HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, WAKATI WA KULIHUTUBIA BUNGE MAALUM LA KATIBA, TAREHE 21 MACHI, 2014, DODOMA
Mheshimiwa Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Pongezi
Nakushukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa ya kuja
kuzungumza na Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge letu Maalum la Katiba katika
siku hii muhimu na ya kihistoria kwa nchi yetu. Nimekuja kuwatakia heri
na naungana na Watanzania wenzetu wote kuwaombea baraka za Mwenyezi
Mungu, ili muweze kuifanya kazi yenu kwa utulivu, hekima, umakini mkubwa
na kuimaliza kwa salama na kwa mafanikio yanayoyatarajiwa na
Watanzania.
Natoa
pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza
Bunge hili maalumu na la kihistoria. Ushindi mkubwa mliopata ni
kielelezo tosha cha imani kubwa na matumaini waliyonayo Wajumbe wenzenu
kwenu. Matumaini yao ndiyo matumaini ya Watanzania wote, kwamba
mtaliongoza vizuri Bunge hili, ili liweze kutimiza kwa ufanisi mkubwa
jukumu lake muhimu sana katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Niruhusu
pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa
bahati ya aina yake waliyopata ya kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Fursa hii hutokea mara chache sana katika
historia ya nchi yo yote na watu wake. Mkifanikiwa kuipatia nchi yetu
Katiba nzuri majina yenu yataandikwa kwa wino wa dhahabu, katika
kumbukumbu za historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni
matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga Katiba itakayokubalika na wengi.
Katiba inayotekelezeka. Katiba itakayoimarisha Muungano wetu kwa
kuondoa changamoto zilizopo sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu mfumo
bora wa kuongoza na kuendesha mambo yetu. Katiba itakayoimarisha umoja,
upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania,
licha ya tofauti zao za asili za upande wa Muungano na maeneo watokako,
au tofauti za jinsia, rangi, kabila, dini na ufuasi wa vyama vya siasa.
Katiba itakayodumisha amani, usalama na utulivu nchini. Katiba
itakayostawisha zaidi demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria,
utawala bora na kudhibiti maovu. Na, mwisho ingawaje siyo mwisho kwa
umuhimu, Katiba itakayoweka mazingira mazuri kwa uchumi wa nchi kukua,
na wananchi wengi kunufaika sawia na maendeleo yatayopatikana.
Historia ya Katiba Nchini
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Hii
itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Aprili 26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato wa kutunga Katiba
mpya. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya Muda na
mara ya pili ni mwaka 1977 ilipotungwa Katiba ya Kudumu tuliyonao sasa.
Tofauti na mara mbili zilizopita, safari hii mchakato unahusisha watu
wengi zaidi. Wananchi wameshiriki moja kwa moja kutoa maoni yao kwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na ndio watakaofanya uamuzi wa mwisho
kuhusu Katiba mpya kwa kura ya maoni. Wananchi pia walipata nafasi ya
kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyojadili Rasimu ya
Kwanza ya Katiba. Pia walipata nafasi ya kutoa maoni yao kupitia
Mabaraza ya Katiba ya taasisi. Katika Bunge hili wapo wananchi 201
kutoka makundi mbalimbali.
Katika
mchakato wa kutunga Katiba za mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo Tume za
Kuandaa Rasimu na Bunge Maalum la Katiba kama ilivyo katika mchakato
huu. Hata hivyo, kwa Katiba zilizopita Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano pekee ndio waliounda Bunge Maalum. Safari hii Bunge Maalum
linajumuisha Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi 201
wanaotoka kwenye jamii, wakiwakilisha asasi na makundi mbalimbali ya
Watanzania kutoka Zanzibar na Tanzania Bara. Mchakato wa sasa utaishia
kwenye kura ya maoni itakayoshirikisha wananchi wote wa Tanzania
wanaoruhusiwa kupiga kura. Michakato iliyopita iliishia Bunge Maalum
pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tangu
kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili, 1977, mpaka sasa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko takriban mara 14.
Mabadiliko hayo yalitokana na kufanyika au kutokea kwa mabadiliko muhimu
ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika nyakati mbalimbali hapa nchini
na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa ruksa yako naomba nitaje baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:-
1. Mabadiliko
ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa
Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya
Afrika Mashariki mwaka 1977.
2. Mabadiliko
ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya Zanzibar,
hivyo kulazimu Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya Jamhuri ya
Muungano.
3. Mabadiliko
ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa vipindi vya Urais ambao
haukuwepo kabla ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za Binadamu (Bill of
Rights) yaliingizwa kwa mara ya kwanza katika Katiba. Vilevile,
Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mambo mengine ya iliyokuwa Jumuiya ya
Afrika Mashariki yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
4. Mwaka
1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi vya
Siasa badala ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia
utaratibu wa uchaguzi wa Rais na Wabunge ulirekebishwa ili uendane na
mfumo wa vyama vingi vya siasa. Vilevile utaratibu wa kuwa na viti
maalum vya wanawake katika Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa
asilimia 15 ya Wabunge wote. Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia
ya nchi yetu Bunge lilipewa mamlaka ya kumwajibisha Rais na Waziri Mkuu
kupitia kura ya kutokuwa na imani.
5. Mabadiliko ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais kupitia Mgombea Mwenza.
6. Mwaka
2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika mabadiliko
yaliyopanua wigo wa Haki za Binadamu na kuongeza uwakilishi wa
wanawake.
Umuhimu wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kufanyika
kwa mabadiliko hayo kunathibitisha utayari wa Serikali kufanya
mabadiliko kila ilipoonekana inafaa kufanya hivyo. Pamoja na kufanya
yote hayo na Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo na madai
yaliyokuwa yanajirudia ya kutaka Katiba ya Tanzania iandikwe upya. Wako
watu walioimithilisha Katiba yetu na nguo yenye viraka vingi mno kiasi
kwamba ingefaa kununua mpya badala ya kuendelea kuivaa.
Madai
ya kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti baada ya kuanza kwa mfumo wa
vyama vingi vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai Katiba mpya kwa imani,
eti kwamba, itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo tu, hata katika
mchakato wa Serikali zetu mbili kushughulikia kero za Muungano,
imedhihirika kuwa baadhi ya changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya
Katiba ili kuzipatia ufumbuzi wa uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
kutambua ukweli huo na baada ya kushauriana na kukubaliana na viongozi
wenzangu wakuu wa Chama tawala na Serikali zetu mbili wakati ule, ndipo
tarehe 31 Desemba, 2010, nikatangaza dhamira ya kuanzisha mchakato wa
kutunga Katiba mpya. Nilieleza siku ile kuwa katika mchakato huo
tutakuwa na ushirikishwaji mpana wa wananchi wa Tanzania kwa makundi yao
ya jinsia, dini, siasa na shughuli wazifanyazo kujipatia riziki na kwa
maeneo wanayotoka katika pande zetu mbili za Muungano.
Mchakato wa Katiba Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tarehe
16 Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa kwa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya kuliongoza taifa katika mchakato wa kutunga
Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 18 Novemba,
2011 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Muswada wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, mchakato wa
kutunga Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya
Katiba. Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza maoni ya wananchi mmoja
mmoja na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao na kupitia Mabaraza ya
Katiba. Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya Katiba mpya
itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kujadiliwa na Katiba mpya
kutungwa. Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa wananchi kupiga kura ya
maoni ya kuamua kama wanaikubali au kuikataa Katiba mpya.
Tarehe
6 Aprili, 2012 nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na kuwaapisha tarehe 13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi tarehe 2
Mei, 2012 na kuikamilisha kwa mafanikio, hatua zote zilizoihusu na
kukabidhi kwangu na kwa Rais wa Zanzibar, Taarifa ya Tume na Rasimu ya
Katiba tarehe 30 Desemba, 2013. Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume,
Mheshimiwa Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo mbele ya Bunge hili
tukufu tarehe 18 Machi, 2014, kinahitimisha rasmi kazi ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. Kazi inayofuatia ni ya Bunge hili kujadili,
kuamua na kutunga Katiba mpya. Baada ya hapo Katiba mpya itafikishwa
kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga kura ya NDIYO au
HAPANA.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Rasimu
ya Katiba ilichapishwa kwenye gazeti la Serikali na magazeti mengine
yanayosomwa na wananchi kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha 20(2) cha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa ya Tume na
Rasimu ya Katiba viliwekwa wazi kwenye tovuti ya Tume kwa kila mtu
kusoma. Inafurahisha kuona kuwa watu wengi wameisoma Taarifa ya Tume na
Rasimu ya Katiba na kumekuwa na mjadala mpana kuhusu nyaraka zote hizo
muhimu. Watu wengi wametoa maoni yao na wanaendelea kufanya hivyo. Kwa
maoni yangu hili ni jambo jema sana na ni kielelezo thabiti kuwa
demokrasia imestawi na inazidi kuota mizizi Tanzania. Pia, kwamba,
Watanzania wako huru kushiriki na kutoa maoni yao kwa mambo
yanayowahusu.
Pongezi kwa Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
mara nyingine tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa Wajumbe wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jaji Joseph
Warioba akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani, kwa kazi
kubwa na nzuri waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi hasa ukizingatia
ukubwa wa nchi yetu, wingi wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la
kumpoteza Mjumbe mwenzao muhimu Dkt. Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele
ya haki katikati ya mchakato.
Pamoja
na hayo, kwa bidii kubwa Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote
nchini na kuwafikia watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa mdomo na kwa
maandishi. Halikadhalika, walipokea na kuchambua maoni 772,211 kutoka
kwa wananchi na taasisi mbalimbali. Baada ya kupokea maoni ya wananchi,
kufanya utafiti na kwa kutumia maarifa na uzoefu wao, Wajumbe wakafanya
kazi ngumu, kuliko yote, ya kutengeneza Rasimu ya Katiba iliyoko mbele
ya Bunge hili. Ni kweli kwamba Wajumbe hawakuweza kuwafikia wananchi
wote wa Tanzania, lakini wameweza kuwafikia wananchi wengi, ambao kwa
kiasi kikubwa wanawakilisha taswira na mitazamo mipana ya jamii yetu.
Baadhi ya Masuala Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume
imefanya kazi nzuri, yenye thamani kubwa na ya manufaa kwa taifa la
Tanzania. Rasimu imeandikwa vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume
imetoa mapendekezo ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha
Katiba ya nchi yetu, kwa namna ya pekee. Katiba inayopendekezwa,
imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati
tulionao na kuweka msingi mzuri kwa huko mbele tuendako. Kwa taratibu
za kawaida za marekebisho ya Katiba tuliyonayo, isingekuwa rahisi
kuingiza mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi. Kina
kurasa 106, sura 17 na ibara 271. Wajumbe wa Bunge hili mnatakiwa
kusoma na kuelewa vizuri kila kilichoandikwa ili muweze kufanya uamuzi
ulio sahihi. Mnawajibika kuchambua kwa kina na umakini mkubwa kila
kilichomo, sura kwa sura, ibara kwa ibara, sentensi kwa sentensi na hata
neno kwa neno. Hamna budi kujiridhisha kuhusu uandishi wa vifungu vya
Rasimu ya Katiba na kufaa kwa dhana mbalimbali zilizoingizwa na
kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kile
ambacho Wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au
kufutwa msisite kufanya hivyo ili Watanzania wapate Katiba iliyo bora.
Msipofanya hivyo kuna hatari ya kupata Katiba ambayo ni ngumu
kuitekeleza. Aidha, tunaweza kuwa na Katiba ambayo itanung’unikiwa na
watu wengi na kusababisha madai ya kutaka ifanyiwe marekebisho muda
mfupi baada ya kupitishwa. Bunge hili linao wajibu maalum wa kuzuia
balaa hilo lisitokee katika nchi yetu. Ngazi mbalimbali zilizowekwa
katika mchakato huu ni kama chujio la kuepusha hali hiyo isitokee. Kile
ambacho hakikuonekana katika hatua moja kitaonekana katika hatua
inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo muitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza kuwa moja ya jambo mnalotegemewa kufanya ninyi wenzetu
mliopewa dhamana ya kutunga Katiba ya nchi yetu ni kujiridhisha na
uandishi wake. Yapo maoni yaliyotolewa kuhusu uandishi ambayo naomba
myatafakari na kuamua ipasavyo. Kwa mfano, kuna baadhi ya vifungu vya
Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi mno kuliko inavyostahili
Katiba kuwa (too prescriptive). Pia kuna mawazo kwamba baadhi ya
mambo hayangetakiwa kuwa katika Katiba bali yawe kwenye Sheria
zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu hatakwenda mahakamani kuidai Serikali impatie (non justiciable).
Mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ni mazuri na yanavutia, lakini lazima
yaendane na uwezo wa nchi na uchumi wake kuhimili. Simaanishi kwamba
tuyatoe kwenye Katiba, bali yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi
utakaporuhusu yatekelezwe. Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali
kujikuta inalaumiwa au hata kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai
ya jambo moja au jingine ambayo haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo
kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na Katiba ambayo ni ngumu
kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Yapo
pia maoni kuwa baadhi ya vifungu vina upungufu katika uandishi wake,
hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza
kuwepo athari na nyingine zinaweza kuwa mbaya. Kwa mfano, Ibara ya 2 ya
Rasimu inayotambulisha eneo na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo
inasomeka kuwa “Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote
la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la
Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari”.
Maelezo
hayo yameacha kutambua, kwa upande wa Tanzania Bara, sehemu yetu ya
maziwa na mito ambayo ni kubwa sana. Kwa nini tuache kuitaja? Je
hatutoi nafasi kwa nchi tunazopakana nazo siku moja wakaja kupora sehemu
zetu hizo na sisi kukosa utetezi kwa kuwa hata Katiba yetu
haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni yetu? Hili ni jambo kubwa ambalo
Bunge hili lazima mlirekebishe. Wakati ndiyo huu hakuna mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo
jingine kuhusu uandishi ni mgongano kati ya pendekezo la msingi la Tume
la kuwa na muundo wa Serikali tatu na majukumu ya Serikali ya Muungano
ambayo kimsingi ni majukumu ya Serikali za nchi washirika. Katika
Rasimu hii malengo ya taifa yameainishwa na Serikali ya Muungano
inatakiwa kuhakikisha kuwa malengo hayo yanatekelezwa na itoe taarifa
Bungeni. Katika mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa na Tume masuala
yahusuyo uchumi na maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo, ufugaji,
uvuvi, viwanda, biashara, pembejeo, elimu, hifadhi ya jamii na kadhalika
yako chini ya mamlaka ya Serikali za nchi washirika. Mamlaka ya
Serikali ya Muungano ni kwa mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na Mamlaka
ya Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia
na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya
Siasa, Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya
Muungano.
Kwa
Rasimu kupendekeza muundo wa Serikali tatu na kuipa Serikali ya
Muungano majukumu ambayo haina mamlaka nayo, ni kuzusha utata na
migongano kati ya Serikali ya Muungano na nchi washirika. Mkichagua
mfumo wa Serikali tatu, inawalazimu muyaondoe mambo hayo kwani Serikali
ya Muungano haistahili kuyatekeleza na wala haina uwezo wa kuweka
masharti kwa Serikali za nchi washirika kwa mambo yaliyo kwenye mamlaka
ya nchi hizo. Lakini kama mtaamua tuendelee na muundo wa Serikali
mbili, mambo haya mazuri yanatekelezeka na Serikali ya Muungano bila ya
matatizo. Katika uandishi wa Rasimu Utumishi katika Serikali ya
Muungano haumo katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Ni lazima liwemo.
Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo uandishi katika Rasimu. Naamini
mkiisoma Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua mengineyo.
Dhana Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
Rasimu kuna dhana mpya na mambo mapya kadhaa yaliyoingizwa ambayo
yanabadili utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa nchi na mambo mbalimbali.
Nawaomba mfanye uchambuzi wa kina kwa kila kinachopendekezwa na
kujiridhisha kuhusu kufaa kwake na manufaa yake. Fanyeni hivyo ili
tujihakikishie kuwepo kwa mambo mazuri na uendeshaji mzuri wa shughuli
katika taifa letu changa.
Mambo
ni mengi na kwa ufinyu wa muda sitaweza kuyazungumzia yote. Niruhusuni
nizungumzie baadhi ya dhana na mambo mapya yaliyomo katika Rasimu.
Jambo la kwanza, kwa mfano, linahusu Ibara ya 128 (2)(d) inayoleta dhana
ya “Mbunge kupoteza Ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi za Mbunge kwa
miezi sita mfululizo kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza”.
Watu hawana tatizo na Mbunge kuwa kizuizini ndani ya gereza kama
amepatikana na hatia Mahakamani na kuhukumiwa kifungo. Lakini,
isijekuwa yuko rumande kwa tuhuma akisubiri kesi kusikilizwa. Je akija
kuonekana hana hatia na kuachiliwa? Naungana na wale wanaoshauri kuwa
jambo hili lifafanuliwe vizuri na kutambua Mbunge kutiwa hatiani na
kupata adhabu ya kifungo cha kipindi hicho. Ni bora ifanyike hivyo
sasa ili kuondoa mikanganyiko. Hakuna haja ya kusubiri mpaka jambo hili
lije kufafanuliwa baadaye kwa Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
upande wa mtu kupoteza Ubunge kwa sababu ya “kuugua kwa miezi sita
mfululizo” ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili ambao haustahili
kufanywa na Katiba. Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine Mbunge
anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake. Anaweza
kuugua kwa miezi sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi chake cha
Ubunge kufika mwisho. Kwa nini awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba ya
mwaka 1977 tunayotumia sasa haina sharti hilo. Watu wanauliza hoja na
haja ya kuwa na sharti hili kwenye Katiba mpya ni ipi? Wanasema kwa
kweli anachostahili Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake iimarike
ili aendelee kutumikia watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake.
Tusiwatie watu kishawishi cha kukatiza matibabu ili kukwepa sharti
hilo. Ni vyema jambo hili mkalitazama kwa makini, na muone kama
linastahili kuwepo au hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
Rasimu hii imeingizwa dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa
Wabunge. Tena mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu mfululizo au
la!. Jambo hilo limezua mjadala motomoto katika jamii. Ni vizuri
mkajiridhisha juu ya sababu za msingi na manufaa ya kufanya hivyo hapa
Tanzania. Mazoea yetu na ya kwingineko duniani ni kuweka ukomo kwa
Wakuu wa Nchi kwa sababu nzuri na rahisi kuzielezea. Lakini, kuwawekea
ukomo Wabunge ni jambo jipya na huenda Tanzania tukawa wa kwanza.
Nashawishika kuungana na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema mno
kuanzisha utaratibu huo hapa kwetu. Nachelea kuwa tutainyima nchi yetu
fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu mzuri wa uongozi kwa
nafasi ya Ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa bila ya sababu za
msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo
lingine jipya linalopendekezwa na Tume ni utaratibu wa kumuondoa Mbunge
katikati ya kipindi chake cha uongozi. Kwa hoja linaonekana kuwa jambo
jema lakini naomba athari zake mzitafakari vizuri. Kuna hatari ya
kuanzisha misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha Wabunge wasifanye kazi
zao kwa utulivu bali wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao
kuwatengenezea fitna za kuwatoa. Utaratibu unaopendekezwa wa Chama
chake kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi katika mazingira hayo nao
unaweza kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha vuguvugu la kumuondoa Mbunge.
Walioshindwa kwenye kura ya maoni wanaweza kufanya kazi ya kuwachimba
wenzao mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima faida na hasa thamani
inayoongezwa na kuanzisha utaratibu huo. Naomba tujiridhishe kama jambo
hili jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi kila miaka mitano kurudi kwa
wananchi hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo wa Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo
lingine kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo limevuta hisia za karibu
watu wote nchini linahusu muundo wa Muungano wetu kuwa wa Serikali tatu
badala ya mbili za sasa. Pendekezo hili limezua mjadala mkubwa tangu
lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza na kurudiwa katika Rasimu ya pili.
Wakati mwingine mjadala umekuwa mkali na wa hisia kali kwa kila
upande.
Kwa
kweli hili ndilo jambo kubwa kuliko yote katika Rasimu kwa sababu
linapendekeza kuanzishwa kwa muundo na mfumo mpya wa kuendesha nchi
yetu. Hii ndiyo agenda mama ya Bunge hili ambayo kila Mtanzania
anasubiri kwa hamu uamuzi wenu utakuwa upi. Ombi langu kwenu ni kuwa
watulivu mnapojadili suala hili. Epukeni jazba ili mfanye uamuzi ulio
sahihi. Lazima mtambue uamuzi usiokuwa sahihi kwa jambo hili una hasara
kubwa. Tunaweza kupoteza kitu tulichokijenga kwa gharama kubwa kwa
nusu karne iliyopita. Tanzania inaweza kuwa nchi iliyojaa migogoro na
matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe;
Kama
alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba,
mara kadhaa, mjadala au madai ya kutaka muundo wa Serikali tatu si jambo
jipya. Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo ya kuunganisha nchi zetu
mbili mwaka 1964. Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya hewa ya
kisiasa Zanzibar mwaka 1984. Muundo huu uliwahi kupendekezwa na Tume
ya Nyalali mwaka 1992, ndiyo hoja ya G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia
na Tume ya Jaji Kisanga ya mwaka 1998. Lakini mara zote hizo
mapendekezo hayo hayakukubaliwa.
Waasisi
wa taifa letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri
ya Tanganyika wakati ule na Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais
wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wakati ule, waliamua kuchagua Muungano
wa Serikali mbili tulionao sasa. Walitoa sababu mbili kuu: “ni
muundo unaoihakikishia Zanzibar kuwa haimezwi na Tanganyika; na pia
unaiepusha Tanganyika kubeba mzigo mkubwa wa kugharamia Serikali ya
Tanganyika na ile ya Muungano”.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Natambua
kuwepo kwa rai ya kutaka Mwalimu Nyerere asitumiwe katika mjadala huu.
Nionavyo mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na
Sheikh Karume katika jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo kujadili na
kukubaliana kuwa mfumo wa Serikali mbili ndiyo bora kwa nchi yetu.
Iweje leo tunapozungumzia kuubadili, mawazo yao yawe hayafai kutumika
au hata kuzungumzwa. Hivi hasa mawazo ya nani pekee ndiyo bora zaidi
kutumika? Tutakuwa hatuutendei haki mjadala huu na sisi wenyewe
tunaoshiriki katika mchakato huu. Rai yangu kwenu ni kuwa mzitazame
hoja zote kwa marefu na mapana yake ili mpime kama zipo sababu za
kuubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa
Serikali tatu. Na, kama zipo mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye
uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye mashiko. (you must make an informed decision).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume
imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu.
Sababu ya kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote
Zanzibar na Tanzania Bara. Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania
waliotoa maoni, yaani asilimia 60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga mkono
muundo wa Serikali ya Mkataba, na asilimia 61.3 wa kutoka Tanzania Bara
wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu. Sababu ya pili ni kwamba muundo
huo unatoa majawabu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa
sasa wa Serikali mbili zinazonung’unikiwa na watu wa pande zetu mbili za
Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sababu
hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii.
Wapo wanaokubaliana na Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo
wanaosema Tume imesema kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono
muundo wa Serikali tatu, hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki.
Ndiyo matakwa ya wengi hivyo msemo wa Kiswahili usemao wengi wape
uheshimiwe.
Lakini
wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo. Wanasema
kuwa taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa
Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi
47,820 au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano
hivyo wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo
wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa.
Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni
wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanasema
pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na
67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu
Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo
waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali
mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7
walipendekeza Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka
Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Takwimu
za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni
772,211. Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa
Muungano na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine.
Hivyo basi wanahoji pia kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo
linalowakera Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu
waliotoa maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo
hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya
watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia
10.4 ya maoni yote. Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya
Watanzania wengi kutaka Serikali tatu uko wapi?”
Changamoto za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Kama
nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa kuhusu
kufaa kwa muundo wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu unajibu changamoto
nyingi za muundo wa Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri changamoto
za muundo wa Serikali mbili. Kwa upande wa Zanzibar wanalalamikia kile
kinachoitwa Tanzania Bara kuvaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na hivyo kutumia mamlaka ya Serikali ya Muungano kujinufaisha yenyewe.
Fursa hiyo Zanzibar hainayo. Aidha, wanasema mipaka na mamlaka ya
Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na kwa mambo ya Tanzania
Bara haijaainishwa vizuri ikaeleweka. Wazanzibari pia, wanazungumzia
mkanganyiko kuhusu ugawanaji wa mapato, na jinsi ya kuchangia shughuli
za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia Rais wa Zanzibar kuondolewa kuwa
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Aidha, kuna malalamiko kuwa
orodha ya mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka mambo 11 mwaka 1964
mpaka 22 mwaka 1992 imepunguza uhuru wa Zanzibar kwa mambo yake ya
ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
upande wa Tanzania Bara, Tume inaeleza kuwepo kwa manung’uniko kuwa
Muungano wa Serikali mbili umepoteza utambulisho wa kihistoria wa
Tanganyika na fursa ya watu wa upande wa Tanzania Bara kutetea maslahi
yao ndani ya Muungano. Wanasema Zanzibar sasa imekuwa nchi huru; ina
bendera yake, wimbo wake wa taifa na Serikali yake. Aidha, wanasema
Zanzibar imebadili Katiba na kujitambulisha kama nchi na kuchukua
madaraka ya Bunge la Muungano, kwa vile Sheria zinazotungwa na Bunge
lazima zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi kupata kibali cha kutumika
Zanzibar. Wananchi wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na haki
ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki
hiyo Tanzania Bara. Na wao vilevile wananung’unikia mkanganyiko kuhusu
ugawaji wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa
shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Zanzibar. Hizi ndizo baadhi ya changamoto ambazo Tume inaona jawabu
lake ili kuzitanzua ni kubadili muundo wa Muungano kuwa wa Serikali tatu
badala ya mbili za sasa.
Faida za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imefafanua kwamba mfumo wa Serikali tatu
utagawanya vizuri madaraka kati ya mamlaka tatu za Muungano. Unawezesha
Washirika wa Muungano kubaki na utambulisho wao wa kihistoria na
kiutamaduni na hivyo, utawezesha kuondoa hisia za Zanzibar kumezwa na
Muungano. Pia unawezesha kila upande wa Tanzania kuendesha mambo yake
yasiyo ya Muungano kadri wanavyoona inafaa. Vile vile unaweza ukaleta
ushindani wa kimaendeleo baina ya washirika na hivyo kusaidia kukuza
maendeleo ya nchi.
Faida za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja
na kuainisha changamoto za muundo wa Serikali mbili na kupendekeza kuwa
muundo wa Serikali tatu ndio utakaosaidia kuzitatua, Tume haikuacha
kutambua manufaa na mchango muhimu uliotolewa na muundo wa Serikali
mbili kwa nchi yetu. Tume inasema kuwa muundo wa Serikali mbili
unapunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za umma. Umesaidia kujenga
uhusiano na ushirikiano mzuri katika nyanja mbalimbali baina ya wananchi
wa pande zetu mbili za Muungano. Umezuia mkubwa kummeza mdogo; na
umedumisha Muungano mpaka kuufikisha hapa ulipo tangu kuasisiwa kwake
takriban miaka 50 iliyopita (1964). Aidha, umesaidia kudumisha amani,
umoja na utulivu hapa nchini.
Changamoto za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja
na kuelezea ubora wa muundo wa Serikali tatu kama jawabu kwa changamoto
za Serikali mbili, Tume inakiri kuwa hata muundo huu nao una changamoto
zake. Kwanza kabisa, Taarifa ya Tume inaeleza kuwa kutakuwa na gharama
kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma. Mheshimiwa Jaji Joseph
Warioba alitutoa hofu kuhusu gharama ingawaje mwaka 1993, Mwalimu
alikuwa na mawazo tofauti. Alisema kwamba: “watu …wanaodhani
kuwa gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa ndogo,
(Waulizeni Wazanzibari) na wala gharama ya Serikali ya Shirikisho
isingekuwa ndogo hata bila gharama ya mambo yasiyo ya Shirikisho”. Ni matumaini yangu kwamba katika mjadala wenu mtajipa nafasi ya kulitafakari suala hili kubwa na nyeti.
Tume
imesema pia kwamba, Muundo huu, unaweza kuibua tatizo la uchangiaji wa
gharama za uendeshaji wa shughuli za umma baina ya nchi washirika.
Vilevile, kuna uwezekano wa kuwepo sera zinazokinzana au kutofautiana
juu ya masuala ya msingi ya nchi na kuzua mgogoro kati ya washirika wa
Muungano na baina ya nchi washirika na Serikali ya Muungano. Aidha, upo
uwezekano mkubwa kwa muundo huu kuleta tofauti za kimaendeleo baina ya
pande mbili za Muungano kutokana na kila upande kuwa na sera na mipango
tofauti.
Tume pia imeelezea hatari ya muundo wa Serikali tatu kukuza hisia za utaifa (nationalistic feelings) kwa nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha Muungano. Muundo huu pia unaweza kuleta misuguano (paralysis and deadklocs in decision making)
katika kufanya uamuzi juu ya masuala muhimu ya kitaifa. Changamoto
hizo si tu zinaweza kuwa tishio kwa ustawi wa Muungano bali pia hata
uhai wake. Kwa ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali tatu kuna maana
ya kufanya kazi ya ziada ya kuzikabili changamoto hizi ili zisiue
Muungano wenyewe. Changamoto ambazo si ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanaounga
mkono muundo wa Serikali mbili wanasema kuwa kwa mlolongo huu wa
changamoto zilizoainishwa na Tume yenyewe, unadhihirisha kuwa muundo wa
Serikali tatu hautapunguza matatizo ya Muungano wetu bali utayaongeza
maradufu kuliko ilivyo sasa. Wanakiri kuwepo kwa changamoto katika
muundo wa sasa wa Muungano. Hata hivyo, wanaamini zinaweza
kushugulikiwa na kupatiwa ufumbuzi bila ya kuhitaji kuwa na Serikali ya
tatu. Wanatoa mifano kadhaa ya jinsi Serikali zetu zilivyoshughulikia
changamoto za Muungano katika kipindi cha uhai wake na mafanikio
yaliyopatikana.
Katika
kushughulikia kero za Muungano, Serikali zetu mbili ziliunda Tume ya
Shelukindo mwaka 1992 na Kamati ya Pamoja ya Serikali zetu mbili mwaka
1993. Mambo mengi yaliyoainishwa katika Tume ya Shelukindo na Kamati ya
Pamoja yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kwa upande wa kero
zilizoelezwa kwenye Tume ya Shelukindo, ilipofikia mwaka 2006 yalikuwa
yamebakia mambo 13 kati ya 31. Kwa jumla, kwa kero zilizoibuliwa na
Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja, hivi sasa yamesalia mambo sita
tu. Kimsingi ni mambo yahusuyo maslahi ya kiuchumi na yote yapo katika
hatua nzuri za kuyamaliza. Mambo hayo ni:
1. Mgawanyo wa mapato:
(a) Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki
(b) Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
2. Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
3. Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
4. Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.
5. Usajili wa vyombo vya moto.
6. Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali
zetu mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato huu wa
mabadiliko ya Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mambo hayo ni matatu
yafuatayo:
1. Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
2. Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
3. Tume ya Pamoja ya Fedha.
Matatu
mengine yatamalizwa kwa kutumia taratibu za kiutawala. Hali kadhalika,
katika kipindi cha mpito kinachopendekezwa na Tume yaani 2015 – 2018 ni
nafasi nzuri ya kushughulikia masuala yenye migongano kati ya Katiba ya
Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano. Mimi naishi kwa matumaini na
kwa vile tunayo dhamira njema ya kuimarisha Muungano wetu, naamini
tutaweza kuziondoa tofauti zilizopo.
Orodha ya Mambo ya Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kuhusu
orodha ya mambo ya Muungano kuwa 22 badala ya 11 ya awali, napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar hazina kigugumizi wala upungufu wa dhamira ya kisiasa ya
kuyapunguza yale yanayopunguzika. Napenda kwanza kabisa, ieleweke kuwa
kilichoongeza orodha hiyo si hila za Serikali ya Muungano kutaka
kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa mambo yake ya ndani. Na, wala siyo
udhaifu wa viongozi wa Zanzibar katika kutetea maslahi ya nchi yao. La
hasha.
Pili,
naomba ieleweke kuwa, kila kilichoongezwa katika Orodha ya Mambo ya
Muungano kilikuwa na sababu inayoeleweka, inayoelezeka na iliyokubalika
na pande zote mbili za Muungano. Hakuna hata jambo moja lililoingizwa
kwenye Katiba kwa kificho. Taratibu stahiki za kikatiba na kisheria
zilifuatwa. Hoja ziliwasilishwa Bungeni na kujadiliwa kwa uwazi na
uamuzi ulifanywa na Bunge kwa kuzingatia kanuni ya theluthi mbili ya
kura za kila upande wa Muungano. Kumbukumbu zipo katika Hansard za
Bunge la Muungano, ambazo ziko wazi kwa kila mtu anayetaka kuzisoma
asome. Nashauri mkazisome ili mpate kujua ukweli na undani wa kila
kilichoongezwa na sababu za kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nchi zetu mbili zilipoungana mwaka 1964 na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kulikuwa na mambo 11 kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Mambo hayo ni haya yafuatayo:
- Katiba ya Jamhuri ya Muungano,
- Mambo ya Nje,
- Ulinzi,
- Polisi,
- Hali ya Hatari,
- Uraia,
- Uhamiaji,
- Biashara ya nje na mikopo,
- Utumishi katika Serikali ya Muungano,
- Kodi ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
- Bandari, Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kati
ya mwaka 1965 na 1992 mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka 11 hadi
kufikia 22, kimsingi kutokana na mambo mbalimbali yaliyotokea nchini na
kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Pande zetu mbili za Muungano
zilikubaliana kuwa mambo hayo yaongezwe katika Katiba na taratibu za
kisheria na Kikatiba zilifuatwa. Kwa idhini yako naomba nitoe maelezo
kwa ufupi kwa yale yaliyoongezwa na kitu kilichosababisha mabadiliko
hayo kufanywa.
- Jambo la kwanza kuongezwa, yaani la 12 lilikuwa ni “sarafu, mabenki na fedha za kigeni”. Hii ilifanyika tarehe 10 Juni, 1965 kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board) mwaka 1964. Kwa ajili hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na sarafu yake na mipango yake ya kusimamia mambo yake ya kibenki na fedha. Serikali zetu mbili zilikubaliana masuala hayo yashughulikiwe na Serikali ya Muungano na Muswada husika wa Bunge uliidhinishwa kuwa Sheria na Mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa akikaimu Urais tarehe 10 Juni, 1965.
- Tarehe 11 Agosti, 1967 yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano:-
(a) Leseni za Viwanda na Takwimu, (Jambo la 13)
(b) Elimu ya Juu, (Jambo la 14)
(c) Jambo
la 15 lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya 10 ya
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nyongeza hiyo ilikuwa na mambo
27 ambayo Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la uratibu. Mambo hayo ni
pamoja na Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, Utabiri wa Hali ya
Hewa, Utafiti, Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli, Barabara,
Usafiri wa Majini na kadhalika.
- Tarehe 22 Julai, 1968 “rasilimali ya mafuta, petroli na gesi asilia” iliongezwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa jambo la 16. Kimsingi Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na gesi asilia kwa ajili ya nchi nzima. Baada ya kupanga upya Orodha ya Mambo ya Muungano, suala la rasilimali ya mafuta likawa la 15.
- Tarehe 22 Novemba, 1973 Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na kuwa jambo la 16. Hii ilifuatia kuvunjika kwa Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki mwaka 1971 na hivyo nchi yetu kulazimika kuunda Baraza la Mitihani la Taifa mwaka 1973.
- Mwaka 1984 yalipofanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya mwaka 1977, Orodha ya Mambo ya Muungano ilipangwa upya. Mambo yaliyokuwemo kwenye Nyongeza ya 10 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo la 15 katika Orodha ya Mambo ya Muungano yalipunguzwa na kubaki matano. Mambo hayo yalipewa namba kama ifatavyo:- Usafirishaji wa Anga kuwa Jambo la 17, Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa la 19 na Takwimu kuwa la 20 na Mahakama ya Rufani ya Tanzania ikawa jambo la 21.
