April 03, 2014

FIFA YAMUAMBIA MALINZI NA WENZAKE; TUNATAKA MCHUKUE KOMBE LA DUNIA HARAKA

Na Mwandishi Wetu, Johannesburg 
KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Jerome Valcke amezungumzia uwekezaji wa FIFA kwa CAF na majukumu ya bodi hiyo ya soka kukuza mpira barani Afrika na kusema kwamba anataka kuona bara hilo linatwaa Kombe la Dunia haraka.
“Shirikisho la Soka Afrika ni mwanachama muhimu sana wa FIFA na tutafanya kila kitu kuwasaidia wanachama wa CAF. Tunataka nchi ndani ya CAF kuzigeuza timu kuwa za kulipwa, kuweka mikakati mizuri na kuwa na mipango mizuri ya uwekezaji katika soka ya vijana,” amesema Valcke leo katika ufunguzi wa semina ya siku tatu ya CAF na FIFA kwenye ukumbi wa hoteli ya Sandton Convention Centre. 

Ufunguzi semina ya FIFA na CAF nchini Afrika Kusini leo
“Huo ndiyo msingi wa timu yoyote nzuri,” amesema Valcke na kuongeza anataka kuona Afrika inatwaa Kombe la Dunia muda si mrefu.
Kwa upande wake, Makamu wa kwanza wa rais wa CAF, Suketu Patel amesema  FIFA imewekeza mabilioni ya fedha kusaidia maendeleo ya soka Afrika na huu ni wakati mwafaka wa bara hili kuinuka kisoka. 
“Afrika ni imara katika kila nyanja. FIFA imewekeza dola za Kimarekani nusu bilioni barani Afrika kupitia Goal Project, Win with Africa na programu za World Cup Legacy. Sasa Afrika inahitaji kuhakikisha inazungumza maendeleo,” amesema Patel leo katika ufunguzi wa semina ya siku tatu ya CAF na FIFA kwenye ukumbi wa hoteli ya Sandton Convention Centre. 
Semina hiyo imewakutanisha pamoja Marais, Makatibu Wakuu na Wakurugenzi kutoka nchi 27 za Afrika, na Tanzania imewakilishwa na Rais wake, Jamal malinzi, Katibu Mkuu Celestine Mwesigwa na Mkurugenzi Salum Madadi.
Patel amesema kwamba Afrika inahitaji kuwa mwepesi katika uanzishaji wa mfumo wa Club Licensing ambao ni njia nzuri ya kushikilia mustakabali wa soka barani.
“Club Licensing ni jambo la kupewa kipaumbele katika soka yetu ili iwe na hadhi, uimara na uwazi. Mfumo mpya wa Club Licensing ni msingi wa maendeleo katika kila nchi na tunahitaji kuwa wepesi katika kuuanzisha kwenye bara letu,” alisema Patel.
Mwenyeji wa semina hiyo, Danny Jordaan Rais wa Chama cha Soka Afrika Kusini (SAFA) amesema ili soka ya Afrika isonge mbele, inahitajika kupanua maendeleo ya miundombinu na masuala ya kibiashara. Soka inakuwa biashara kubwa hivi sasa na inahitaji misingi hiyo, yenyewe tu itakuwa biashara rasmi,”alisema Jordaan.
Ufunguzi semina ya Makamisaa mjini Cairo leo

Wakati huo huo: Katibu wa CAF, Hicham El Amrani alikuwa mjini Cairo nchini Misri leo kufungua semina ya Makamisaa wa mechi na akauelezea kwa mapana marefu mfumo wa Club Licensing na mfumo wa uongozi wa Kielektroniki.
Semina hiyo ya siku mbili itazungumzia na kufafanua majukumu na haki za Maofisa hao katika maeneo yote yanayohusu mechi, ikiwemo uandaaji wa mechi na kujadili mada mbalimbali ikiwemo sheria na kanuni za mashindano ya CAF, Masoko, Vyombo vya Habari na Urefa.  Jumla ya washiriki 110 kutoka nchi 56 wamehudhuria.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »