Na Magreth Kinabo –maelezo
…………………………………
Serikali imemtaka kila
mwanajamii kutafakari haki ambazo wazee wanastahili na kuweka mipango ya
makusudi katika kuwawezesha kuzipata haki hizo.
Kauli hiyo imetolewa Septemba
30, 2015 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,Dkt, Donan
Mmbando kupitia tamko la wizara hiyo kuhusu maadhimisho ya siku ya
kimataifa ya wazee duniani itakayofanyika kesho Oktoba Mosi ,mwaka huu
wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Umuhimu Kuwashirikisha Wazee Kwa Ustawi Endelevu Mijini”
“Uko umuhimu kwa jamii yetu
kutafakari iwapo tunatambua mahitaji halisi na kuthamini michango yao
kama rasilimali muhimu katika maendeleo ya taifa.
“Tunawashirikisha, tunawaheshimu
na kuwaendeleza kama wananchi wengine na tunaheshimu mila na desturi
nzuri za kuwaenzi wazee hao,” alisema Dkt. Mmbando.
Aliongeza kwamba wazee katika
nchi yetu wanayo nafasi kubwa katika juhudi za kuleta maendeleo. Katika
maisha ya kila siku ya jamii, wazee wanakubalika kuwa ni watoa habari,
ujuzi wa mila na desturi, washauri na wapatanishi. Pia wazee ni walezi
wa watoto wadogo,hususan kwa watoto yatima walioachwa na wazazi wao
kutokana na janga la UKIMWI.
“ Natoa wito kwa watendaji wote
kwa nafasi zao mbalimbali hususan wakurugenzi watendaji Halimashauri
za Miji/Manispaa/Wilaya na wakala mbalimbali zinazotoa huduma kwa wazee
ili ziweke mipango inayozingatia haki za wazee na kuimarisha mifumo ya
kinga ya jamii iliyopo ili kuboresha huduma wanayopata,” alisisitiza.
Aidha Dkt. Mmbando alisema
alisema suala la wazee ni mtambuka, hivyo kila idara na asasi mbalimbali
za Serikali na watu binafsi zishiriki katika kuhakikisha kwamba
juhudi juhudi za makusudi zinafanywa ili kuboresha maisha ya wazee.
Alisema Serikali itaendelea kutambua na kuthamini michango inayotolewa na wazee katika maendeleo ya taifa letu.
“ Hivyo nawaomba wazee waendelee
kushirikiana na Serikali yao katika kuendeleza utulivu na amani
tuliyonayo na pia waendelee kuwa kielelezo bora na urithi kwa vijana
wetu kwa manufaa ya taifa letu,” alisema.
Alitoa changamoto kwa vijana
kuwa karibu na wazee ili kujifunza maadili mema toka kwao na kuwajibika
kuwahudumia ipasavyo na kuweka taratibu za kujiwekea akiba kila
wanavyopata ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kufanya maandalizi ya maisha
kuelekea uzeeni.