WANAFUNZI WA UDOM MWAKA WA MWISHO, WAAHIDI KUJIUNGA NA PPF
Meneja
Uhusiano na Masoko wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Lulu Mengele, akitoa
mada kuhusiana na huduma mbalimbali zitolewazo na Mfuko huo kwenye
semina iliyoandaliwa na Mfuko huo kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambapo zaidi ya wanafunzi 500 walihudhuria
semina hiyo Jumamosi Machi 29, 2014.
Baadhi
ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wakifuatilia mada kutoka
kwa Meneja Uhusiano na Masoko wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Lulu Mengele.
Meneja
wa Kanda ya Mashariki na Kati wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, John
Mwalisu, akitoa mada kwenye semina ya siku mbili, iliyoandaliwa na Mfuko
huo kwa wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM).
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wakifuatilia mada.
WANAFUNZI
wa mwaka wa mwisho wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wameridhishwa na
mada mbalimbali zilizotolewa na Mfuko wa Pensheni wa PPF, na wameahidi
kujiunga kwa wingi na Mfuko huo, kwani wengi wao wanatarajia kujiajiri,
hivyo itakuwa fursa nzuri kwao kuandaa maisha yao ya baadaye
watakapostafu.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti chuoni hapo jana mara baada ya semina iliyoandaliwa
na PPF kwa wahitimu wa elimu ya juu, walisema awali walidhani kwamba
Mfuko wa Pensheni wa PPF ni kwa ajili ya wafanyakazi walioajiriwa tu,
lakini sasa wamefahamu kuwa milango iko wazi hata kwa wale ambao
wamejiari ili mradi tu wawe na umri wa kuanzia 18.
Mmoja
wa wanafunzi hao, Oneck Mwalongo, alisema kwa muda wote ambao amekuwa
chuoni alikuwa hajawahi kuona maofisa wa mifuko inayojihusisha na
masuala ya hifadhi ya jamii wakifika kwa ajili ya kuwapa semina
kuhusiana na fursa zinazotolewa, lakini PPF imekuwa ya kwanza kuwapa
elimu hiyo.
“Lakini
leo hii tunashukuru PPF wametufumbua macho kwani tulikuwa tunajua ili
uwe mwanachama ni lazima uwe umeajiriwa, kwangu mimi nitajiunga na PPF
kwa sababu kozi yangu ya sayansi ya kompyuta si lazima niajiriwe
nitajiajiri mwenyewe,” alisema Mwalongo.
Alisema mfumo wa uwekaji amana wa hiari ulioanzishwa na PPF utasaidia vijana wengi watakaokuwa wamejiajiri kujiwekea akiba.
Pia
alisema amefurahishwa na mpango wa baadaye wa PPF wa kuanza kukopesha
wanachama wake viwanja, kwani nyumba ndiyo jambo muhimu kwa maisha ya
binadamu.
Mwalongo,
alisema wakati akiingia kwenye semina hiyo alikuwa hafahamu kama
maisha ya kesho huanza kuandaliwa leo, hivyo atakapoondoka chuoni hapo
ataanza kujiwekea akiba ili asikumbane na msemo wa fainali uzeeni.
“Nilikuwa sifahamu kama maisha ya kesho yanaandaliwa leo wamenionesha njia sasa naanza kuandaa maisha ya uzeeni,” alisema.
Kwa
upande wake, Elizaberth Elibarick, alisema PPF ni mfuko wa kujiunga nao
hasa kwa kuzingatia mfuko huo una mfumo wa uwekaji amana wa hiari na
unatoa fao la elimu kwa watoto wa mwanachama anapofariki akiwa bado
kazini.
Alisema
si jambo la mchezo Mfuko kumsomesha mtoto au watoto wa wanachama ambao
wamefariki kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita na kizuri zaidi
wanalipa mafao kwa wakati.
Naye
Leonard Mgeja, alisema kupitia semina hiyo yeye na wanafunzi wenzake
wameweza kufahamu vitu vya msingi ambavyo walikuwa hawafahamu kuhusiana
na Mfuko wa PPF.
“Leo
tumefahamu umuhimu wa maandalizi ya maisha ya baadaye tukiwa na umri
mdogo ili kufanya mambo sahihi kabla ya kufikia uzeeni,” alisema na
kuongeza kwamba;
“Hivi
sasa ambapo tunakaribia kwenda makazini tunaenda na mwanzo mzuri kwani
hatutegemei kuajiriwa tu, bali na kujiajiri hivyo tutajiunga na
uchangiaji wa hiari kama hatutakuwa kwenye mfumo rasmi wa ajira.”
Awali
Meneja Uhusiano na Masoko wa Mfuko huo, Lulu Mengele, aliwaasa
wanafunzi hao wa mwaka wa mwisho zaidi ya 500 waliohudhuria semina hiyo,
kujiunga na PPF kupitia Mfumo wa asili wa Pensheni au ule wa uwekezaji
amana pale ambapo wataamua kujiajiri wenyewe.
“Mfumo
wa uwekezaji amana, unaandikisha watu kutoka sekta isiyo rasmi, kama
wakulima, wafugaji, machinga na mama lishe”. Alifafanua.
Katika mada ya uwekezaji amana, Lulu alisisitiza umuhimu wa kuweka akiba kwani matayarisho ya maisha ya kesho yanaanza sasa.
Kwa
upande wake Meneja wa Mfuko wa Pesnheni wa PPF, Kanda ya Mashariki na
Kati, inayojumuisha Mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida, John Mwalisu,
alisema PPF imeandaa semina hiyo kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho wa
chuo hicho kwa kuwa wao ndiyo wanaingia kwenye soko la ajira.
Alisema
kutokana na wao kuwa na nguvu ya kuajiriwa au kujiajiri wameona ni vema
kuwaelimisha namna nzuri ya kutunza akiba ili iwasaidie watakapokuwa
fikia hatua ya kustaafu.
EmoticonEmoticon