📌 *Ni sehemu ya ushirikishwaji Taasisi za Umma katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.*
📌 *Watumishi watakiwa kuwa Mabalozi wa kuhamasisha Nishati Safi ya Kupikia.*
Katika jitihada za kuimarisha utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Wizara ya Nishati kupitia kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia kimetoa mafunzo kwa watumishi 133 wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Akiwasilisha taarifa ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya nishati safi ya kupikia, Mhandisi Anitha Ringia kutoka Wizara ya Nishati ameeleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa juu ya faida za nishati safi, ikiwemo kupunguza athari za kiafya na kimazingira zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa katika kupikia huku akiwaeleza Watumishi kuwa matumizi ya nishati safi ni sehemu ya ajenda ya kitaifa ya kulinda mazingira na kuboresha ustawi wa wananchi.
“Mafunzo haya yanaonesha dhamira ya Serikali katika kuhakikisha Taasisi za Umma zinakuwa mfano wa kuigwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia na kupitia ninyi watumishi mtafanya uhamasishaji utakaoleta mwamko mpana zaidi kitaifa katika matumizi ya nishati safi na hatimaye kupunguza utegemezi wa nishati zisizo rafiki kwa mazingira." Amesema Ringia
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa urahisi, na inawanufaisha Watanzania wote ili kuhakikisha ifikapo 2034 asilimia 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Aidha Kupitia mafunzo hayo Mha. Ringia ametoa wito kwa watumishi wote wa umma kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia huku akiwahimiza kutumia uelewa walioupata kuwa mabalozi katika maeneo yao ya kazi na jamii wanazoishi.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Nishati Bi. Neema Mbuja ameeleza kuwa kupitia Mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa Mwaka 2024 uliundwa Mkakati wa Kitaifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa umma na taasisi kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupika ili kufanikisha malengo ya Taifa ya kuhakikisha wananchi wanapika kwa kutumia nishati safi, salama na rafiki wa mazingira.
" Mkakati wa mawasiliano umetokana na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na lengo lake ni kutoa elimu na kuwawezesha watanzania kupata taarifa sahihi juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, elimu hii wanaipata kupitia njia mbalimbali ikiwemo redio, televisheni, mitandao ya kijamii na maonyesho ya wazi, pia kupitia mkakati huu tumeendelea kuhamasisha umma na kufanya kampeni mbalimbali sambamba na kauli mbiu isemayo Nishati Safi ya Kupikia Okoa Maisha na Mazingira." Amesema Bi. Mbuja
Aidha Bi. Mbuja ameongezea kuwa Mkakati wa Mawasiliano umelenga kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia vyombo vya habari, mikutano ya hadhara na mafunzo mbalimbali lakini pia kushirikisha kila mtanzania kulingana na rika na nafasi ya kila mtu mmojammoja kwa lengo la kuhakikisha ujumbe uliokusudiwa unawafikia Watanzania wote.
Naye Mhandisi Mwandamizi wa Utafiti kutoka Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO) Mha. Catherine Mwegoha ameeleza kuwa TANESCO imeendelea kutoa elimu juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia hususani nishati ya umeme kwani ni salama na nafuu kwa watumiaji hususani kwa kutumia majiko kama “Pressure Cooker” na “Induction cooker” (Jiko Janja ) kwani majiko haya yamefanyiwa utafiti na hupika vyakula vya asili kama vile ugali maharage makande na ndizi kwa kutumia umeme kidogo ukilinganisha na majiko mengine.
Akifunga Mafunzo hayo Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - UTUMISHI ambaye ni Mkurugenzi wa uendelezaji Sera wa Ofisi hiyo Bw. Cyrus Kapinga amesisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kuongeza kasi ya matumizi ya teknolojia bora na rafiki kwa mazingira kwa kuendelea kuchangia juhudi za Serikali katika kupunguza hewa ukaa na kulinda afya za wananchi.
“Sisi kama watumishi wa Umma ni sehemu ya jamii tunaopaswa kuhakikisha tunatekeza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwani kila Wizara ina jukumu la kuhakikisha watumishi wanatumia nishati safi hivyo katika kutekeleza hilo tutaanzisha mkakati wa ndani wa namna tutakavyopata majiko ya positive cooker kama Taasisi na kuhakikisha kila Mtumishi anapatiwa jiko hilo ili kila Mtumishi aweze kuendana na mabadiliko hayo.”Amesisitiza Bw. Kapinga
Katika mafunzo hayo Watumishi walipata fursa ya kuona namna jiko janja (Induction Cooker) linavofanya kazi kwa ufaisi na kuokoa muda bila kutumia gharama kubwa.

.jpg)

.jpg)


EmoticonEmoticon