MCHEZAJI WA ZAMALEK AFARIKI DUNIA, RAIS CAF ASHIRIKI MSIBA

April 03, 2014

Na Salum Esry, Cairo
RAIS wa Shirikisho la Soka (CAF), Issa Hayatou ameelezea mshituko wake kufuatia kifo cha kiungo wa zamani wa Misri, Taha Basry.
Basry, gwiji wa Zamalek amefariki dunia jana Aprili 2, mwaka 2014 katika hospitali ya Cairo alikokuwa amelazwa kwa matibabu akiwa na umri wa miaka 68.
Pumzika kwa amani; Taha Basry enzi za uhai wake akiwa kocha

“Kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya CAF na mimi mwenyewe, natoa salamu zangu za rambirambi kwa Chama cha Soka Misri (EFA) na familia ya marehemu. Fikra zangu zipo nao katika wakati huu mgumu,” amesema Hayatou.
Basry alijiunga na Zamalek mwaka 1965 na alikuwemo kwenye kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Misri msimu wa 1977/1978 na Makombe mawili ya Misri mwaka 1975 na 1977.
Alicheza Fainali tatu za kombe la Mataifa ya Afrika katika miaka ya 1970, 1974 na 1976, wakati mwaka 1986 alikuwepo kwenye benchi la Ufundi la Mafarao. Pia aliwahi kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka Misri msimu wa 1977/1978. Akiwa kocha, alizifundisha timu za ENPPI, Arab Contractors, Ghazl El-Mahalla na Petrojet.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »