
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mkazo katika kuwawezesha vijana na kuzipa kipaumbele shughuli zao za uzalishaji ili kuongeza mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo wakati alipotembelea mabanda ya maonesho katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana 2026, yanayofanyika katika Viwanja vya Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa na kuona bunifu mbalimbali za vijana.
Amesema dhamira ya Serikali ya kuwawezesha vijana inaonekana kupitia hatua mbalimbali zinazochukuliwa, ikiwemo kutenga Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi.
“Mara tu baada ya kumalizika kwa uchaguzi, Rais Dkt. Samia alitenga Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwezesha shughuli za vijana, na tunaona matunda yake,” amesema Dkt. Mwigulu.
Ameeleza kuwa Serikali inafurahishwa na mwitikio wa vijana katika kujikita kwenye shughuli za uzalishaji, hali inayoonesha kuongezeka kwa matumizi ya fursa zinazopatikana kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuongeza bajeti kwa ajili ya shughuli za uzalishaji za vijana ili kupanua wigo wa wanufaika na kuwawezesha vijana wengi zaidi kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
“Vijana endeleeni kukua zaidi kimtaji ili uchumi wa Tanzania uweze kushikwa na Watanzania. Hongereni sana,” amesisitiza.
Kadhalika, Dkt. Mwigulu amempongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, kwa kutekeleza kwa vitendo maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Wizara ya Vijana kuwa Wizara ya uzalishaji.





EmoticonEmoticon