WAKULIMA WA MKONGE WAISHAURI SERIKALI KUPITIA UPYA VIWANGO VYA KODI.

April 08, 2014
NA RAISA SAID,TANGA.
WAKULIMA wa zao la Mkonge mkoani Tanga wameishauri Serikali ipitie upya viwango vya kodi ya ardhi na kufanya uchambuzi yakinifu ikiwahusisha wadau katika sekta mbalimbali ili kufanya maamuzi kwa maslahi ya walio wengi na Taifa kwa ujumla.
 Akizungumza katika mahojiano na vyombo vya habari vya mkoa wa Tanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya mkonge ya Katani Limited, Salum Shamte alisema kuwa kodi ya ardhi ni suala mtambuka ambalo Serikali haitakiwi kulifumbia macho.

"liko ndani ya uwezo wa Serikali, kwamba mwekezaji anaweza kuruhusiwa kuwekeza kabla ya kulipa kodi hadi atakapoanza kuwa na mapato kama ilivyo kwenye sheria ya uwekezaji katika sekta nyingine," alishauri Shamte.
Sekta ya Kilimo ndiyo inayoajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania, kulisha Watanzania wote kwa asilimia 95 na kuchangia pato la taifa kwa 24.
"Ongezeko la kodi kwa asilimia 500 linakinzana na matarajio ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na hivyo kuhatarisha ongezeko la uzalishaji, tija na kipato katika sekta ya kilimo," alieleza Mkurugenzi huyo.

Alisema kuwa ongezeko la kodi ya ardhi linaonekana litaathiri
wawekezaji walio wengi katika sekta ya kilimo zikiwemo sekta ya mazao na mifugo.
Uwekezaji katika sekta ya kilimo mara nyingi huhitaji eneo kubwa
tofauti na uwekezaji wa aina nyingine, na hasa kwa wawekezaji wakubwa. Tozo la kodi ya Sh. 1000 kwa eka kwa mwaka inaonekana ni ndogo kwa wale wanaowekeza katika maeneo madogo kwa mfano eka 2 hadi 5.
Hata hivyo, kwa mwekezaji mwenye eneo kuanzia eka 5,000 na kuendelea, kiwango hiki ni kikubwa na wakati mwingine sio rahisi kulipika kwa wakati mmoja kama inavyodhaniwa.
Shamte alisisitiza kuwa kutokana na athari hizo Serikali ifanye
marekebisho ya haraka kabla ya kutekelezwa kwa kuzingatia vigezo na uhalisia katika masuala ya kiuchumi.
"Tunapendekeza kwamba mwekezaji apewe muda wa kutosha kwa ajili ya kuzalisha kabla ya kuanza kulipa kodi ya ardhi," alisema.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »