Rais Kikwete atimiza ahadi yake ya kujenga daraja la Mwanhuzi wilayani Meatu

November 30, 2013



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiongozwa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kukagua daraja la Mwanhuzi lililoko Meatu Mkoani Simiyu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiongozwa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kukagua daraja la Mwanhuzi lililoko Meatu Mkoani Simiyu.


Muonekano wa Daraja la Mwanhuzi.

Ahadi ya ujenzi wa daraja la Mwanhuzi katika wilaya ya Meatu mkoani Simiyu imetimia baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete kulifungua rasmi daraja hilo ambalo ujenzi wake umekamilika na tayari limeanza hutumika.

Awali kabla ya kulifungua daraja hilo Rais Kikwete aliwaasa wananchi wa eneo hilo la Mwanhunzi pamoja na watumiaji wengine kulitunza daraja hilo ili liweze kudumu kwa muda uliokusudiwa na hivyo kuhakikisha panakuwepo huduma hiyo muhimu ya usafiri kati ya Wilaya ya Meatu na Mikoa ya jirani ya Arusha na Singida.


‘Ninawasihi mlitunze daraja hili na asije akatokea mtu kwenda kuanza kukata vyuma au kunyofoa vifaa vingine vya daraja kwani kwa kufanya hivyo mtalidhoofisha ubora wake na hatimaye kuharibika kabisa tukajikuta tunarusi katika kero ya usafiri katika eneo hili kama ilivyokuwa hapo awali kabla ya kujengwa kwa daraja” Alisisitiza Rais kikwete .

Aidha, Mhe. Rais aliongeza kuwa atahakikisha katika kipindi cha miaka miwili kilichobakia akishirikiana na Waziri Magufuli watahakikisha wanafikisha sehemu nzuri ahadi zote za miradi ya barabara katika wilaya hiyo na mkoa wa Simuyu kwa ujumla.

Daraja la hilo lenye urefu wa meta 40 ni kiungo muhimu cha usafiri kuvuka mto Mwanhuzi ambako barabara kuu inayo tokea Kolandoto mkoani Shinyanga kupitia Lalago katika mkoa wa Simiyu na kuelekea mikoa ya Singida na Arusha.

Awali wakati akimkaribisha Rais, Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alielezea kuwa usanifu pamoja na usimamizi wa daraja hilo umefanywa na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kwa gharama ya Shilingi milioni 13.45 na ujenzi wake umetekelezwa kwa awamu mbili.

”Kukamilika kwa mradi huu ni moja ya ushahidi unaothibitisha kuwa ahadi ulizotoa kwa wananchi zinakamilika popote bila kuangalia itikadi za vyama au watu” alisema Waziri Magufuli

Waziri Magufuli alifafanua kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa daraja hilo ilikamilika mwezi Agosti mwaka 2013 ikiwa imejengwa na Mkandarasi M/S Pet Cooperation kutoka Kahama kwa gharama ya Shilingi milioni 355.58.

Awamu ya pili ya mradi huu ambazo zilianza mwezi Agosti 2013 na kukamilika nwezi Oktoba 2013 zilijumuisha ujenzi wa kingo za daraja. Kazi hizo zillitekelezwa chini ya usimamizi wa Ofisi ya Meneja wa Tanroads mkoa wa Simiyu mara baada ya mkoa huo mpya kuanzishwa. Awamu hii ya pili ilitekelezwa na Kampuni ya Ms Tolerance Engineering Ltd ya Dar es Salaam kwa gharama ya Shilingi milioni 97.55.

Fedha hizo zote zilizotumika katika ujenzi wa awamu zote mbili pamoja na usimamizi ambazo ni jumla ya Shilingi milioni 455.58 zimetolewa na Mfuko wa Barabara (Roads Fund).

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »