March 31, 2014


JK aitaka halmashauri ya Jiji la Tanga kulipa fidia wananachi. .



NA OSCAR ASSENGA, TANGA.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dokta Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Halmashauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha inawalipa fidia wananchi waliojenga karibu na eneo la kituo cha mabasi na eneo la kuegeshea malori Kange kwa sababu walipima wenyewe viwanja wakati wakijua kutakuwa na ujenzi huo.

Agizo hilo alilitoa jana wakati alipotembelea stendi hiyo kuweka jiwe la msingi  na kupokea taarifa wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi wilayani Tanga ambayo aliianza Jumapili wiki hii ya kugadua miradi mbalimbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara.


Alisema haiwezekani stendi hiyo kujengwa bila kuwepo kwa eneo mbadala ambalo litaweza kuongezeka wakati matumizi yake yatakapongezeka kutokana na mahitaji ya wakazi wa jiji la Tanga hivyo wanapaswa kufikiria namna ya kufanya ili kuweza kupanua ikiwemo kuwalipa fidia wananchi waliojenga stendi hiyo pembeni yake.

    “Hakikisheni mnafikiria namna ya kuongeza eneo la stendi ili liweza kukidhi mahitaji yatakayotokana na mabasi kuongezeka hivyo halmashauri mnakazi kulipatia ufumbuzi suala hilo kabla ya kukumbana na hali hiyo “Alisema Rais Kikwete.


Aidha aliwataka wasifanye makosa kama waliyoyafanya kwa mara ya kwanza kujenga kwenye eneo hilo kuwa dogo ikiwemo kujenga hapo sasa hakikisheni mipango yenu mengine mnatafuta eneo la kupanua stendi.

    
    “Kama eneo hili mmepanga kuligawa kwa wananchi bila kuangalia athari ambazo zinaweza kutokea sasa tafuteni fedha za kuwalipa fidia watu hao ili kupata upanuzi wa eneo hilo la stendi “Alisema Rais Kikwete.

Hata hivyo Rais Kikwete alishauri kuwa eneo la stendi ya malori kuwa mbele ya kiwanda cha saruji jijini Tanga ili iweza kurahisisha usafiri wao wa kutokana na kuingia jijini Tanga ikiwemo kuondoa kero ya msongamano.

Awali akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi na eneo la kuegeshea malori lililopo eneo la kange jijini Tanga,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga,Juliana Malange alisema ujenzi huo ulianza Novemba mosi mwaka jana ambapo utekelezaji wake ulifanyika kwa kipindi cha miezi 16 na umefikia asilimia 90.

Malange alisema ujenzi wa kituo hicha cha mabasi kange chenye ukubwa wa mita za mraba 36,708 umegharimu bilioni 40.7 chini ya mkandarasi M/S Elerai Construction ya Arusha Tanzania kwa gharama hizo chini ya msimamizi mshauri UWP Consulting (T) kwa kushirikiana na halmashauri ya Jiji la Tanga.

Alisema mkandarasi huyo hivi sasa anaendelea kukamilisha kazi zilizobakia ikiwa ni pamoja na ufungaji wa taa,vibanda vya abiria,vyoo kwa ajili ya wasafiri na maeneo ya kuegeshea mabasi pamoja na uzio .

Aliongeza kuwa halmashauri kwa kushirikiana na msimamizi mshauri  na wakala wa barabara(Tanroad) imekamilisha usanifu wa barabara ya kuingia mabasi na malori ambapo hivi sasa mchakato wa kuanza ujenzi unaendelea.

Kituo cha mabasi kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuwahudumia mabasi 80-100, taxi 36,mabasi madogo ya wasafiri(Daladala 36) na magari madogo ya watu binafsi 40 kwa wakati mmoja.

Mradi huo  wa ujenzi unatekelezwa kwa ufadhili wa benki ya dunia kupitia mradi wa Tanzania Strategic Cities Project (TSCP) ikiwa ni miradi inayotekelezwa ni pamoja na ukarabati ya barabara kufikia kiwango cha lami km 15,ujenzi wa mifereji mkubwa wa maji ya mvua km 5.62,ujenzi wa kituo kipya cha mabasi chenye ukubwa wa mita za mraba 36,708,ujenzi wa eneo la kuegeshea  malori lenye ukubwa mita za mraba 29,952 na ununuzi wa vifaa kwa ajili ya usafi wa Jiji.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »