April 08, 2014

PINDA MGENI RASMI, HAFLA YA KUKABIDHI HUNDI ZA RUZUKU KWA WACHIMBAJI WADOGO










TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda atakuwa mgeni rasmi katika hafla iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini ya kukabidhi hundi za ruzuku ya Dola za Marekani 500,000 kwa wachimbaji wadogo 11 waliokidhi vigezo.

Hafla ya Utoaji wa hundi hizo kwa wachimbaji wadogo itafanyika mjini Dodoma tarehe 9/4/2014 katika Chuo cha Madini ambapo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiambatana na  Naibu Waziri anayeshughulikia Madini, Stephen Masele pamoja na watendaji kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA) watashuhudia utoaji wa hundi hizo.

Ruzuku hiyo ya Dola za Marekani 500,000 imetolewa na Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ulio chini ya Wizara ya Nishati na Madini.

Kutolewa kwa hundi hizo ni matokeo ya mkataba ambao Wizara ya Nishati na Madini iliingia na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ili Benki hiyo iwe Wakala wa kutoa mikopo na ruzuku kwa wachimbaji wadogo kwa niaba ya serikali.

Mkataba wa uendelezaji wachimbaji wadogo ulioingiwa kati ya TIB na Serikali unasisitiza ruzuku kutolewa kwa wachimbaji wadogo wenye sifa ili kuwawezesha kufanya shughuli zao za uzalishaji mali, wakiwepo wanawake wanaojishughulisha na utoaji huduma katika maeneo ya uchimbaji mdogo.

Wachimbaji wadogo 11 watakabidhiwa hundi hizo za ruzuku baada ya kukidhi vigezo vya kuwa na uzoefu wa uchimbaji mdogo usiupungua miaka Tano, kuwa na leseni hai ya uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini pamoja na kuwa na ushahidi wa upatikanaji wa mashapo au mali ghafi inayohitajika kwa ajili ya mradi unaoombewa ruzuku.
Imetolewa na;

BADRA MASOUD
MSEMAJI WA WIZARA

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »