Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Wananchi wa Dodoma wamepongeza juhudi za Serikali kupitia mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, wakieleza kuwa mkakati huo unasaidia kuboresha afya, kuokoa muda na kulinda mazingira.
Hayo yamejiri leo tarehe 4 Mei 2026 katika Soko la Mavunde, Chang’ombe, ambapo wananchi wamepata elimu ya nishati safi ya kupikia kwa nadharia na vitendo, ikiwemo mafunzo ya jinsi ya kutumia nishati hizo kwa usahihi na kwa ufanisi zaidi katika shughuli za upishi wa kila siku.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria wamesema kuwa elimu hiyo ya vitendo imewasaidia kuelewa kwa urahisi faida za nishati safi, hususan kupunguza moshi majumbani unaochangia magonjwa ya njia ya hewa na kurahisisha shughuli za upishi.
Aisha Ramadhani, mmoja wa wananchi waliohudhuria na ni mkazi wa Kata ya Chang’ombe, amesema amefurahishwa na kampeni hiyo inayoendelea jijini Dodoma, akibainisha kuwa elimu aliyoipata imemsaidia kubadili mtazamo wake kuhusu matumizi ya nishati, na sasa anaelewa vizuri faida za kutumia nishati safi kama vile kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kuokoa muda pamoja na kuboresha afya ya familia.
Akizungumza katika eneo hilo, mtaalamu kutoka Wizara ya Nishati, Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Nsajigwa Maclean, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mkakati kwa kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa urahisi, kwa gharama nafuu na kuwafikia wananchi wa makundi yote bila kujali kipato au eneo wanaloishi.
Aidha, amefafanua kuwa serikali imeweka juhudi katika kutoa elimu endelevu kwa jamii kupitia mafunzo ya vitendo, ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kina kuhusu matumizi salama ya nishati safi, pamoja na kuhimiza mabadiliko ya tabia kutoka matumizi ya kuni na mkaa kwenda nishati mbadala inayolinda afya na mazingira.
Wananchi waliohudhuria wameeleza kuridhishwa na juhudi hizo za Serikali na kuahidi kuendelea kuhamasishana juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo yao wanayoishi.












EmoticonEmoticon