NA HAMISI RAMADHANI,MKINGA.
BAADHI ya wakazi wa Kata ya Mhinduro
iliyopo wilaya ya Mkinga mkoani Tanga wamesusia kushiriki katika shughuli zote
za maendeleo huku wengine wakitishia kurudisha kadi za Chama cha Mapinduzi
(CCM) kufuatia serikali kupiga marufuku shughuli za kundi la watu wanaodaiwa
kufichua wachawi maarufu kama Lambalamba.
Hasira hiyo imefuatia baada ya wananchi
wanaoishi katika vijiji vilivyomo ndani Kata hiyo kuchanga fedha zaidi ya
shilingi laki nane kwa ajili ya kuwaleta Lambalamba kwenye maeneo yao ili
aweze kuwaondolea kero ya vitendo vya kishirikina ambavyo wamedai kuwa vimekuwa
vikichangia kurudisha nyuma jitihada zao za kujiletea maendeleo.
Zoezi la mgomo dhidi ya shughuli
zote za maendeleo limeingia siku ya saba tangu kundi hilo la Lambalamba kupigwa
marufuku na serikali ili kuzuia uvunjifu wa amani unaoweza
kujitokeza miongoni mwa jamii.
Kutokana na mgomo huo Mkuu wa wilaya
ya Mkinga Mboni Mgaza alijikuta akihutubia watoto wadogo na watumishi wa serikali
tu kwenye sherehe za zoezi la upandaji
miti zilizofanyika katika Kijiji cha Churwa wilayani humo baada ya wananchi
kukataa kutoka majumbani mwao.
“Mheshimiwa Mkuu wa wilaya hii
iliyojitokeza leo ndiyo hali halisi iliyopo hapa Kijijini tangu serikali
ilipopiga marufuku kuendelea kwa zoezi la Lambalamba wananchi hawa wamekuwa
wakikataa kushiriki shughuli zote za maendeleo “,alisema Anthon Mlola Mwenyekiti
Serikali Kijiji cha Churwa.
Akielezea hatua hiyo baada
ya wananchi kususia mkutano wake pamoja na shughuli za maendeleo
Mkuu wa wilaya ya Mkinga Mgaza alisema serikali itaendelea na msimamo
wake wa kupiga marufuku watu hao wanaojiita ni watoa uchawi ikiwa ni hatua moja
wapo ya kupingana na vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani.
“Pamoja na mgomo huo lakini niwaombe
wananchi watambue kuwa serikali haitakubaliana na maamuzi hayo ya kuwaleta
lambalamba na kusababisha uvunjifu wa amani hivyo nawaomba viongozi wa Kamati
ya ulinzi na usalama kwa ngazi zote kuhakikisha wanaendelea kusimamia agizo
hili la kupiga marufuku vikundi vya aina hii”,alisema Mgaza.
Kufuatia hatua hiyo Askari Mgambo na
wale wa kutoka kikosi cha 838 KJ cha Maramba JKT walilazimika kushiriki zoezi
la upandaji miti ambapo zaidi ya miti 39,000 ilipandwa katika misitu mitatu ya
hifadhi ya asili wilayani humo.
EmoticonEmoticon