DC DENDEGO ASIKITISHWA NA BAADHI YA WAZAZI KUWAOZA MABINTI ZAO WALIOPO MASHULENI.

April 14, 2014
(mkuu wa wilaya ya Tanga,Halima Dendego wa kwanza kushoto akisikiliza maelekezo toka kwa mwanafunzi wa kidato cha sita wa shule ya sekondari st.Christina wakati alipotembelea chumba cha maabara ya sayansi shuleni hapo kwenye mahafali
Salim Mohammed,TANGA
MKUU wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego amesikitishwa na baadhi ya wazazi kuwaoza mabinti zao wakati wako katika masomo na kutoa ovyo kuwa mtu yoyote atakaebainika kumuachisha masomo mtoto wake atapambana na sheria.



Ameyasema hayo  wakati wa mahafali ya 12 shule ya sekondari ya St Christina iliyoko Kange Maziwa mjini hapa na kusema kuwa tabia ya wazazi kuwapa waume mabinti zao wakati wakiwa shuleni inasikitisha na hivyo ofisi yake kuadhimia kuikomesha.



Alisema kitendo hicho kinawanyima mabinti hao haki ya kupata elimu na kuweza kumkomboa mwanamke katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii hasa kwa wakati uliopo  sasa wa sayansi na teknolojia ulimwenguni.


“Kupitia mahafali haya ya 12 ya shule hii ya St Christina  tukiwa na  mama na wababa wetu natoa wito kukomeshwa watoto wetu wa kike kupewa waume wakati wanasoma----hili binafsi nitalivalia njuga kuhakikisha halitendeki” aliongeza na kusema


“Nadhani hao wazazi wenye tabia hii kwa kweli  wako na jambo kama sio maslahi ni shida za papo kwa papo---sera ya mwanamke kuongoza na kuweza bila kuwezeshwa haijawafika baadhi ya wazazi na hivyo nawataka kuelimika” alisema Dendego


Alisema ofisi yake haitomvumilia mzazi wala mlezi yoyote atakaebainika kumuoza binti yake wakati yuko katika masomo na hivyo atahakikisha tabia hiyo inakomeshwa ili kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu na kuweza kuleta mapinduzi ya ukombozi wa wanawake katika kujiletea maendeleo.


Akizungumzia wazazi kuwabidiisha watoto wao katika elimu, Dendego aliwataka kuwa na ada ya kuwafuatilia maendeleo yao shuleni na kuacha kuwaruhusu kushiriki katika shughuli ambazo zinaweza kumtoa kimawazo katika masomo yake.


Alisema kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwatumia vibaya watoto vipindi vya likizo kwa kuwapa kazi ambazo ziko nje ya uwezo wao pamoja na kuwashirikisha katika biashara na kusahau kuwa vipindi hivyo ni vya maandalizi ya kujiandaa na masomo yalioko mbeleni kwao.


“Ni jambo la kushangaza kuona vipindi vya likizo kwa wanafunzi wazazi wanafurahia kama wamepata kitu kizuri---kumbe furaha yao ni kuwatumikisha katika kazi ambazo ziko nje ya uwezo wao na kusahau kuwa nihatari” alisema Dendego


Alisema ili kuwawezesha watoto kufanya vizuri vipindi vyote vya masomo yao ni jukumu la wazazi kuwabidiisha katika masomo vipindi vya likizo ili karo wanazolipa faida yake iweze kuonekana na kuacha kuzilaumu shule kuwa hazisomeshi.

                                            
   Mwisho

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »