TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Aprili 2, 2014
WACHEZAJI NGORONGORO HEROES WAAHIDI USHINDI
Nahodha
wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro
Heroes), Aishi Manula amesema wamejipanga kwa ajili ya kupata ushindi
kwenye mechi dhidi ya Kenya itakayochezwa Jumapili (Aprili 6 mwaka huu)
katika mji wa Machakos.
Akizungumza leo (Aprili 2 mwaka huu)
kwenye hafla ya kukabidhiwa bendera kwa timu hiyo kwenye ofisi za
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Manula ambaye pia anaidakia
timu ya Azam alisema lengo lao ni kufanya vizuri kwenye mechi hiyo.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya
Michezo, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juliana Yasoda
akikabidhi bendera hiyo, aliwataka wachezaji hao kujituma na
kutanguliza uzalendo mbele bila kusahau kuwa mchezo wa mpira wa miguu ni
ushirikiano.
Alisema Tanzania ina wachezaji wengi
wenye vipaji, hivyo waliopata fursa ya kuwemo Ngorongoro Heroes wakati
huu wajue kuwa wamepata bahati, na wanatakiwa kufahamu kuwa wao ni
wawakilishi wa Tanzania, na Watanzania wana kiu ya kusikia matokeo ya
mechi hiyo.
Ngorongoro Heroes inayofundishwa na John
Simkoko inaondoka kesho (Aprili 3 mwaka huu) saa 4.30 asubuhi kwa ndege
ya Kenya Airways, na mara baada ya kuwasili itakwenda moja kwa moja
kwenye hoteli ya Garden iliyopo Machakos ambayo ndiyo imepangiwa kufikia
na Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF).
Wachezaji waliopo kwenye msafara huo
unaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF), Ayoub Nyenzi ni
Abrahman Mohamed, Aishi Manula, Ally Idd, Ally Mwale, Athanas Mdamu,
Ayoub Semtawa, Bryson Raphael na Edward Manyama.
Wengine ni Gadiel Michael, Hamad Juma,
Hassan Mbande, Ibrahim Ahmada, Idd Ally, Kelvin Friday, Michael Mpesa,
Mohamed Ibrahim, Mudhathir Yahya, Pato Ngonyani, Peter Manyika na Salum
Mineli.
TIMU YA WATOTO WA MITAANI YACHACHAFYA BRAZIL
Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania
kutoka Kituo cha Mwanza inaendelea vizuri katika mashindano ya Kombe la
Dunia kwa Watoto wa Mitaani yanayoendelea Rio de Janeiro nchini Brazil
ambapo katika mchezo wake wa kwanza ilitoka sare ya mabao 2-2 na
Burundi.
Juzi (Machi 31 mwaka huu), timu hiyo
inayoongozwa na mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kutoka Mkoa wa Mwanza, John Kadutu ilicheza mechi mbili.
Katika mechi ya kwanza iliifunga Argentina mabao 3-0 na baadaye ikailaza
Nicaragua mabao 2-0.
Michuano hiyo ya siku kumi inashirikisha timu kumi. Mbali ya Tanzania, nyingine ni
Argentina, Burundi, India, Kenya,
Liberia, Marekani, Mauritius, Misri na Pakistan. Kwa wasichana ni Afrika
Kusini, Brazil, El Salvador, Indonesia, Msumbiji, Nicaragua,
Philippines, Uingereza na Zimbabwe.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
EmoticonEmoticon