Kituo cha kisasa cha michezo kufunguliwa Dar mwezi ujao
- Kinaitwa Jakaya M. Kikwete Park na kitafunguliwa na Rais Kikwete
- Ni cha kwanza cha aina yake nchini na kitafundisha watoto wadogo michezo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete mwezi ujao, Alhamisi, Oktoba 17, 2015, atazindua rasmi Kituo cha
Michezo cha Kisasa cha Jakaya M. Kikwete Youth Park (JMK Park), Kidongo
Chekundu, Dar es Salaam, kituo cha kwanza cha aina yake nchini chenye
kulenga miongoni mwa mambo mengi kuanza kulea wanamichezo tokea wakiwa
wadogo.
Rais Kikwete alikubali kuzindua Kituo hicho wakati wa mazungumzo kati
yake na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Umeme ya Symbion Power, Bwana Paul
Hinks kwenye Hoteli ya JW Marriot Essex House, mjini New York, Marekani
ambako Rais alikuwa anafanya ziara rasmi ya kikazi. Rais Kikwete
alikiwekea Kituo hicho jiwe la msingi mwaka jana.
Katika mkutano huo, uliofanyika jana, Jumanne, Septemba 29, 2015,
Bwana Hinks alimweleza Rais Kikwete kuwa ujenzi wa Kituo hicho sasa
umekamilika tayari kwa uzinduzi na hivyo kuongeza thamani kubwa kwenye
eneo ambalo miaka ya nyuma lilikuwa gereji ya kutengenezea magari.
Kituo hicho cha JMK Park kimegharimu kiasi cha dola za Marekani
milioni mbili na ni matokeo ya ushirikiano ya Kampuni ya Symbion Power
ya Marekani, Klabu ya Soka la Ligi Kuu ya Uingereza ya Sunderland AFC na
Taasisi ya Grasshopper Soccer.
Baada ya uzinduzi huo, Kituo hicho kitafunguliwa kwa umma kwa mara ya
kwanza Jumamosi ya Oktoba 19, 2015, na hivyo kukiwezesha kuanza
shughuli zake, shughuli kubwa ikiwa ni kulea watoto wa kike na kiume kwa
kupitia michezo.
Kwa mujibu wa mipango ya sasa, Kituo hicho kitaanza kwa kutoa mafunzo ya michezo ya soka, mpira wa kikapu (basketball), netiboli, mpira wa wavu (volleyball) na mpira wa magongo (hockey), michezo ambayo viwanja vyake vya kisasa kabisa vimekamilika kujengwa.
Kuhusu soka, JMK Park kitaanza kutoa mafunzo ya mchezo huo kuanzia
Januari 2016 kwa timu za watoto wa chini ya umri wa miaka 16 na miaka 14
na pia kitatoa mafunzo maalum kwa watoto wadogo zaidi wa kati ya miaka
10 na 11.
Mafunzo hayo yatatolewa na makocha wenye weledi na uzoefu kabisa ambao watatolewa na Klabu ya Sunderland.
Kuhusu mpira wa kikapu, mafunzo yataanza kutolewa kwa watoto wa kiume
wa kati ya miaka 12 na 15 kutoka shule 30 za msingi katika Mkoa wa Dar
es Salaam ambazo zitaunda timu 30 zitakazoshiriki katika ligi ya mchezo
huo kila mwaka. Mafunzo ya mchezo huo kwa ajili ya watoto wa kike,
utaanza katika mwaka wa pili wa kufunguliwa kwa Kituo hicho.
Kituo hicho ambacho kitafunguliwa kila siku kwa mwaka mzima pia
kitatoa nafasi kwa watu wazima wapenzi wa michezo kukitumia kwa mujibu
wa taratibu zitakazotangazwa baadaye na wahusika.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
30 Septemba, 2015
Crdt:http://blog.ikulu.go.tz/