Mkurugenzi
Uendeshaji na Utumishi wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo
Joseph Kilangi akitoa hutuba yake ya ufunguzi katika Semina ya
majadiliano ya “Rasimu ya Sera ya Urithi wa Utamaduni” iliyofanyika
Forodhani Mjini Zanzibar,kulia kwake ni Mkurugenzi wa Uendeshaji na
Utumishi, Sera na Utafiti wa Wizara hiyo na kushoto ni Mkurugenzi wa
Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Dkt. Amina Ameir Issa.
Mwalimu wa Historia Chuo Kikuu cha Taifa Suza Bi Zainab Othman akitoa
mawazo ya kuiboresha Rasimu hiyo katika Semina ya kuijadili ‘Rasimu ya
Sera ya Urithi wa Utamaduni’ Semina hiyo iliyofanyika Forodhani Mjini
Zanzibar.
Mkurugenzi
wa Sanaa Zanzibar Mdungi Ussi akichangia Rasimu ya Sera ya Urithi wa
Utamaduni ambapo pamoja na mambo mengine ameshauri Sera hiyo
isiingiliane na Sera zingine.Picha na Faki Mjaka
Mkurugenzi
wa Idara ya Makumbusho na mambo ya kale Dkt Amina Ameir Issa
akiwashukuru Washiriki kwa michango yao katika Semina ya Majadiliano ya
Rasimu ya Sera ya Urithi wa Utamaduni iliyofanyika Forodhani mjini
Zanzibar,kulia kwake ni Mkurugenzi wa Uendeshaji, Sera na Utafiti wa
Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Mashaka Hassan
Mwita na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Magofu Zanzibar Abdallah Khamis
Magofu-Picha na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
………………………………………………………………………………….
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Urithi wa Utamaduni umeelezwa kuwa
ni moja kati ya Vitega uchumi muhimu ambapo kama utatumika vyema
utapelekea mchango mkubwa kwa Wananchi na Serikali kwa ujumla.
Mchango huo unaweza kuwepo katika Nyanja mbalimbali ikiwemo ya Utalii,Teknolojia, Utafiti na Elimu.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa
Idara ya Mambo ya Kale Dkt. Amina Ameir Issa wakati wa mjadala wa Rasimu
ya Sera ya Urithi wa Utamaduni uliofanyika Forodhani Mjini Zanzibar.
Amesema Nchi nyingi duniani
huingiza mapato kutokana na utalii ambao kwa kiwango kikubwa hutegemea
vivutio vinavyotokana na urithi wa utamaduni.
Dkt Amina ameeleza kuwa Utalii
huchangia na kuongeza pato la Wananchi kutokana na kuuza bidhaa na
huduma mbalimbali kwa watalii zinazotokana na Urithi wa Utamaduni
zikiwemo Sanaa, Mikoba na Milango.
Amesema kukamilika kwa Sera hiyo
na utekelezaji wake kutawezesha watu kutambua na kuthamini utu wao,
historia na utamaduni wao jambo ambalo litapelekea watu hao kuamua
kuyalinda maeneo ya Uhifadhi na utamaduni wao.
“Watu hufurahia kushuhudia Urithi
wa Utamaduni wenye mahusiano na historia ya jamiii mablimbali kama vile
maendeleo ya sayansi, mabadiliko ya sura ya nchi na viumbe,aina ya
uburudishaji,ukarimu, huba na maisha ya watu kwenye maeneo hayo” Alisema
Dkt Amina.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Uendeshaji na Utumishi wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo
Joseph Kilangi amesema kukamilika kwa Sera ya Urithi wa Utamaduni
kutaisaidia Serikali kuanzisha Utalii wa Utamaduni wa Zanzibar ambao
utakuwa ni kivutio kwa Wenyeji na Wageni mbalimbali nchini.
Amesema hatua hiyo ni miongoni mwa
jitihada mbali mbali zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha Sekta
hiyo ambayo ndio tegemeo la Uchumi wa nchi.
Amesema Zanzibar ina utamaduni
wake ambao unatofautiana na Nchi nyingine hivyo ipo haja ya Utamaduni
huo kuenziwa na kufanywa uwe kivutio kwa Wageni ili waweze kuja nchini
kwa ajili ya kujionea utamaduni huo.
“Zanzibar tuna utamaduni wetu wa
Asili ikiwemo Mavazi, Tabia njema, Ukarimu, kupendana,amani na
utulivu,mambo ambayo tukiyaratibu vyema katika Sera hii itakuwa kivutio
cha Utalii’’ Alisema Mkurugenzi Kilangi.
Kwa upande wao Washiriki wa Semina
hiyo wameipongeza Serikali kwa uamuzi wake na kuomba kufanyika kwa
majadiliano mapana kutoka kwa Wadau mbali mbali hasa wa Vijijini ambao
pia Sera hiyo inawahusu.
Hata hivyo Wachangiaji hao
wameiomba Idara ya Makumbusho ambao ndio Wasimamizi wakuu wa Sera hiyo
kuhakikisha Sera hiyo haipingani na Sera nyingine.
EmoticonEmoticon