Tembo wakivinjari hifadhi ya Taifa ya Ruaha
Viongozi
wa makundi ya tembo kati ya 20 na 30 waiishio kwenye ikolojia ya Ruaha
wanatarajiwa kufungwa vifaa maalumu kwa ajili ya kufuatilia nyendo zao
ikiwa ni mkakati wa kuwalinda dhidi ya ujangili.
Ikolojia
ya Ruaha inayojumuisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA) ndio yenye
tembo wengi kuliko eneo jingine kwa Tanzania kwa sasa hivyo zinahitajika
juhudi za pamoja katika kuwalinda tembo hao.
Akizungumza na waandishi wa habari,
Mratibu wa Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi
Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwel Ole Meing'aki alisema eneo hilo
lina tembo wanaofikia 20,090 ambao ni wengine kuliko eneo jingine.
Mpango huo utakaotumia teknolojia ya
kisasa ya mawasiliano ya setilaiti ya utambuzi wa jiografia ya maeneo
(GPS) na kompyuta utatekelezwa kupitia SPANEST ikiwa ni mkakati wa
kuimarisha ulinzi dhidi ya majangili.
"Kwa kawaida tembo huongozwa na jike
mkubwa ambaye anajua njia na kuelekeza kundi zima na ndio watakaofungwa
vifaa hivyo. Zoezi hili linahitaji gharama kubwa kwa kuwa litahusisha
wataalamu wengi" alisema.
Alisema awali Selous ndio iliyokuwa
ikiongoza kwa kuwa na makundi makubwa ya tembo hapo awali lakini
kutokana na zoezi la kuhesabu lililofanyika mwaka jana kwa ufadhili wa
mradi huo imebainika kuwa Ruaha inaongoza.
"Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa
Wanyama Tanzania (TAWIRI) ambao waliendesha zoezi la kujua idadi ya
tembo eneo la Ruaha ni tembo 20,090 waliopo idadi ambayo huenda miaka
michache iliyopita ilikuwa zaidi ya 30,000", alisema.
Alisema tembo hao watafungwa 'Color'
ambazo zitakuwa na vifaa maalumu vitakavyokuwa vikionesha mahali walipo
kwa nyakati tofauti.
Alisema sambamba na kufanya zoezi hilo
Shirika la Maendeleo la Kimataifa (UNDP) kupitia SPANEST litaimarisha
mfumo wa mawasiliano kwenye hifadhi hizo ili iwe rahisi kwa askari,
kituo na kituo kuweza kuwasiliana kwa urahisi.
Mwenyekiti wa Mpango wa Matumizi Bora
ya Maliasili Idodi na Pawaga (MBOMIPA), unaojumuisha vijiji vyote
vinavyozunguka RUNAPA, Philip Mkumbata alisema mpango huo ni mzuri na
utasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ujangili hasa dhidi ya tembo.
EmoticonEmoticon