********
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Profesa Palamagamba Kabudi amejibu baadhi ya hoja za watu
wanaopendekeza muundo wa serikali mbili na kusema Serikali ya Zanzibar
ndiyo iliyoanza kutaka serikali tatu mwaka 1984.”
Aidha, amewashangaa wanaolibeza jina la Tanganyika
kutumika serikalini kwa madai kuwa jina hilo siyo haramu kwa kuwa limo
ndani ya Katiba ya sasa.
Alisema kuwa wakati huo madai ya serikali tatu
yalitolewa na Zanzibar na kusimamiwa na Rais aliyekuwa pia Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Alhaji Aboud Jumbe.
“Hoja ilipelekwa pia kwenye Baraza la Wawakilishi,
Brigedia Mstaafu Ramadhan Haji Fakhi (aliyekuwa Waziri Kiongozi),
alikuwa akiongea kwa sauti nzito, kama ulikuwa ukimsikiliza, unasema
muungano haupo,” alisema Profesa Kabudi na kueleza kuwa Fakhi alisema:
“Zanzibar siyo koloni la Tanganyika.”
Alikuwa akichangia hotuba katika Kongamano la
Kujadili Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lililofanyika
mjini Zanzibar jana. Alieleza kwamba mjadala wa sasa wa muungano siyo
mkali kama uliokuwepo mwaka 1983 na 1984.
Hata hivyo, hotuba hiyo ya Profesa Kabudi
iliyokuwa ikirushwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC1) ilikatishwa kabla mzungumzaji kumaliza hotuba yake.
Katika maelezo yake, Profesa Kabudi ambaye pia ni
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kuwa Fakhi alikuwa
haongei kama mtu baki, bali aliagizwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Lugha ilikuwa ni kali,” alisema.
Akifungua kongamano hilo, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilal alisema kuwa
masuala mengi yanayoleta mgogoro kwenye Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar yanaibuliwa na wanasiasa.
“Unawezekana kuwa muungano unatunyima fursa moja
ua mbili, unatunyima uwezo wa kuamua katika masuala hayo, lakini
wananchi hawayaoni hayo. Muungano ni wa wananchi, viongozi wana fursa
zao, lakini wahakikishe wanawahudumia wananchi,” alisema.
Mjumbe huyo ametoa kauli hiyo siku chache baada ya
Rais Jakaya Kikwete na baadhi wanasiasa kutoka CCM, wakiwamo Wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba kuikosoa Rasimu ya Katiba Mpya.
Kikwete pamoja na wajumbe hao kwa nyakati tofauti,
walisema kuwa Rasimu iliyowasilishwa bungeni na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba haionyeshi uhalisia wa matakwa ya wananchi walio wengi kuhusu
muundo wa muungano.
EmoticonEmoticon