Hatimaye
wiki moja iliyopita Mwadui ya Shinyanga ilitwaa ubingwa wa Ligi Daraja
la Kwanza na kuzipiku timu nyingine tatu zilizofanikiwa kupanda ligi
msimu ujao. Timu zingine zilizorejea Ligi Kuu ni African Sports ya
Tanga, Majimaji FC ya Songea na Toto Africans ya Mwanza.
Timu
hizo zilimaliza kwenye nafasi mbili za juu za makundi mawili (Kundi A
na B) katika mechi za Ligi Daraja la Kwanza kwani kila kundi lilitakiwa
kutoa timu mbili zitakazopanda daraja.
Kwa upande wa Kundi A, African Sport na Majimaji zilifuzu wakati kwenye Kundi B zilifuzu timu za Mwadui FC na Toto Africans.
Timu
hizo zinazomilikiwa na wakazi wa maeneo timu zinapotokea, siyo ngeni
kwenye Ligi Kuu kwani kwa miaka ya nyuma timu zote zilishawahi kushiriki
Ligi Kuu kabla ya kushuka. Hivi sasa timu hizo zinatarajiwa kutoa
upinzani mkubwa kwenye Ligi ikiwamo kuwania ubingwa wa ligi. Timu hizo
ziko kama ifuatavyo:
Majimaji FC ‘Wanalizombe’
Ni
miongoni mwa timu ambazo zilikuwa tishio nchini katika miaka ya 1980
hadi iliposhuka daraja mwaka 2000. Kisha ikarejea tena mwaka 2009 na
kushuka mwaka 2010. Mashabiki wengi wa soka nchini wanaikumbuka Maji
Maji ya Songea maarufu kwa jina la Wanalizombe.
Maji
Maji ambayo ilianzishwa mwaka 1977 ilipata umaarufu mkubwa mwaka 1980,
mwaka ambao timu hiyo ilipata nafasi ya kushiriki kwa mara ya kwanza
Ligi Daraja la Kwanza ambayo kwa sasa ni Ligi Kuu.
Uwezo wa timu hiyo
Kocha
Mkuu wa Majimaji, Hassan Banyai anasema, “Mafanikio ya timu yangu
yalitokana na kufanya kazi kwa umoja, nilishirikiana na wachezaji, pia
umoja uliokuwapo kati ya viongozi, benchi la ufundi, wafadhili na
mashabiki ulitufanya twende vizuri na tufanikiwe.”
Mipango kwenye Ligi Kuu
Kocha
wa Majimaji, Banyai anasema kuwa ndoto zake kwa timu hiyo ni kuchukua
ubingwa wa ligi ndani ya muda mfupi. “Tuliwahi kuchukua ubingwa wa
Muungano miaka ya nyuma, hivi sasa tunataka kurudisha heshima yetu ya
hapo awali kwa kuchukua ubingwa mapema,” alisema kocha huyo.
African Sport ‘Wanakimanumanu’
Hii
ni moja ya timu ambazo ziliwahi kufanya vizuri miaka ya nyuma na
kujiwekea heshima. Mpinzani wake mkubwa ni Coastal Union iliyopo Ligi
Kuu. African Sport iliwahi kutwaa ubingwa wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania huku ikitamba kati ya miaka ya 80 na 90.
Ilitwaa kombe hilo mwaka 1988, lakini ikateremka daraja miaka mitatu baadaye, mwaka 1991.
Kocha
Mkuu wa timu hiyo, Joseph Lazaro ambaye ni beki wa kushoto wa zamani wa
Coastal Union na Yanga anasema katika mpango wao wa kutengeneza timu
mpya amepanga kuongeza wachezaji saba tu kwenye usajili.
“Tuna
imani kubwa na uwezo wa hawa vijana wetu, yatakuwapo maboresho kidogo
tu, Tunajua Ligi Kuu ina ugumu wake, kikubwa kwetu kitakuwa ni
maandalizi ya mapema,” anasema.
Nguvu ya timu yake
Kocha
wa timu hiyo, Joseph Lazaro anasema kuwa kilichowabeba zaidi ni umri
mdogo wa wachezaji ambao uliwawezesha kucheza vizuri. Pia ushirikiano na
nidhamu ya mazoezi.
“Pia tulijiandaa vyema kwa kufanya zaidi mazoezi na kucheza kama timu,” anasema Lazaro.
Uongozi ulivyojipanga
Katibu
Mkuu wa timu hiyo, Khatibu Enzi anasema,”Tunataka kurudisha historia ya
nyuma kwa kupanda ligi na kuchukua ubingwa kama tulivyofanya mwaka
1988, hakuna kinachoshindikana kwetu. Tuna nguvu na umoja katika timu
yetu, ugumu ulikuwa kupanda, lakini sasa tumefika.”
Toto Africans ‘Wanakishamapanda’
Toto
Africans imepanda Ligi Kuu baada ya juhudi za muda mrefu. Klabu hiyo
ilishuka daraja kutokana na ukata ulioikabili mwaka 2013. Kabla ya
kushuka daraja miaka miwili iliyopita, Toto ilikuwa imecheza misimu sita
mfululizo kwani ilikuwapo kwenye ligi tangu msimu wa 2007/08. Hivi sasa
timu inaongeza utamu wa soka kwa Kanda ya Ziwa baada ya Kagera Sugar,
Stand United na Mwadui nao kuwa na nafasi kwenye ligi.
Nguvu za timu hiyo
Kocha
Mkuu wa Toto, John Tegete anasema, “ Kilichotubeba kupanda Ligi Kuu ni
usajili mzuri, licha ya umaskini wa timu yetu tulitafuta wachezaji bora
wenye viwango na uzoefu mzuri.”
Mipango kwenye ligi
Kocha
Tegete anasema watafanya marekebisho kwenye nafasi mbalimbali ili
kuhakikisha ligi ya msimu ujao wanafanya vyema na kuleta ushindani.
Mwadui FC
Kifedha
wako vizuri na wako chini ya udhamini wa mgodi wa almasi wa Petra
Diamonds -Wiliamson uliopo Mwadui Shinyanga. Timu hii ilitamba msimu
uliopita kwenye Ligi Daraka la Kwanza, lakini ikashindwa kwa pointi
mbele ya majirani zao Stand United.
Mwadui FC ni moja ya timu kongwe nchini, Ilicheza Ligi kuu kati ya miaka ya 70 na kisha kushuka kwenye miaka ya 80.
Moja ya mafanikio ya timu hiyo ni kufika nusu fainali ya kusaka ubingwa wa Tanzania kwa kuitoa Yanga kwa mikwaju ya penalti.
Nguvu ya timu
Kocha
Mkuu wa Mwadui FC, Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ anasema, “ Timu yangu
ilikuwa bora kwenye idara zote hasa kwenye idara ya ushambuliaji kwani
ilifunga mabao mengi zaidi kuliko timu zingine zilizocheza na sisi.
“Usajili
wa wachezaji wazoefu kama Athumani Iddi ‘Chuji’, Uhuru Selemani, Razack
Khalfani uliisaidia timu, kimsingi usajili ndiyo uliochangia Mwadui
kupanda Ligi Kuu,” anasema Julio.
Mipango kwenye Ligi
Kocha
Julio anasema,”Mimi na timu yangu tumekuja kusaka ubingwa wa Ligi Kuu
na kama siyo hivyo basi nikichemka sana niwe kwenye nafasi ya tatu.
EmoticonEmoticon