- Tarehe 17 Mei, 1992 likaongezwa jambo la “Uandikishaji wa Vyama vya Siasa” na kuwa jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa na hasa uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Bila ya shaka maelezo haya yatasaidia kuelezea nini kimeongezwa na
mazingira ya kuongezwa kwake ni yepi. Kulikuwepo na sababu za msingi na
wala siyo hila ya namna yo yote ile iliyofanywa na mtu ye yote mwenye
nia mbaya na Zanzibar. Kama tulivyoona mambo mengi yalihusu
kilichokuwa kinatokea ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kila
yalipotokea mabadiliko katika uendeshaji wa shughuli za Jumuiya ya
Afrika Mashariki, huduma zilizokuwa zikitolewa na Jumuiya zilikabidhiwa
Serikali ya Muungano kubeba kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kiuchumi.
Yale yaliyokuwa yanagusa sehemu zetu mbili za Muungano yaliingizwa
katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Mengineyo yaliachiwa kila upande
kushughulikia ilivyoona inafaa. Kwa maana hii basi, mambo ambayo
yalitokana na uamuzi wetu wenyewe ni mawili tu. Mambo hayo ni
rasimali ya mafuta na gesi asilia (1968), na uandikishaji wa vyama vya
siasa (1992).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni
msimamo wa Serikali zetu mbili, tangu mwanzo mpaka leo kwamba, iwapo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajenga uwezo wake wa kufanya
baadhi ya mambo katika Orodha ya Mambo ya Muungano ipewe uhuru wa
kufanya hivyo. Lililo muhimu ni kuwa zisiondolewe tunu zenyewe za
Muungano wetu. Ndiyo maana, mambo kama vile bandari, takwimu, kodi ya
mapato, leseni za biashara, utafiti na mengineyo, yanasimamiwa na
kuendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuwemo kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano. Imekuwa hivyo kwa miaka kadhaa sasa na
imethibitika kuwa Zanzibar inayamudu. Ni makusudio yetu kutumia fursa
ya mchakato huu sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na mengineyo
tutakayokubaliana kutoka kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
ajili hiyo tumekubaliana kuliondoa suala la rasilimali ya mafuta na
gesi asilia lisiwe jambo la Muungano. Jambo hili tulishakubaliana tangu
wakati wa Rais Amani Abeid Karume tuliondoe na hata alipokuja Rais
Shein msimamo haukubadilika. Kilichotuchelewesha kutekeleza ni kuibuka
kwa fikra za kuwa na mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona kuwasilisha
Bungeni Muswada wa Sheria wa kuondoa jambo hili katikati ya mchakato
huu, ingeweza kuzua matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tungeulizwa haraka
ni ya nini tungeweza kukosa majibu.
Hatimaye
wakati wake wa kulimaliza suala hili sasa umefika. Misemo ya wahenga
ya “subira yavuta heri” na “kawia ufike” imetuongoza vyema tumefika
mahali tunaweza kufanya hivyo. Zipo sababu mbili zilizotushawishi kuamua
kuitoa rasilimali hii kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Kwanza
kwamba, siku hizi Serikali haiagizi mafuta. Kazi hiyo hufanywa na
makampuni binafsi. Pili, kwamba, rasilimali ya mafuta na gesi
yakipatikana Zanzibar ni suala la kiuchumi ambalo lipo kwenye mamlaka ya
Zanzibar kama ilivyo karafuu, hiliki, mwani na kadhalika. Au kama
ilivyo dhahabu, gesi, pamba, kahawa na kadhalika kwa upande wa Tanzania
Bara. Hivyo, Zanzibar iachwe kumiliki rasilimali yake ya kiuchumi.
Zanzibar na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo
lingine muhimu ambalo Serikali zetu mbili zimelizungumza na kukubaliana
tulitafutie ufumbuzi ni kuhusu Zanzibar kupata fursa ya kujiunga na
mashirika ya kimataifa, kukopa na kupata misaada kutoka nchi za nje bila
kizuizi. Kwa sasa fursa hiyo ina vikwazo vya namna mbalimbali. Ni
ukweli usiopingika kuwa jambo hili limechangia kwa kiasi kikubwa kujenga
hisia hasi kuhusu Muungano kwa upande wa Zanzibar. Aidha, limechangia
sana kuchafua hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar kwa nyakati mbalimbali.
Hata zile kauli kwamba Tanzania Bara imejificha kwenye koti la Serikali
ya Muungano, na kutaka itoke ionekane ili iache kunufaika isivyostahili,
zinazochangiwa sana na mazingira haya iliyonayo Zanzibar. Serikali zetu
mbili zinaamini kuwa mambo haya yakipatiwa ufumbuzi tutakuwa tumeondoa
kizingiti kikubwa katika ustawi wa Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar tumekubaliana kuwa, tutumie fursa za mchakato huu kuyamaliza
mambo haya yaishe! Bahati nzuri dhana iliyopo katika Ibara ya 65(2) ya
Rasimu inatoa jawabu mwafaka kwa tatizo hili. Tukikubaliana, itaipa
Zanzibar “uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano na ushirikiano na jumuiya
au taasisi yo yote ya kikanda na kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya
mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi” bila kizuizi. Ni maoni ya
Serikali zetu mbili kuwa fursa hiyo inaweza kutolewa kwa Zanzibar bila
ya kulazimika kuwa na muundo wa Serikali tatu. Hatuuoni ulazima huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
maoni yangu kitu kingine muhimu cha kufanya ni kuongeza msukumo,
utakaohakikisha kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha inatimiza ipasavyo majukumu
yake. Wanaohusika na utekelezaji wa maamuzi yake wabanwe ipasavyo
kutimiza wajibu wao. Iwekwe mifumo na masharti katika sheria au Katiba
ya kuwabana watekelezaji kwa ajili hiyo. Hali kadhalika ihakikishwe
kuwa, Akaunti ya Pamoja inaanzishwa bila ajizi na kutumika na pande
zote. Aidha, mfumo wa mawasiliano na ushirikiano baina ya Serikali zetu
mbili yaani Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya kisheria na kama hapana budi upewe
nguvu ya Kikatiba. Tukifanya hivyo tutafanikiwa kuyaweka mambo yote
sawa hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Katika
mjadala kuhusu mapendekezo ya kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali
tatu, wananchi wametoa maoni na mapendekezo mengi mazuri kuhusu
changamoto za Serikali tatu zilizoainishwa na Tume na namna ya
kuzitatua. Tena yapo maoni ya watu wanaopenda muundo wa Serikali tatu
na wasiopenda muundo wa Serikali tatu. Nawaomba myatafakari kwa uzito
unaostahili. Yapo mambo muhimu ya kuyatafutia ufumbuzi. Kwanza, kwa
mfano ni ile hoja kwamba Serikali ya Muungano inayopendekezwa
haikujengeka kwenye msingi imara. Haina nguvu yake yenyewe za kusimama.
Inategemea mno ihsani ya nchi washirika. Kwa sababu hiyo inaweza
kuanguka wakati wowote, na Muungano kusambaratika, iwapo itakosa ihsani
ya nchi washirika. Tena inaweza kuwa hivyo hata kama ni mmoja wa
washirika amefanya hivyo.
Pili,
kwamba, haielekei Serikali hiyo ina chanzo cha uhakika cha mapato ya
kuiwezesha kusimama yenyewe na kutekeleza majukumu yake. Ushuru wa
bidhaa unaopendekezwa unatiliwa shaka kuwa hautatosheleza mahitaji.
