Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim,Majaliwa akipokea tuzo ya filamu kutoka
kwa msanii Single Mtambalike aliyoshinda katika Tuzo za Filamu Afrika
kwa mwaka 2016 zilizofanyika chini Nigeria hivi karibuni kulia ni msanii
Elizabeth Michael.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim,Majaliwa (katikati) akiwa katika picha
ya pamoja na washindi wa Tuzo za Filamu Afrika kwa mwaka 2016 pamoja na
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia
Wambura(wa pili kulia), Katibu Mkuu wa Wizara wa Habari, Utamaduni,Sanaa
na Michezo Prof Elisante Ole Grabriel(wa pili kushoto), kulia ni Katibu
Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Joyce Fisso na kushoto ni Rais wa
Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Simon Mwakifamba.
Picha na Raymond Mushumbusi MAELEZO
………………………………………………………………………………………………………………………………….
Na: Immaculate Makilika MAELEZO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amesema Serikali imefarijaka kwa ushindi wa wasanii wa filamu nchini
walioshinda tuzo za filamu Afrika za mwaka 2016(African Magic Viewers
Choice Award) ziliyofanyika jijini Lagos nchini Nigeria mwishoni wa wiki
iliyopita.
Waziri Mkuu Majaliwa, amesema
hayo leo katika ukumbi wa mikutano ulipo katika Ofisi yake Jijini Dares
Salaam, alipokutana na washindi wa tuzo za filamu Afrika za mwaka 2016
(AMVCA) ambao ni Elizabeth Michael ‘Lulu’ aliyeshinda tuzo ya Filamu
Bora ya Afrika Mashariki na Single Mtambalike ‘Richie’ aliyeshinda tuzo
ya Filamu Bora ya Kiswahili pamoja Naibu Waziri wa
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Mhe. Annastazia Wambura,Katibu Mkuu
wa wizara Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya
Filamu Tanzania Bi Joyce Fisso na wasanii wa filamu.
“Serikali imefarijika sana kwa
nyie kwenda Nigeria na kushinda na mmetumia lugha ya Kiswahili, lazima
tutumie nafasi hii kuwatangaza pia mmuendelee na fani hii ili kuvutia
wengi zaidi” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu amewapongeza
wasanii hao na kusema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wasanii
wakati wowote na amewataka kujipanga vizuri kutumia vyama vyao vya
sanaa na kusisitiza kuwa Mhe. Rais John Pombe Magufuli ametoa matamko
kadhaa kuhusu sanaa na wasanii na ameendelea kushughulikia malalamiko
yao ikiwemo suala la COSOTA, na kusema kuwa baada ya taratibu zote
kukamilika suala hilo litasimamiwa na Wizara inayohusika na kazi za
Sanaa.
Waziri Mkuu Majaliwa, pia
amewataka watanzania kuacha tabia ya kutojiamini na kujidharau, na
kuwataka watu waige mfano kwa wasanii hao, na kuwashauri wasanii wote
kwa ujumla kutumia vyombo vya habari kujiimarisha na kujitangaza.
Kwa upande wao, wasanii
waliopata tuzo hizo kwa filamu ya “mapenzi ya Mungu” ya Elizabeth
Michael na filamu ya “Kitendawili” ya Single Mtambalike, wameishukuru
Serikali kwa kuwathamini na kuonesha ushirikiano katika kazi zao za
sanaa, na wameahidi kuendelea kutengeneza kazi nzuri za sanaa ili
ziweze kuitangaza Tanzania kimataifa.
Naye, Rais wa Shirikisho la
Filamu Tanzania(TAFF) Saimon Mwakifamba ameishukuru Serikali kwa
jitihada mbalimbali inazofanya katika kusaidia tasnia ya sanaa kwa
ujumla na ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza
tasnia hiyo kimataifa.