Serikali
imetoa tamko la kulaani kitendo kilichotokea nchini India kwa
mwanafunzi wa kike wa kitanzania kuvuliwa nguo na kutembezwa barabarani
ambapo Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje,Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Kikanda na kimataifa imetoa tamko la kulaani suala
hilo kwa kuitaka Serikali ya india kuchukua hatua.
Akitoa
tamko hilo Bungeni Mjini Dodoma Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Dkt. Augustine Mahiga
amesema ni kweli kwamba kuna mwanafunzi wa kike wa kitanzania alifanyiwa
kitendo cha udhalilishaji nchini India kwa kuvuliwa nguo na kutembezwa
barabarani suala ambalo lilizua mijadala mikubwa nchini kuhusu
udhalilishaji huo.
“Wizara
yetu imezungumza na Balozi wa India nchini na kumweleza ni kwa jinsi
gani watanzania wamefadhaika na kusononeshwa na kitendo alichofanyiwa
mtanzania mwenzao huko India na Balozi alituhakikishia kwamba
amewasiliana na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi yake na kusema Serikali
ya India kwa kushirikiana na Jeshi la polisi nchini humo wamefanikisha
kuwakamata wote waliohusika na kitendo hicho na kuwafikisha mahakamani
kujibu mashataka hayo”
“Pia
Serikali ya India imeahidi kutoa ulinzi kwa wanafunzi wa kitanzania na
wenye asilia ya Afrika wanaosoma huko ili kuwalinda na kuwaepusha na
vitendo hivyo vinavyofanya na raia ambao hawana nia njema kwa mahusiano
mazuri ya kimataifa yaliyopo kati ya India na Tanzania”Alisema Mhe.
Mahiga.
Serikali
ya Tanzania imekuwa na mahusiano mazuri na Serikali ya India kwa miaka
mingi sasa na kutokana na kitendo hiki kilichotokea nchini India,Waziri
wa Mambo ya Nje ya India amefatana na Balozi wa Tanzania nchini humo
kwenda Mji wa Bangalo ili kuongea na wanafunzi wakitanzania na wale
wenye asili ya Afrika wanaosoma huko ili kujenga mahusiano mazuri na
wazawa ikiwa ni jitihada za kupunguza vitendo hivyo kutokea mara kwa
mara.
Imendaliwa na Raymond Mushumbusi – MAELEZO