Pia, kwamba, hakuna uhakika wa fedha hizo kupatikana kwa vile, Serikali
ya Muungano haina chombo chake chenyewe cha kukusanya mapato hayo.
Itategemea vyombo vya nchi washirika kuikusanyia na kuipelekea. Kuna
hatari ya shughuli za Serikali ya Muungano kusimama wakati wo wote au
hata kusimama kabisa kwa sababu ya nchi washirika kuchelewa au kushindwa
kuwasilisha makusanyo ya kutoka kwao.
Bahati
mbaya Serikali ya Muungano haina uwezo wala nyenzo za kuhakikisha kuwa
mapato yake yanawasilishwa. Serikali hiyo haina mamlaka ya kuzibana
nchi washirika kuwasilisha au kuziwajibisha zisipofanya hivyo. Katika
mazingira hayo ni rahisi kwa Serikali ya Muungano kukwama na kushindwa
kutekeleza majukumu yake. Huu ni muundo ambao inakuwa ni rahisi sana
kwa Muungano kuvunjika.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano inapewa fursa ya kukopa kama
chanzo cha kujipatia mapato ya kuendesha shughuli zake. Lakini, kwa
sababu ya kukosa rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa vigumu kwa
Serikali hiyo kukopesheka. Kwa jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake
hauna nguvu iliyo thabiti, na watu wengine wanaona kama vile ukuu huo
haupo kabisa. Akitokea kiongozi ye yote wa nchi washirika akatunisha
misuli dhidi ya Rais wa Muungano au kupinga maamuzi ya Serikali au
chombo cha Muungano, Rais na Serikali yake watakuwa hawana lo lote la
kufanya. Kwa kweli uhai wa Muungano katika muundo wa Serikali tatu ni
wa mashaka makubwa.
Hofu
hizi kuhusu udhaifu wa Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa Serikali
tatu unaopendekezwa, zinawasumbua hata wale wanaopendelea mfumo wa
Serikali tatu kuwepo. Wao wangependa iwepo Serikali ya Muungano yenye
nguvu na inayoweza kusimama yenyewe kwa kujitegemea. Wanaona
kilichopendekezwa hakitoi matumaini hayo. Hii ina maana kuwa lazima
mawazo bora zaidi yatolewe ili kupata Serikali ya tatu yenye ukuu
unaoonekana na inayoweza kusimama yenyewe bila kuwa tegemezi na egemezi
kwa nchi washirika. Pia inaweza kuwa nguzo ya kutegemewa na nchi
washirika. Bila ya shaka Bunge hili likiamua tufuate mfumo huo linaweza
kuonyesha njia ya kuondoa hofu hizo. Kwa waumini wa Serikali mbili
wanaona kuwa huu ni uthibitisho wa ubora wa muundo wa Serikali mbili.
Changamoto za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
kuainisha changamoto za muundo wa Serikali tatu, Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imeyataja mambo mengine mawili makubwa ambayo ningependa
Waheshimiwa Wajumbe muyape tafakuri stahiki. Mambo hayo ni mosi,
misuguano na mikwamo (deadlocks and paralysis) katika kujadili na kufanya uamuzi kuhusu mambo muhimu ya Muungano. Na pili, ni kuibuka kwa hisia za utaifa (nationalistic sentiments)
wa zamani kwa nchi washirika. Nawaomba myatafakari kwa makini sana
mambo haya, kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu
ustawi na uhai wa Muungano, bali hata usalama wa raia na mali zao.
Naona hata Tume haikuweza kupata ufumbuzi ulio mwafaka kabisa kwa
changamoto hizi. Bila ya shaka katika mijadala yenu Waheshimiwa Wajumbe
mnaweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni
lazima lifanyike kila linalowezekana kuhakikisha kuwa maamuzi hayakwami
kwani yakikwama maana yake shughuli za Muungano zitakuwa zimekwama.
Kama hazitakwamuliwa kwa wakati ustawi wa Muungano utaathirika.
Ikishindikana kabisa kupatikana ufumbuzi Muungano unaweza kuvunjika.
Kuibuka na kukua kwa hisia za utaifa (nationalistic feelings) kwa
nchi washirika, yaani Utanganyika na Uzanzibari ni tishio kubwa sana
kwa uhai wa Muungano. Hebu fikiria, watu walioishi pamoja kidugu na kwa
kushirikiana, kama watu wamoja na raia wa nchi moja yaani Watanzania
kwa miaka 50, kuja kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya Watanganyika na
Wazanzibari na siyo kati ya Watanznaia. Kwa mujibu wa sensa iliyopita
takriban asilimia 90 ya Watanzania waliopo sasa wamezaliwa baada ya
mwaka 1964. Nchi wanayoijua ni Tanzania. Litakuwa ni jambo lenye
mshtuko mkubwa na athari zisizoweza kutabirika, watu hao watakapojikuta
ni wageni wanaotakiwa kutengenezewa utaratibu maalum wa kusafiri na
kuishi wakiwa upande wa Muungano ambao siyo kwao kwa asili. Wanakuwa
wageni na fursa walizokuwa wanazipata waendapo popote haiwi rahisi tena
kuzipata.
Katika
mazingira hayo ni rahisi sana chuki kupandikizwa na watu waliokuwa
ndugu mara moja watajikuta maadui. Aidha, watu wanaweza kujikuta
wakilazimika kurudi kwao kwa asili ama kwa kufukuzwa au kwa sababu ya
mazingira kuwa magumu kiasi cha kuona bora waondoke. Watu hao wanaweza
kulazimika kuondoka huku wakiacha nyuma kila kitu walichokichuma
maishani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Changamoto
hizi kubwa mbili za mfumo wa Serikali tatu ambazo Tume imeziona, ni za
kweli. Si mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta watu wenye asili ya
Tanzania Bara ya kuchomewa moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012 na watu
wenye hisia kali za Uzanzibari, na kuwataka watu wa Bara waondoke
Zanzibar, huenda yakawa madogo. Matukio ya namna hii yanaweza kutokea
pande zote mbili na kusababisha maafa makubwa. Itaanza baina ya watu,
baadaye itakuwa baina ya Serikali zetu mbili na kuzifikisha nchi zetu
mbili zilizokuwa ndugu na rafiki, kwa nusu karne, ghafla kuwa maadui
wasioombana chumvi na wasiotakiana heri. Umoja wetu utatetereka na
Muungano wetu unaweza kuvunjika. Kwa nini tufike huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sisi
viongozi tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba ya wananchi wetu, hatuna
budi kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa ili tufanye uamuzi ulio
sahihi. Tusije tukajutia uamuzi wetu tutakapoona watu wanafukuzana,
wanauana na mali zao kuporwa. Na, tukifikia hatua hiyo Muungano
kusambaratika halitakuwa jambo la ajabu.
Kwa
kweli, unapoyatafakari haya, ni rahisi kuelewa kwa nini wazee wetu
waasisi waliamua walivyoamua. Waliona mbali. Tusipuuze fikra zao na
maono yao. Kuna hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza kila kitu
tulichokijenga kwa miaka 50. Badala ya kujenga tunaweza kujikuta
tumebomoa hata msingi katika nchi washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere mwaka 1993 alituasa kuhusu hatari hiyo: “Hamuwezi kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu… na adhabu nyingine zimo mle mle ndani ya kitendo hazisubiri.”
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Siku moja kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini aliniuliza: “Hivi
Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu ni kuongeza ya tatu? Si
matatizo ndiyo yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu
si kila mtu atachukua njia yake? Mtakuwa mmepoteza kila kitu. Mimi
nawashauri msichoke kutafuta majawabu kwa matatizo ya hizi mbili! Huko
mnakotaka kwenda kuna hatari nyingi”.
Pengine na ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Kazi Yenu Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mambo
ya kuyasemea ni mengi mno lakini kwa sababu ya ufinyu wa muda,
nisingeweza kuyazungumzia yote. Naamini, mtayaona katika kuipitia
Rasimu na kwenye majadiliano yenu. Napenda kusisitiza kwenu kuwa kazi
iliyo mbele yenu ni kubwa sana. Ni kubwa kwa maana mbili. Kwanza,
jukumu lenyewe la kutunga Katiba ya nchi ni zito sana. Taswira ya nchi
yetu itakuwaje na itaendeshwa vipi kwa miaka mingi ijayo iko mikononi
mwenu. Ipeni nchi yetu hatima njema. Pili, ni kubwa kwa maana ya uzito
wa mambo ya kujadili na kuyafanyia uamuzi. Kwa ajili hiyo, ni muhimu
sana kuisoma Rasimu na Taarifa ya Tume kwa makini na kuzielewa. Jipeni
muda wa kutafakari kila neno, kila sentensi, na kila dhana ili muweze
kufanya uamuzi ulio sahihi. Mkifanya hayo mtakuwa mmeisaidia nchi yetu
na Watanzania wote kupata Katiba nzuri.
Nimefarijika
sana kusikia kuwa mtajigawa kwenye Kamati 12 wakati wa kujadili
Rasimu. Huu ni utaratibu mzuri kwani mkiwa katika vikundi vya watu
wachache, mtakuwa na mijadala ya kina zaidi. Watu wote wanaweza kupata
fursa ya kutoa maoni yao, kwa kila kifungu na kila jambo linaloibuliwa
na kuzungumzwa. Kwa kufanya hivyo, mtatimiza kwa ukamilifu jukumu lenu
la kutunga Katiba. Wote mtakuwa mmeshiriki kujadili kila sura na
vipengele vyake vyote. Mkimaliza kazi yenu mtapokea kwa haki sifa nzuri
kama Katiba itakuwa nzuri, au lawama stahiki iwapo itakuwa kinyume
chake.
Pongezi kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama nitamaliza hotuba yangu bila ya kutambua kazi
nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza
la Wawakilishi, alipokuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hili. Kazi yake
haikuwa rahisi hata kidogo, lakini kwa umahiri na ustadi mkubwa ameweza
kufanikisha mambo kwa kiasi ambacho anastahili pongezi zetu sote.
Anastahili pongezi kwa sababu yeye aliendesha Bunge hili bila ya kuwepo
kwa kanuni. Tatizo hili hatakuwa nalo Mwenyekiti wa Kudumu kaka yangu
Mheshimiwa Samuel Sitta.
Napenda
pia kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa hatua
mliyofikia. Hata hivyo, mmechukua muda mwingi katika hatua ya awali
hivyo hamna budi kuongeza kasi. Naomba niwakumbushe kuwa mijadala yenu
hii inafuatiliwa kwa karibu sana na Watanzania. Wamewekeza sana
matarajio yao kwenu. Hamna budi, haiba na taswira ya uongozi muionyeshe
wakati wote wa kuendesha mijadala yenu kwa lugha na vitendo vyenu.
Wakati wa semina na mjadala wa kupitisha Kanuni za Bunge hili, baadhi ya
wananchi wamekwazika sana na mwenendo wa baadhi ya Wajumbe.
Hawakutegemea kuyaona matendo waliyoyaona mkifanya na kusikia maneno
waliyoyasikia kutoka kwenye vinywa vya baadhi yenu.
Ni
matumaini yangu na ya Watanzania wote kuwa hali ile haitajirudia tena
katika awamu hii. Tusiwafikishe mahali Watanzania wakakata tamaa na
Wajumbe wao au na hata chombo hiki muhimu sana kwa mustakabali wao na wa
nchi yao. Tutoe hoja badala ya kupiga kelele (argue don’t shout) au
kuzomea. Hakuna haja ya kutumia lugha isiyokuwa ya staha katika
kujieleza. Hakuna haja ya kukingiana ngumi, kutishiana hili na lile au
hata kugombana. Ni utovu wa uungwana usiotegemewa kutoka kwenu.
Tusiwaangushe wananchi wa Tanzania wanaotutegemea sana.
Wekeni Maslahi ya Taifa Mbele
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ombi
langu la mwisho kwenu ni kuwasihi kuwa wakati wote muongozwe na kujali
maslahi mapana ya nchi yetu na watu wake badala ya kujali maslahi yenu
binafsi au ya makundi yenu. Naomba kaulimbiu yenu iwe “Tanzania
Kwanza”. Najua kila mmoja wenu amekuja na maoni yake au atakuwa nayo
kwa kila jambo litakalojadiliwa. Wengine wamepewa misimamo na vyama
vyao au makundi yao. Si jambo baya na ni hatua muhimu ya kuleta
mafanikio, kama misimamo hiyo na mawazo hayo ni ya kujenga.
Hata
hivyo, mnachotegemewa kufanya ni kuwa tayari kuwianisha na kuunganisha
mawazo yenu mazuri na ya wenzenu, ili kupata msimamo wa pamoja na uamuzi
wa pamoja ulio bora. Kwa sababu hiyo, hamna budi kuwa tayari
kusikiliza mawazo ya wengine, hata kama ni tofauti na yenu mliyokuja
nayo. Tafuteni kilicho chema kwa yale yanayosemwa na watu wengine hata
kama ni watu usiokubaliana nao au huwapendi au hampendani. Kunaweza
kuwepo kitu chenye manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Nawaomba
muwe hodari wa kushawishi badala ya kulazimisha. Mkifanya hivyo
hamtalazimika kutumia muda mwingi wa kula njama za namna ya kuwazidi
maarifa wale mnaotofautiana nao kwa mawazo. Lazima pia mtafute namna ya
kushirikiana na kuwasiliana na makundi mengine. Msitafute kushindana,
hili ni jambo ambalo lazima wote mtoke hapa mkiwa washindi. Yaani
lazima Watanzania wote washinde kwani wao ndiyo wenye Katiba yao.
Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa na asasi mbalimbali kwa
kutambua na kuthamini umuhimu wa kuwa na taratibu za mawasiliano,
mashauriano na ushirikiano. Daima muwe watu wa kutafuta maridhiano.
Mmefanya vizuri katika hatua ya awali. Mmejiwekea taratibu nzuri za
kufanya hayo, tafadhalini zitumieni. Jengeni madaraja imara zaidi
katika awamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Naomba
nimalize kwa kuwaomba Watanzania wote tukiongozwa na viongozi wetu wa
dini tumuombe Mola wetu ajalie rehema zake ili mchakato wa kutunga
Katiba uende salama. Aliongoze Bunge hili na Wajumbe wake waweze
kufanya uamuzi ulio sahihi na wenye manufaa kwa taifa letu kwa kila
watakaloliamua.
Baada
ya kusema maneno yangu mengi hayo, nirudie kukushukuru Mheshimiwa
Mwenyekiti kwa kunipa fursa hii adhimu ya kulihutubia Bunge Maalum la
Katiba. Nawatakieni kila la heri na mafanikio mema. Katiba Mpya
Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Libariki Bunge Maalumu la Katiba!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!
EmoticonEmoticon