NAIBU Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha Tanzania inapata umeme wa uhakika, unaopatikana masaa 24, ili kuvutia wawekezaji na kukuza uchumi wa nchi.
Makamba ameyasema hayo leo Novemba 25,2025 jijini Dodoma, baada ya kukagua Kituo cha Kupoozea Umeme cha Zuzu.
Ameongeza kuwa kutokana na uwekezaji mkubwa wa fedha uliofanywa na serikali, ni matarajio yake kuwa mitambo yote itasimamiwa vyema ili kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana.
“Niwasihi waliopewa dhamana ya kusimamia uwekezaji huu kuhakikisha mitambo iliyofungwa katika vituo hivi inalindwa ili isije kuharibiwa, na pia waendele kufanya kazi kwa bidii kufanikisha azma ya serikali ya kuwa na umeme wa uhakika,” amesema Makamba.
Aidha, Makamba amebainisha kuwa licha ya ukuaji wa haraka wa jiji la Dodoma, uwekezaji katika sekta ya nishati bado unakidhi mahitaji ya sasa. Kituo cha Zuzu kilipoanzishwa mwaka 1986 kilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2, lakini sasa kinazalisha megawati 86, ikiwa 70 Dodoma na 16 Kondoa.
Kituo hicho kina uwezo wa kufikia megawati 200, kinachotakiwa kulisha mkoa mzima wa Dodoma.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Athanasius Nagali, amesema kituo hicho ni kitovu cha kusambaza umeme ndani na nje ya nchi.
“Kituo hiki ndicho hub ya kusambaza umeme kutoka Mtwara, na ule unaotoka bwawa la Mwalimu Nyerere kupitia Chalinze pia utasafirishwa hapa na kupoozwa kabla ya kusambazwa kwenda Singida, Mwanza, na hata Kenya,” amesema Mhandisi Nagali
Ameongeza kuwa uwepo wa umeme wa uhakika unatoa fursa kwa wawekezaji wakubwa kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.
.

EmoticonEmoticon