January 02, 2014
WASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA KUKUTWA NA BUNDUKI AINA YA SHORT GUN.
JESHI  la Polisi Mkoa wa Tanga linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kukutwa na bunduki moja aina ya short gun pamoja na sare za jeshi la polisi ambazo zilikutumika katika matukio ya kiuhalifu wilayani Korogwe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,Constatine Massawe ameiambia TANGA RAHA BLOG  kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Desemba 28 mwaka jana majira ya saa nne usiku katika eneo la kambi ya Mkonge ya Gomba kata ya Makuyuni Tarafa ya Mombo.

Massawe alisema watuhumiwa hao walikuwa wakiitumia bunduki hiyo yenye namba za usajili 807028 ikiwa na risasi tatu na ganda moja ambapo ilikuwa katika harakata za kufanyia uhalifu katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Aliwataja majina ya watuhumiwa hao kuwa Zakaria Jelas(50),Moses Jonas(44),Selemani Hassani (21),Taratibu Hemed (74) na Hemed Taratibu(32) wote wakazi wa Makanya wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Aidha Kamanda Massawe alisema baada ya upekuzi watuhumiwa hao walikamatwa na sare mbili mali ya Jeshi la Polisi Tanzania  ambapo katika mahojiano na Jeshi hilo watuhumiwa hao walikiri kuhusika na matukio mbalimbali ya unyang’anyi na utekaji wa magari barabarani.

Katika tukio lengine,Jeshi la Polisi Mkoani Tanga linawashikilia wakazi watatu kwa kupatikana na mali inayodhaniwa kuwa ni mali wizi katika kuzuizi cha Polisi kilichopo Kijiji Kwasunga kata ya Makuyuni Tarafa ya Mombo wilayani Korogwe.

Kamanda Massawe alisema tukio hilo lilitokea Desemba 31 majira ya saa sita mchana baada ya watuhumiwa hao kufika kwenye kizuizi hicho wakiwa na pikipiki mbili za wizi ambazo ziliibiwa Kariakoo Jijini Dar es Salaam.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Jackson Aloyce (25), Leonard Fredick(21) wakiwa na pikipiki yenye namba za usajili T.274 CQV aina ya Boxer rangi ya blue na Karist Adolf (22)akiwa na pikipiki yenye namba T.162 CKL aina ya Boxer rangi nyeusi  ambapo watuhumiwa hao wote ni wakazi wa Dar es Salaam.

Hata hivyo alisema katika mahojiano na polisi watuhumiwa hao walikiri kutenda kosa hilo  maeneo ya Kariakoo mkoani Dar es Salaam na wanashikiliwa na jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »