“RC MAGALULA: MSIWAFUMBIE MACHO WANAOCHAFUA TAALUMA YENU”

September 20, 2015
AMINA OMARI TANGA.

MKUU wa Mkoa wa Tanga,Said Magalula ameitaka bodi ya Usajili wabunifu wa Majengo na wakadiriaji wa Majenzi nchini kutowafumbia macho baadhi yao wanaotaka kuchafua sifa ya taaluma hiyo kwa kushindwa kutimiza wajibu wao badala yake wahakikisha wanachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni.

Magalula alitoa wito huo juzi wakati akifungua semina endelevu ya 24 ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji  Majenzi inayofanyika mjini hapa iliyowahusisha wataalamu kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.

Alisema kuwa uchukuaji wa hatua hizo kali utawafanya wenye tabia za aina hiyo kuacha mara moja kutokana na kuwa endapo watafanya hivyo wataweza kukumbana na adhabu ikiwemo kulipishwa faini ili iweze kuwa fundisho kwa wengine.

  “Nisema tu hatua mnazozichukua katika kusimamia sheria pamoja na kuwafutia usajili na kuwalipisha faini wale wanaokiuka maadili ya taalumu itasaidia hii ni njia nzuri kwa sababu itaongeza ufanisi kwa baadhi yao kuepuka kufanya vitendo visivyotakiwa “Alisema RC Magalula.

Alisema kuwa katika mkakati wa kuwajengea uwezo wataalamu wazawa,aliwashauri kuungana na kuomba kazi kwa pamoja ikiwemo kuacha ubinafsi kwani hilo limekuwa tatizo kubwa kwa watanzania wengi hali ambayo imepelekea kulalamika kuwa serikali kuwa haiwajali.

Aidha aliwataka wataalamu kuhakikisha wanajitangaza kwa kufuata sheria pamoja na kuonyesha jamii kazi zao zinazotokana na ubora ili kuweza kuwapa utofauti wa kazi iliyofanywa na mtaalam na ile iliyofanywa na mtu asiyekuwa na taaluma.

Mkuu huyo wa mkoa aliipongeza bodi hiyo kwa kuanza kujenga mahusiano na taasisi zingine za nchi za Afrika Masharika na nchi za SADC kwa lengo la kupata uzoefu zaidi katika utekelezaji wa majukumu yenu itakayowezesha kupanua wigo wa kupata kazi.

  “Nipongeza juhudi hizi nikiamini kuwa mahusiano hayo yatakuwa ya manufaa kwenu kama bodi na wataalamu wenu …lakini pia kwa manufaa kwa Taifa kwa ujumla kwa kuzingatia nia dhabiti ya serikali kushirikiana na Mataifa mbalimbali katika kukuza Uchumi…

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mwenyekiti wa Bodi ya ya wabunifu wa Majengo na wakadiriaji wa Majenzi,Tonnie Ambwene Mwakyusa alisema kuwa lengo la semina hiyo ni kuwakutanisha wataalamu katika sekta ya ujenzi hususani wabunifu wa majengo,wakadiriaji majenzi,wataalamu wa mpango wa miji na wahandisi ili kujifunza na kubadilisha ujuzi.

Alisema kuwa katika utendaji kazi wa wataalamu wao wamekuwa wakikumbana changamoto mbalimbali zikiwemo uelewa mdogo kwa baadhi ya waendelezaji kuhusu umuhimu wa kutumia wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi katika kubuni na kutekeleza miradi yao.

Aliongeza kuwa bodi hiyo kwa kuliona hilo inaendelea kuchukua hatua za kutembelea miradi ya ujenzi na kuelimisha waendelezaji wa miradi na wadau wengine ambao wanakiuka sheria kwa ikiwemo kuwachukulia hatua kali kwa kuwasimamisha ujenzi wa mradi na kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »