TFF YAISHAURI WILAYA YA HANDENI JUU YA UWANJA WA AZIMIO ULIOPO MJINI HUMO

January 09, 2014

 Msemaji wa TFF, Boniface Wambura, pichani.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF), limesema ili Uwanja uweze kutumiwa katika mechi za Ligi Kuu unahitajika kuandaliwa vizuri, ikiwa ni pamoja na kuwa na eneo zuri la kuchezea, uzio na maeneo ya kukaa kwa mashabiki na wahusika wengine.

Maneno ya TFF yanaweza kuwa majibu kwa Wilaya ya Handeni inayojipanga kuhakikisha uwanja wao wa Azimio uliyopo wilayani humo unaweza kutumiwa katika mechi za ligi kuu, kwa kupitia timu ya Mgambo Shooting yenye maskani yake Kabuku wilayani Handeni.
Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita, Msemaji wa TFF, Boniface Wambura, alisema kwamba kuwa na timu inayoshiriki ligi kuu ni jambo moja na uwanja uliopo kwenye timu hiyo kutumika ni jambo jingine, hivyo ni wakati wa kuukarabati uwanja huo.
 
“Hata kama si uwanja huo kutumiwa kwenye ligi kuu, bado unaweza kuingizwa kwenye programu ya ligi daraja la kwanza na mashindano mengine, lakini hadi uwe kwenye mazingira mazuri.
 
“Uwanja wowote lazima uwe katika kiwango kizuri kama vile sehemu ya kuchezeaa, vyoo, uzio, majukwaa na mengineyo ya msingi, hivyo kama baadhi yake kwenye uwanja huo hakuna ni jukumu la kuweka mipango kuuweka sawa,” alisema Wambura.
 
Katikati ya mwezi Desemba, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Thomas Mzinga, alizungumzia hamu ya kuona uwanja wao unatumiwa katika mechi mbalimbali zenye ushindani, zikiwapo timu za Simba na Yanga.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »