Hakuna fidia kwa wakazi watakaopisha miradi ya REA- Prof Muhongo

August 13, 2016
fid1
Mkandarasi kutoka kampuni ya Future Century Limited  ya  Tanzania Hellen Masanja (kushoto) akielezea utekelezaji wa usambazaji wa umeme  katika jimbo la Handeni Vijijini mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) katika eneo la Kweditilibe wilayani Handeni mkoani Tanga. Profesa Muhongo  yupo mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme  vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati  Vijijini (REA) pamoja na kuzungumza na wananchi.
fid2
Mbunge wa Handeni Vijijini (CCM), Mboni Mhita akielezea utekelezaji wa miradi ya  umeme  vijijini  (REA) uliofanywa na kampuni ya Future Century Limited katika  jimbo hilo katika eneo la Kweditilibe wilayani Handeni mkoani Tanga.
fid3
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akielezea mikakati ya usambazaji wa umeme vijijini itakavyotekelezwa na  Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya  Tatu katika eneo la Kweditilibe wilayani Handeni mkoani Tanga
fid4
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akipokea zawadi  ya mbuzi kutoka kwa baadhi wa wakazi kutoka eneo la Kweditilibe wilayani Handeni mkoani Tanga
fid5
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisalimiana na wanakijiji wa kata ya Kwamgwe iliyopo wilayani Handeni mkoani Tanga
fid6
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisani kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika  kata ya Kwamgwe wilayani Handeni mkoani Tanga.
fid7
Afisa Mtendaji wa Kata ya Kwamgwe iliyopo wilayani Handeni mkoani  Tanga, Athumani Ndutu (kushoto) akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya usambazaji  wa umeme vijijini  inayotekelezwa na  Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili.
fid8
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akisikiliza maoni yaliyokuwa yanawasilishwa na mmoja  wa wakazi wa Kata ya Kamgwe wilayani Handeni mkoani Tanga. Kulia ni Mbunge wa Jimbo  la Handeni Vijijini, Mboni Mhita.
…………………………………………………………………………….
Na  Greyson Mwase, Tanga
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa hakuna fidia yoyote itakayotolewa kwa wananchi watakaopisha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme  vijijijni unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Profesa Muhongo aliyasema hayo alipokuwa  akizungumza  kwa nyakati tofauti na wakazi kutoka katika vijiji vya Kweditibile na  Kamgwe  vilivyopo katika wilaya ya Handeni mkoani  Tanga. Profesa Muhongo  yupo mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi ya  usambazaji wa umeme  vijijini  inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na kuzungumza na wananchi.
Profesa Muhongo alisema kuwa serikali imetenga kiasi kikubwa cha  fedha kwa ajili ya usambazaji wa umeme  vijijini  ambapo  iwapo fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kulipa  fidia, inaweza kuathiri utekelezaji wa miradi  ya REA
“Mkumbuke kuwa  iwapo fedha hizi zitatumika kulipa  fidia kwa wananchi wanaopisha miradi ya umeme  vijijini, fedha nyingi zitatumika na kukwamisha utekelezaji wa miradi ya REA,” alisema Profesa Muhongo
Aliendelea kusema kuwa miundombinu ya umeme haihitaji eneo kubwa hivyo haiwezi kuathiri mazao kwenye mashamba kama inavyoaminika na watu wengi
Alifafanua kuwa nishati ya umeme ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuongeza kuwa serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 vijiji vyote nchini  vinapata huduma ya umeme na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi
Alisema kuwepo kwa nishati ya uhakika  vijijini kutapelekea wanavijiji kuanzisha  viwanda vya kusaga  na kukoboa nafaka, kilimo cha  kisasa na kuongezeka kwa ufaulu darasani.
Hata hivyo Profesa Muhongo alitoa agizo kwa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuhakikisha kuwa wananchi waliostahili kuunganishiwa umeme kupitia REA Awamu ya pili wanaunganishiwa kabla ya mwezi Oktoba mwishoni kwa gharama  ya shilingi 27,000.
Wakati huohuo Mbunge wa Handeni Vijijini, Mboni Mhita aliishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kasi kubwa ya usambazaji wa umeme  vijijini na kuwataka wananchi  wa jimbo lake kuchangamkia fursa hiyo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »