Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati wa Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Bi. Rose Mdami, akizungumza na waandishi
wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Saalam.
Katika kikao hicho NIDA iliwasilisha mpango usajili kufikia 31 Desemba
2016 ambapo usajili utakamilika nchini nzima na wananchi kuanza kutumia
namba ya utambulisho kupata huduma. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara
ya Udhibiti Mifumo ya Komputa (TEHAMA) Ndugu Mohamed Khamis, kushoto ni
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji Vitambulisho Ndugu Alphonce
Malibiche
Mkurugenzi
wa Idara ya Udhibiti Mifumo ya Komputa (TEHAMA) Ndugu Mohamed Khamis,
akifafanua namna mwananchi anaweza kutumia tovuti salama kujua taarifa
zake wakati wa kikao na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa idara ya
Habari Maelezo Jijini Dar es salaam. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano na Hifadhi Hati wa NIDA Bi Rose Mdami.
Serikali imekusudia kukamilisha Usajili Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wote kufikia Desemba 31 mwaka huu.
Akuzungumza
na vyombo vya habari leo, msemaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
Bi. Rose Mdami, amesema NIDA imepanga kutumia taarifa za NEC kukamilisha
usajili wa awali na kutoa namba ya Utambulisho kwa wananchi wote ambao
hawakusajiliwa katika mfumo wa NIDA.
Akifafanua,
Bi Rose amesema baada ya kuhakikisha kila mwananchi ana Nambari ya
Utambulisho, kila mwananchi atalazimika kukamilisha usajili wake ikiwa
ni hatua ya kujaza vipengele vya maswali vilivyobakia katika fomu ya
maombi ya vitambulisho kabla ya kupata utambulisho kamili.
“kama
mnavyofahamu, katika usajili wa NEC fomu ilikuwa na vipengele 32 vya
kujaza kulinganisha na fomu ya NIDA ambayo ina vipengele 74, hivyo ni
lazima kila mwananchi kutambua, ili kuwa na utambulisho kamili lazima
kujaza vipengele vilivyobaki pamoja na kuambatanisha nakala ya viambata
vyake muhimu kuthibitisha taarifa za umri, uraia na makazi” alisisitiza.
Amesema
lengo la kuanza kutoa namba ya utambulisho ni kuwawezesha wananchi
kuanza kufaidi huduma zinazotolewa, wakati uzalishaji Vitambulisho
ukiendelea. Uwezo wa mashine za NIDA ni kuzalisha vitambulisho 24,000
kwa siku hivyo itachukua muda kukamilisha uchapishaji wa vitambulisho
kulingana na idadi ya Watanzania, Wageni na Wakimbizi watakao
andikishwa.
Akifafanua
namna NIDA ilivyojipanga kuhakikisha zoezi la usajili linakamilika kwa
wakati iliyojiwekea, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji
Vitambulisho Ndugu Alphonce Malibiche, amesema NIDA imeshapokea BVR Kit
5000 na kwakuwa NIDA tayari ilishakuwa na MEU (Mobile Enrolment Unit)
1500, vifaa hivi vitasambazwa nchi nzima mpaka ngazi ya Kata ambapo
wananchi watasajiliwa kwa hatua zote; lengo ni kuwafikia wananchi ambao
hawakujisajili kupiga kura na vijana wanaotimiza umri wa miaka 18.
“NIDA
imejipanga kuchakata taarifa za NEC na kuingiza taarifa hizo katika
mfumo wa NIDA utakaoondoa durufu ili kuruhusu majina kupelekwa kwenye
Kamati za Ulinzi na Usalama kwa uhakiki pamoja na kuruhusu wananchi
kuweka mapingamizi kwa wale wote watakaotiliwa shaka ya uraia”.
Amesema
NIDA itatumia mbinu zote katika kusambaza namba za Utambulisho mpaka
vijijini, pamoja na kutumia ofisi za NIDA zitakazofunguliwa katika
Wilaya zote nchini, kuwezesha kuanza kwa matumizi ya utambulisho
yatakayojikita katika huduma mbalimbali zitolewazo nchini.
Akipambanua
namna mfumo wa Utambulisho wa Taifa utakavyotumika katika kutoa huduma
mbalimbali, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uchambuzi Mifumo ya Kompyuta ndugu
Mohamed Khamis amesema tayari NIDA imeshabuni mifumo mbalimbali
itakayotumika kusoma taarifa katika mfumo Mama (Kanzidata) ya NIDA
ikiwemo tovuti salama ambayo itamwezesha mtoa huduma kusoma taarifa za
mteja wake mahali alipo kwa idhini itakayotolewa na mteja mwenyewe.
Amesema
mfumo huu wa kitaalamu umebuniwa katika kumrahisishia mwananchi kupata
huduma pamoja na kufuatilia hatua ya usajili wake ilipofikia. Mbali na
tovuti salama pia njia ya SMS itatumika kusoma taarifa za mwombaji.
Katika
hatua zote hizi suala la usalama wa taarifa limezingatiwa na hakutakuwa
na taarifa za mwananchi zitakazosomwa bila idhini ya mhusika ambaye ni
mmiliki wa Utambulisho/kitambulisho.
“kupitia
mfumo huu wa NIDA Serikali itaweza kubaini na kuondokana kabisa na
tatizo la wafanyakazi hewa kwani namba ya utambulisho niya kipekee na
hivyo hakutakuwepo durufu ya taarifa” alisema.
Tayari
NIDA imeshaanza mazungumzo na Utumishi kufanya usajili wa watumishi
Nchi nzima ili mfumo wa mishahara kuunganishwa na mfumo mama wa taarifa
(Kanzidata) NIDA.
Mpaka
sasa NIDA imekamilisha ujenzi wa miundombinu na kusajili wananchi
katika mikoa ya Dar-es- salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Tanga, Morogoro na
Zanzibar.
Zaidi
ya vitambulisho mil 2.7 vimeshagawanywa kwa wananchi na kuanza matumizi
katika baadhi ya huduma zikiwemo za kibenki katika baadhi ya mabenki
nchini.
EmoticonEmoticon