Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Maji Bw.
Athumani Sharif akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo
pichani) kuhusu mikakati ya Serikali kutatua tatizo la upatikanaji wa
maji jijini Dar es Salaam mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto
ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa.
(Picha na Fatma Salum.)
…………………………………………………………………………………………..
Na. Georgina Misama – Maelezo
Serikali inatarajia kuzalisha maji lita milioni 270 kwa siku
baada ya kukamilika kwa mradi wa upanuzi wa Chanzo cha Maji cha Ruvu
Chini na upanuzi wa mtambo wa kusafishia maji.
Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika
la Kimarekani la Millenium Challenge Co-operation umegharimu kiasi cha
shilingi bilioni 66.24 na unatarajiwa kukamilika wakati wowote baada ya
kukamilika kwa kazi ya kulaza bomba linalosafirisha maji toka Ruvu chini
kuja Jijini Dar es Salaam.
Akiongea na waandishi wa habari, leo Jijini Dar es Salaam, Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Maji, Bw. Shariff
Athumani amesema kwamba mradi wa upanuzi wa mtambo wa ujenzi wa bomba
la Ruvu Chini utapunguza kero ya maji kwa wakazi wote wanaotumia maji
kutoka Ruvu Chini.
Akiyataja maeneo yatakayofaidika na kukamilika kwa mradi huo ni
pamoja na Bagamoyo na vitongoji vyake, Bunju, Mabwepande, Boko, Tegeta
Kunduchi na Mbezi Beach. Maeneo mengine ni pamoja na Mbezi Juu,
Salasala, Kawe, Makongo, Chuo Kikuu, Mikocheni, Msasani, Masaki,
Mwananyamala, Kinondoni, Magomeni, Sinza, Manzese, Ubungo, Mabibo,
Kigogo, Buguruni, Ilala, Kurasini, Bandarini na maeneo yote ya katikati
ya jiji la Dar es Salaam.
EmoticonEmoticon