mwanamke kukuza ujuzi katika fani ya uhandisi na kuchangia maendeleo ya jamii’. Lengo likiwa ni kuhamasisha wanawake wahandisi kuzigundua na kutumia fursa mbalimbali kujiendeleza katika fani ya uhandisi na kutatua changamoto zinazokabili jumuiya ya Watanzania.
 
Serikali kwa kutambua umuhimu wa wahandisi katika  maendeleo ya nchi hususani katika  sekta za: Nishati; madini; mabarabara; maji; uvuvi, kilimo n.k imeendelea kuweka mipango madhubuti ya kuinua na kuimarisha fani ya uhandisi. Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuongeza vyuo vya uhandisi kutoka kimoja miaka ya 1970 mpaka vyuo 9 kwa sasa.  Mbali na kuongeza idadi ya vyuo imeendelea kuongeza  maabara katika shule za umma ili kuwavutia wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.  Aidha Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo kwa njia ya vitendo kwa wanafunzi.
 
 Pamoja na kuongezeka kwa vyuo vya uhandisi na mikakati mingine ya Serikali, udahili wa wanawake katika fani mbalimbali za kihandisi umebaki kuwa wa chini. Hivyo basi kuna haja ya kuongeza ushawishi kwa watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi na hisabati na kudahiliwa katika vyuo vinavyofundisha fani ya uhandisi.
 
Sambamba na kupata mafanikio ya kuongeza idadi ya wahandisi watalaamu wanawake kutoka 39 mwaka 2005 hadi 298 mwaka 2015, bado idadi ya wahandisi wanawake wabobezi imekuwa ndogo. Hii ni moja ya changamoto ambazo kitengo cha wanawake wahandisi kinatakiwa kufanyia kazi ili kuhakikisha idadi hii inaongezeka mwaka hadi mwaka.
 
Ninafarijika kuona kuwa kongamano limepambwa kwa mihadhara toka kwa wahandisi wanawake waliobobea na kufanikiwa katika ngazi mbalimbali za kihandisi wakitumia uzoefu wao kuhamasisha wengine. Mihadhara hiyo inayojumuisha ukuaji katika fani ya uhandisi na changamoto zake, uvumbuzi na matumizi ya teknolojia, ujasiriamali na  biashara pamoja na utawala na uongozi. Mada hizi zitasaidia kuwahamasisha na kuwaongoza wanawake wahandisi kufanikiwa zaidi katika fani.
 
Niwapongeze pia kwa kujumuisha kongamano na maonesho ya bidhaa/huduma zinazotolewa na wahandisi wanawake wenye weledi katika fani zao. Maonesho hayo nayo ni chachu kwa wahandisi wanawake kutumia ujuzi na fursa zilizopo kuwa wajasiriamali. Ikumbukwe kwamba nchi hii ina vyuo tisa vinavyofundisha uhandisi, na kutokana na ajira kuwa chache, ujasiriamali unaweza kuwa suluhisho la kudumu.  Hivyo basi nitoe wito kwa  wahandisi waliojikita kwenye ujasiriamali  kuhakikisha kuwa  wanafanya biashara  hiyo kwa ustadi mkubwa  ili kufikia malengo yao.
 
Nitoe pongezi pia kwa kuwajumuisha wanafunzi wa kike wa sekondari na vyuo katika kuonesha miradi yao. Hii inawapa fursa ya kuonesha uwezo wao katika masomo ya sayansi na uhandisi na pia kuwapa mazoea ya kujieleza na kujiamini. Vile vile, shule na vyuo vilivyoonesha miradi yao ni zile zilizoko Dar es Salaam peke yake. Mnayo changamoto ya kuangalia ni kwa jinsi gani mtaweza kutoa hamasa hii pia kwa shule na vyuo vilivyo nje ya Dar es Salaam.
 
Ndugu Mwenyekiti;
Kama ulivyoeleza awali, kuna changamoto mbalimbali zinazokikabili Kitengo cha Wahandisi Wanawake. Napenda kuwaahidi kuwa kama serikali, tutazichukua na kuzifanyia kazi. Lengo ni kuhamasisha wahandisi wanawake kufanya kazi kwa bidii zaidi na kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya Watanzania.
 
Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwa serikali ya viwanda. Hii ni kusema, serikali itatumia rasilimali zilizopo kujenga na kuimarisha viwanda vilivyopo nchini, ili kuhakikisha kwamba Tanzania inafikia uchumi wa kati ifikapo 2025. Matumaini yetu mtatuunga mkono kwenye azma yetu hii  na kuhakikisha mnafanya kazi kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu. Kama Serikali tutahakikisha kuwa nafasi za kusimamia miradi ya kihandisi itatolewa kwa kampuni za wazawa wenye uzoefu na weledi kabla ya kutolewa kwa kampuni za nje na iwapo zitapewa kampuni za nje basi tutazingatia suala zima la ubia.
 
Kabla ya kumalizia Hotuba yangu napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Norway kwa mchango wao wa Tshs. 4.3bn ili kuchangia mpango wa miaka mitano wa (2016- 2021) ambao  utasaidia kuwajengea uzoefu wahandisi wanawake ili waweze kusajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi. Mpango huu unatarajia kunufaisha wanafunzi wa kike 150.  Hivyo basi kwa niaba ya Serikali tunasema asante sana kwa marafiki zetu wa Norway. Msaada huu ni muhimu katika kufanikisha lengo la kufikia uchumi wa viwanda na kipato cha kati ifikapo 2025. Vilevile utatusaidia katika kufikia lengo namba Tano la Kumuwezesha Mwanamke kiuchumi la Malengo ya Maendeleo endelevu ya Dunia ya mwaka 2030.
 
Nimalizie kwa kutoa wito kwa Taasisi ya Wahandisi Tanzania kuendelea na jukumu la kuwaunganisha wahandisi wote walio nje na ndani ya nchi kwa manufaa ya nchi yetu. Serikali inaikaribisha Taasisi kuishauri katika mambo mbalimbali yanayohusu uhandisi na wahandisi Tanzania ili kuhakikisha azma ya Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati inafikiwa ifikapo 2025.
 
Baada ya kusema hayo, natangaza rasmi Kongamano na Maonesho ya Wahandisi Wanawake 2016 yamefunguliwa.      
 
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »