Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Serikali ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania imesaidia jumla ya viwanda vidogo 48,996 kwa kuvipa
huduma muhimu zinazowawezesha wajasiriamali kusimama wenyewe ili
kuondokana na lindi la umasikini.
Takwimu hizo zimetolewa na
Mkurugenzi wa Viwanda Vidogo na vya Kati kutoka Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Dkt. Consolatha Ishebabi alipokuwa akizungumza na
mwandishi wa habari hii kuhusu mikakati ya Serikali juu ya kuendeleza
viwanda vidogo pamoja na umuhimu wa viwanda hivyo.
Dkt. Ishebabi amesema kuwa
Viwanda Vidogo vikiendelezwa ndio mwanzo wa kuwa na viwanda vya Kati na
Vikubwa na hiyo ndio sababu kubwa inayoifanya Serikali kutilia mkazo na
kuzidi kuweka mikakati mingi ya kuviinua viwanda hivyo ili vikue na
kufikia viwanda vya kati au vikubwa.
“Kwa mujibu wa Sensa ya Viwanda
ya mwaka 2013, Tanzania ina jumla ya viwanda vidogo 48,996 ambavyo
vimesaidia kutoa jumla ya ajira 156,476 kwa wananchi, hivyo tunaona
umuhimu wa viwanda vidogo katika suala la kutoa ajira na kupunguza
umasikini kwa kiasi kikubwa”, alisema Dkt. Ishebabi.
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa
viwanda vidogo sio mali ya Serikali bali Serikali iko pamoja na viwanda
hivyo katika kuvisaidia ili viendelee na kuhakikisha vinakuwa kufikia
viwanda vya kati au vikubwa hivyo, kazi ya Serikali ni kuwahamasisha
wananchi na kuwapa misaada ya elimu, mikopo pamoja na kuwawezesha maeneo
ya kufanyia shughuli hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Masoko na Habari wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Viwanda Vidogo (SIDO),
Janeth Minja amesema kuwa Shirika hilo ni kubwa na liko katika Mikoa
yote Tanzania, linawasaidia wajasiriamali kwa kuwapa huduma za aina 4
ambazo ni; mafunzo, teknolojia, mikopo pamoja na kuwatafutia masoko ya
bidhaa zao.
“Napenda kutoa rai kwa wananchi
hasa vijana na wanawake wasio na ajira kuwa wasijibweteke tu majumbani
bali watumie fursa zinazotolewa na SIDO ili waweze kujikwamua kiuchumi
na kuondokana na umasikini, kama mtu ana wazo la biashara anatakiwa
awasiliane na ofisi zetu za SIDO zilizopo kwenye Mkoa husika”, alisema
Janeth.
EmoticonEmoticon