DC GAMBO AHIMIZA UJENZI WA MAABARA KWA SHULE ZA SEKONDARI ZA KATA KWA WANANCHI.

April 14, 2014
Na Mashaka Mhando,Korogwe
MKUU wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo amehimiza wananchi wilayani humo, kuwa mstari wa mbele katika kushiriki shughuli za ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari za kata unaoendelea wilayani humo ili kuwawezesha watoto waweze kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo na kupata elimu sahihi.

Akizungumza na wananchi wa kata ya Makuyuni wakati alipotembelea ujenzi wa smaabara ya shule ya sekondari Madago iliyopo katika kata hiyo, Gambo alisisitiza kwamba katika mpango huo wa ujenzi wa maabara wananchi wote wanawajibu wa kushiriki kikamilifu kwa kutoa michango ili kufanikisha ujenzi katika kipindi kilichopangwa.

Alisema mpango huo wa ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari ni agizo la Rais Jakaya Kikwete ambaye leo atakuwa wilayani hapa, hivyo wananchi wanatakiwa kulitekeleza ili kusaidia kuboresha maendeleo ya sekta ya elimu na kuwawezesha watoto wanasoma na kupenda masomo ya sayansi.

“Ndugu zangu wananchi napenda mwelewe kwamba hili ni agizo la Rais na hizi maabara sitosoma mimi wala kiongozi yeyote hapa ila watoto wetu ndiyo watakaonufaika nazo, hivyo ni vyema mkashiriki kikamilifu katika ujenzi huu,” alisema Gambo.

Hata hivyo, Gambo aliwapongeza wananchi wa kata hiyo pamoja na Mtendaji wa Kata Bonifasi Siruri kwa jitihada walizozifanya kuhakikisha maabara ya shule yao ya Madago imefikia katika hatua nzuri ya kuezekwa bati tofauti na maeneo mengine katika wilaya hiyo.

Awali Mtendaji huyo akimsomea taarifa hiyo Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa hadi kufikia hatua hiyo wananchi tayari wametumia kiasi cha sh. 60,670,000 ambapo wamejenga kwa nguvu zao na kufikia hatua ya kumalizia chumba kimoja kati ya vitatu vilivyopo kupiga bati.

Siruri ambaye ni kati ya watendaji wachache wilayani humo wanaojituma kusimamia na kumaliza miradi kwa wakati, alisema maabara hiyo hadi itakapomalizika itatumia kiasi cha sh. 133,070,960 ambapo hata hivyo, sasa aliiomba serikali iisaidie maabara hiyo.
MWISHO

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »