NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO AFUNGUA KIKAO CHA TATU CHA BARAZA KUU LA PILI LA WAFANYAKAZI WA TAASISI YA UHASIBU TANZANIA (TIA).

February 19, 2016

tk1
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji akiwahutubia wajumbe wa Baraza kuu la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wakati akifungua kikao cha tatu cha Baraza hilo kilichofanyika leo katika ukumbi wa TAFORI mkoani Morogoro.
tk2
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha na Mipango Prof. Isaya Jairo akisoma hotuba ya kumkaribisha mgeni rasmi wakati wa kikao cha tatu cha Baraza Kuu la Pili la wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kilichofanyika leo katika ukumbi wa TAFORI mkoani Morogoro.
tk3
Baadhi ya wajumbe wa Baraza kuu la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa kikao cha tatu cha Baraza hilo kilichofanyika leo katika ukumbi wa TAFORI mkoani Morogoro.
tk4
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (wa tano kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza kuu la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) baada ya kufungua kikao cha tatu cha Baraza hilo kilichofanyika leo katika ukumbi wa TAFORI mkoani Morogoro.
……………………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Morogoro.
WITO umetolewa kwa watumishi wa Umma kufanya kazi kwa uadilifu na kutimiza wajibu wao kikamilifu katika sehemu zao za kazi.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji wakati akifungua kikao cha tatu cha Baraza kuu la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), katika ukumbi wa TAFORI mkoani Morogoro.
Dkt. Kijaji amesema kuwa, Serikali haitamvumilia mtumishi wa ngazi yeyote wa wizara ya Fedha na Mipango atakayeshindwa kutimiza wajibu wake kikamilifu ikiwa ni pamoja na kushindwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Naibu Waziri huyo ameuagiza uongozi wa Taasisi hiyo kuendelea kusimamia kwa karibu kazi zote na kutathimini utendaji kazi wa watumishi wake.
“Haipendezi kukuta meza ya Mkurugenzi imejaa majalada huku watumishi wa chini yake wakiwa hawana kazi za kufanya” alisema Naibu Waziri huyo.
Dkt. Kijaji amesisitiza kuwa, wakati umefika kwa kuwapatia watumishi hao kazi za kufanya ili nao wapate uzoefu ambao tayari viongozi waliopo ngazi za juu  wameshaupata.
Pamoja na mambo mengine, Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango amewataka watumishi wa Serikali wakiwemo wa Wizara hiyo kila mmoja wao kuwajibika  katika nafasi yake kwani suala hilo ni  muhimu katika kuleta tija sehemu ya kazi.
“Sasa ni wakati wa watumishi wa umma  kujituma pamoja na kufanyakazi kwa bidii kwa kuwa mmepewa dhamana ya kuwatumikia watanzania wote “ amesema Naibu Waziri huyo.
 Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Dkt. Joseph Kihanda, amesema kuwa Taasisi imejiimarisha katika utoaji wa elimu yenye ubora ili kuwawezesha wahitimu kufanya vizuri katika masomo yao na baadaye katika sehemu zao za kazi.
Amesema jitihada zao za kutoa elimu bora zimethibitishwa na bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) na bodi ya Wataalamu wa manunuzi na ugavi (PSPTB).
Hata hivyo Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema Taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoikabili kwa muda mrefu ikiwemo ya uhaba wa majengo kwani kwa kipindi cha miaka minane Taasisi hiyo imekuwa ikiomba ruzuku Serikalini kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini bado haijapata ruzuku hiyo.
Pia ameitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na uhaba wa wafanyakazi ambapo uwiano wa wahadhiri haulingani na wanafunzi.
Hali hiyo inatokana na Taasisi kupata vibali vichache vya kuajiri wahadhiri na wafanyakazi waendeshaji kutoka Utumishi ikilinganishwa na maombi ya Taasisi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »